PWANI-Mkaguzi wa Polisi Anna Mawala, Msimamizi wa Dawati la Jinsia na Watoto wilayani Kibaha Mkoa wa Pwani, Agosti 15, 2026 amewataka wazazi kudhibiti utoro wa wanafunzi shuleni.
Hayo yamesemwa katika kikao cha wazazi na uongozi katika shule ya Sekondari Msangani Government pamoja na Polisi Kata, ambapo Mkaguzi Mawala amewataka wazazi kufatilia nyendo za watoto wao na makundi wanayojumuika nayo ili kujua ni ya aina gani.
"Wazazi wengi wamekuwa wavivu kufatilia maendeleo ya watoto wao na kuwaachia jukumu waalimu peke yao, kitendo ambacho kinawapa mwanya wanafunzi kujiunga na makundi mabaya yanayopelekea mmonyoka wa maadili kwakukosa Usimamizi sahihi toka nyumbani, wazazi wengi wamekuwa na madai ya utafutaji wa kipato kwa muda mwingi zaidi na kushindwa kuwafatilia watoto wao,"amesema Mawala.
Kupitia kikao hicho kilichojumuisha wazazi, walezi, uongozi wa shule pamoja na Polisi Kata wameeazimia kuungana kwa pamoja ili kutokomeza utoro mashuleni ndani ya Kata ya Msanagani na kuboresha taaluma na kupandisha ufaulu kwa kuwafatilia wanafunzi wote kuanzia nyumbani, mtaani na shuleni.
