BoT yahimiza matumizi sahihi ya sarafu na noti, yaonya vikali michezo ya upatu nchini

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi kuboresha utunzaji na matumizi ya noti na sarafu, huku ikiwasihi wasanii na watengeneza maudhui kutumia ushawishi wao kuelimisha jamii kuhusu matumizi sahihi ya fedha na huduma salama za kifedha nchini.
Wito huo umetolewa leo Agosti 31,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa semina ya elimu ya fedha iliyoandaliwa na BoT na kuwashirikisha wasanii wa muziki, waigizaji,watengeneza maudhui na washereheshaji mbalimbali wenye ushawishi katika jamii.

Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tafiti na Uchumi wa BoT, Dkt.Suleiman Misango amesema, wasanii ni kundi muhimu katika kufikisha elimu ya fedha kwa umma kutokana na ushawishi mkubwa walionao kupitia majukwaa mbalimbali.

“Tumekuwa tukifanya kazi hii kwenye maonesho na matukio mbalimbali, lakini tumeona wadau hawa wanaweza kutusaidia kufikisha elimu kwa jamii kwa njia bora zaidi."

Dkt.Misango amesema,ushirikishwaji wa wasanii na watengeneza maudhui ni sehemu ya mkakati wa BoT wa kupanua wigo wa elimu ya fedha kwa kutumia majukwaa yanayowafikia wananchi wengi na kuchochea mabadiliko chanya ya tabia katika matumizi ya fedha.

Vilevile,Dkt.Misango amesema,utunzaji usio sahihi wa noti husababisha kuchakaa na kuharibika kwa haraka, jambo linalolazimisha Benki Kuu kuziondoa katika mzunguko na kuingiza nyingine badala yake.

Amesema,mchakato huo una gharama zinazohusisha uchapishaji, usafirishaji, usambazaji na uingizwaji wa noti mpya katika mzunguko wa fedha.

Dkt.Misango amewataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuzitunza fedha taslimu na maeneo safi ili kuongeza muda wa noti na sarafu kutumika katika shughuli za kiuchumi.

“Utunzaji wenye uwajibikaji wa noti unasaidia shughuli za kiuchumi huku ukipunguza gharama zinazohusiana na uchapishaji na usambazaji wa fedha,”amesema.

Amefafanua kuwa,BoT hufuatilia muda ambao noti hukaa katika mzunguko wa fedha kabla ya kuchakaa na kurejea katika mfumo wa kibenki kwa ajili ya kubadilishwa.
Kwa mujibu wa Dkt.Misango, muda wa matumizi ya noti unaweza kutofautiana kulingana na mazingira ya matumizi, ikiwemo tofauti kati ya maeneo ya mijini na vijijini.

Amesema,kupungua kwa muda wa noti kukaa katika mzunguko kuliko ilivyotarajiwa kunaweza kuwa kiashiria cha matumizi au utunzaji usio sahihi.

BoT pia imewataka wananchi kutumia zaidi mifumo ya kielektroniki katika kuhamisha fedha, hasa katika miamala yenye thamani kubwa ambayo haihitaji matumizi ya fedha taslimu.

Dkt.Misango amesema,baadhi ya desturi katika hafla za kijamii, ikiwemo kutoa zawadi kubwa kwa fedha taslimu zinaweza kubadilishwa kwa kutumia huduma za benki.

Ametoa mfano wa mtu anayepanga kutoa zawadi ya Shilingi milioni 100, akisema si lazima kubeba kiasi hicho cha fedha taslimu kwenda kwenye sherehe, bali fedha hizo zinaweza kuhamishwa moja kwa moja kwenye akaunti ya anayetarajiwa kuzipokea.

Mkurugenzi huyo amesema, matumizi ya mifumo ya kidijitali yanaweza kurahisisha miamala kwa wananchi na wakati huohuo kupunguza utegemezi wa fedha taslimu, jambo linaloweza kusaidia kupunguza mahitaji ya kuchapisha na kusambaza noti mbadala.

BoT yaonya ukopeshaji holela na upatu

Katika semina hiyo, BoT pia imewaonya wananchi wakiwemo wasanii, kujiepusha na biashara ya ukopeshaji fedha au ukusanyaji wa amana kutoka kwa wananchi kupitia mifumo isiyosajiliwa na mamlaka husika.

Akiwasilisha mada kuhusu Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018, Afisa wa BoT kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha,Bi.Joseph Lubava amesema, mtu au taasisi inayofanya biashara ya huduma ndogo za fedha bila kuwa na leseni halali kutoka BoT inakiuka sheria.
Pia, amesema ukiukwaji huo unaweza kusababisha hatua za kisheria, zikiwemo adhabu za kifedha na kifungo, pamoja na hatua nyingine za kiutawala kwa mujibu wa sheria.

Lubava amesema,BoT pia inaweza kuchukua hatua dhidi ya shughuli zinazofanyika kinyume cha sheria, ikiwemo kuzifunga na kuchukua hatua nyingine zinazotambuliwa kisheria.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuhakiki uhalali wa taasisi za kifedha kabla ya kuingia katika miamala au mikataba ya kifedha.

Chunguzeni watoa mikopo

Lubava amewataka wananchi wanaohitaji mikopo kuhakikisha kwanza kwamba taasisi wanayotaka kukopa ina leseni halali na inasimamiwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema, ni muhimu pia kwa mkopaji kusoma na kuelewa mkataba wa mkopo kabla ya kuusaini, akitaja mambo muhimu ya kuangalia kuwa ni pamoja na kiwango cha riba, tozo, gharama nyingine na masharti ya urejeshaji wa mkopo.

Amesema, hatua hiyo inaweza kusaidia kupunguza migogoro inayoweza kujitokeza kutokana na wananchi kuingia katika mikataba bila kuelewa kikamilifu wajibu na gharama zinazohusika.

Lubava pia amewasihi wasanii kutumia umaarufu wao kwa manufaa ya jamii, hasa katika kueneza elimu sahihi kuhusu huduma za fedha, badala ya kusambaza taarifa zinazoweza kupotosha wananchi.

Amesema, wasanii wana uwezo wa kufikisha ujumbe kwa watu wengi zaidi ndani na nje ya nchi.

Ameongeza kuwa,wananchi wenye changamoto au malalamiko kuhusu huduma za kifedha wanapaswa kutumia mifumo na dawati la malalamiko la BoT ili kupata msaada au ufafanuzi kwa wakati.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA), Edward Buganga ameishukuru BoT kwa kuwaandalia wasanii mafunzo hayo na kuwataka kutumia maarifa waliyoyapata kwa manufaa ya jamii.

Buganga amewasihi wasanii kuwa mabalozi wa elimu ya fedha kwa kufikisha ujumbe kwa wananchi kupitia shughuli zao, majukwaa ya kijamii na maeneo mengine wanayofanya kazi.

Amesema,ushirikiano kati ya taasisi za umma na sekta ya ubunifu unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya uchumi na fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here