Wasanii waahidi kulinda thamani na heshima ya Shilingi ya Tanzania

NA GODFREY NNKO

WASANII nchini wameahidi kutumia nafasi yao kama kioo cha jamii kuhamasisha na kuelimisha wananchi kuhusu matumizi sahihi ya fedha, hususan utunzaji na matumizi yanayolenga kulinda thamani na heshima ya Shilingi ya Tanzania.
Rais wa Shirikisho la Sanaa za Maonesho Tanzania (SHISAMA), Dkt.Cynthia Patrick Henjewele ameyasema hayo leo Agosti 31,2026 wakati akiishukuru Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuwaandalia wasanii semina kuhusu elimu ya fedha jijini Dar es Salaam.

Dkt. Henjewele amesema,semina hiyo imewapa wasanii uelewa mpana kuhusu masuala ya fedha, huku akieleza kuwa wamefurahishwa zaidi na ombi la BoT la kuwashirikisha kama mabalozi wa kueneza elimu hiyo kwa wananchi.

“Tumefurahia zaidi kwa kututuma kuwa mabalozi wenu. Kikubwa kabisa, sisi vyama vya shirikisho kutoka BASATA tuko tayari kufanya kazi na kupeleka elimu hii Tanzania nzima, kwa maana vyama na mashirikisho yetu ni ya Tanzania nzima,”amesema.
Amesema,elimu ya fedha ni muhimu kwa wasanii kutokana na changamoto ya usimamizi na matumizi yasiyo sahihi ya fedha ambayo imekuwa ikilalamikiwa katika jamii.

Akitoa mfano wa uzoefu wake binafsi, Dkt. Henjewele amesema,amepata uelewa mpya kuhusu matumizi ya fedha katika shughuli za sanaa na sherehe, ikiwemo kitendo cha kupamba fedha, ambacho alisema hakujua awali kuwa ni kosa.

“Elimu kubwa inahitajika na sisi wasanii tunapaswa kushiriki ipasavyo kuhakikisha tunatoa elimu hiyo,”amesema.

BASATA

Kwa upande wake, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA),Edward Buganga amesema,semina hiyo iliyoandaliwa na BoT ni muhimu kwa wasanii kwa kuwa imewapa uelewa mpana kuhusu masuala ya fedha, maarifa ambayo bila ushiriki wa Benki Kuu yasingekuwa rahisi kuyapata kwa kiwango hicho.
Amesema,elimu hiyo inapaswa kutazamwa zaidi ya maarifa binafsi, kwa kuwa fedha ni sehemu muhimu ya uchumi na ustawi wa Taifa, hivyo kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha inatunzwa na kutumiwa kwa usahihi.

“Tumepata elimu ya fedha ambayo kimsingi inaitazama fedha kama tunu ya nchi. Kwa hiyo, tutumie nafasi hiyo kuhakikisha kwamba tunailinda na kuitunza fedha yetu ili iweze kuendelea kubaki salama,”amesema.

Aidha,amdwataka wasanii kutambua nafasi yao katika jamii na kuitumia kueneza elimu waliyoipata kutoka kwa wataalamu wa BoT.

Amesema,wasanii ni miongoni mwa watu wanaofuatiliwa kwa karibu na wananchi, hivyo wana nafasi kubwa ya kuathiri mitazamo na mienendo ya jamii.

“Wasanii ni kioo cha jamii, hivyo wanapaswa kutumia nafasi yao kuhakikisha elimu waliyoipata kutoka kwa maafisa wa Benki Kuu ya Tanzania wanaitumia na kuifikisha kwa wananchi ambao muda wote wamekuwa wakiwaangalia kama kioo cha jamii,”amesema.

Pia,amewataka wasanii wanaohusika na shughuli za burudani na urembo katika sherehe mbalimbali kuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya fedha.

Amesema,washereheshaji na wasanii wengine hushiriki katika matukio yanayohusisha matumizi na usambazaji wa fedha, hivyo wana nafasi ya kuhakikisha wananchi wanaelimishwa kuhusu namna sahihi ya kuitumia na kuitunza.
“Ni hili, kufikisha elimu sahihi ya matumizi sahihi ya sarafu. Mwisho,niwaombe tena wasanii, na nikirejea kwa wale washereheshaji, ninyi mmekuwa mbele sana kwenye matukio mbalimbali yanayohusu shughuli na sherehe mbalimbali,”amesema.

Amewataka wasanii hao kuwa mfano katika kuhakikisha fedha zinatumika kwa utaratibu unaostahili, hasa wakati wa sherehe ambapo wakati mwingine fedha hutumiwa kwa namna inayoweza kuathiri ubora na usalama wake.

“Niwaombe sana mkawe kielelezo cha kwanza cha kutoa elimu ya matumizi ya fedha wakati sherehe zikichangaya na watu wakianza kutunza. Mkatilie maanani jambo hilo ili angalau fedha zetu zitumike kwa usahihi,” amesema.

Kutokana na hali hiyo, ameiomba BoT na wadau wa sanaa kushirikiana kuweka utaratibu mzuri wa kushughulikia matumizi ya fedha katika sherehe na matukio mbalimbali bila kuathiri utunzaji na heshima ya Shilingi ya Tanzania.

Amesema,ushirikiano huo ni muhimu katika kuhakikisha shughuli za burudani na sherehe zinaendelea bila kuhatarisha utunzaji wa sarafu ya Taifa.

Bodi ya Filamu

Kwa upande wake, mwakilishi wa Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania ambaye pia ni Meneja wa Kitengo cha Uhakiki wa Filamu wa Bodi hiyo,Bi.Boppe Kyungu amesema, mafunzo hayo ni ya kipekee kwa kuwa ni mara ya kwanza BoT kuwakutanisha pamoja wadau hao wa sanaa na kuwapatia elimu kuhusu masuala ya fedha.

Amesema,hatua hiyo ni muhimu katika kujenga uelewa miongoni mwa wasanii ambao wana nafasi kubwa ya kufikisha ujumbe kwa jamii kupitia kazi zao.

Kyungu pia ameiomba BoT kuandaa mkakati mpana wa kuwafikia wasanii wengi zaidi pamoja na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha elimu ya fedha inawafikia watu wengi nchini.

Amesema,sekta ya filamu inaweza kuwa nyenzo muhimu katika kufikisha ujumbe huo kwa jamii kwa wakati mmoja kutokana na uwezo wake wa kuwafikia watu wengi kupitia maudhui ya kisanii.
“Kama tulivyosema, hawa ni kioo cha jamii. Pia ninaweza kusema kuwa filamu ndiyo nyenzo pekee ambayo inaweza kufikia jamii kubwa kwa wakati mmoja. Tutumie wasanii wetu hawa ambao wamefika leo na wengine ambao hawajafika leo waweze kufanya kazi nanyi kwa ajili ya kutengeneza filamu ambazo zitatoa ujumbe kwa jamii kupata elimu kwa wakati mmoja,”amesema.

Amesema, ushirikiano kati ya BoT na wadau wa sanaa unaweza kuongeza ufanisi katika utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi, huku kazi za sanaa zikitumika kama nyenzo ya mawasiliano yenye uwezo wa kufikisha ujumbe kwa hadhira pana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here