BoT yawataka wasanii kuwa mabalozi kuhusu utunzaji fedha

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wasanii na washereheshaji nchini kutumia ushawishi wao kwa jamii kuhamasisha wananchi kutunza na kutumia kwa usahihi noti na sarafu, ikieleza kuwa utunzaji wa fedha ni jukumu la kila mmoja.
Wito huo umetolewa leo Agosti 31,2026 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Tafiti na Uchumi wa BoT, Dkt. Suleiman Misango wakati akifungua semina maalum iliyowakutanisha wasanii wa muziki, waigizaji, watengeneza maudhui na washereheshaji mbalimbali wenye ushawishi katika jamii.

Dkt.Misango amesema,ushiriki wa wasanii katika kuelimisha jamii kuhusu matumizi na utunzaji sahihi wa fedha ni muhimu kutokana na nafasi yao kubwa katika jamii na uwezo wao wa kufikisha ujumbe kwa hadhira pana.

Amesema,wananchi wanapaswa kuelewa kuwa namna wanavyoshughulikia noti na sarafu ina mchango mkubwa katika kuhakikisha fedha hizo zinadumu katika mzunguko na kupunguza gharama zinazotokana na kuzibadilisha mara kwa mara.

“Jukumu la fedha ni la kila mmoja,” amesema Dkt. Misango, akisisitiza umuhimu wa wananchi kuwa waangalifu katika matumizi na utunzaji wa noti na sarafu wanazozitumia katika shughuli zao za kila siku.

Ameeleza kuwa,fedha zinapochanika, kuchafuka au kuharibika kutokana na kutotunzwa ipasavyo, huathiri matumizi yake katika mifumo mbalimbali ya malipo ikiwemo mashine za kutolea fedha (ATM).

Kwa mujibu wa Dkt. Misango, noti zilizochakaa au kuharibika zinaweza kusababisha changamoto katika utendaji wa baadhi ya mashine za ATM, hali inayoweza kuongeza gharama za uendeshaji na matengenezo kwa watoa huduma za kifedha.

“Hizi fedha, noti na sarafu usipozitunza vizuri, hata kwenye mashine hasa za ATM hazitoki vizuri, bila kujua kuwa unamuongezea gharama mtoa huduma wa fedha,benki. Hivyo, mwisho wa siku mnaweza kugawana gharama za kuhudumia mashine,”amesema.

Amesema suala la utunzaji wa fedha halipaswi kuangaliwa kama jukumu la Benki Kuu pekee, bali ni wajibu unaohitaji ushirikiano wa wananchi, taasisi za fedha na wadau wengine, wakiwemo wasanii wenye ushawishi mkubwa katika jamii.

Semina hiyo ni sehemu ya juhudi za Benki Kuu za kuongeza uelewa kwa wasanii na wadau wengine kuhusu masuala yanayohusu fedha, ikiwemo utunzaji sahihi wa noti na sarafu.

Aidha, BoT imewaelimisha kuhusu shughuli za kifedha zinazohitaji leseni,na madhara ya vitendo vya kukusanya amana kutoka kwa wananchi na kutoa mikopo bila kuwa na leseni kutoka Benki Kuu ya Tanzania.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa miongoni mwa wadau hao ili waweze kutambua mipaka ya shughuli za kifedha zinazoweza kufanywa na mtu au taasisi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.

Dkt.Misango pia amesisitiza kuwa, kuna manufaa mbalimbali ya kutunza fedha na kuzitumia kwa njia sahihi katika huduma na shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini.

Amesema,matumizi sahihi ya fedha, pamoja na utunzaji wake, yana umuhimu katika kuimarisha mifumo ya malipo na kuhakikisha fedha zinaendelea kutumika kwa ufanisi katika shughuli za kila siku za wananchi.

Kwa nafasi yao ya kuwa na ushawishi mkubwa kupitia muziki, filamu, televisheni, mitandao ya kijamii na majukwaa mbalimbali ya burudani, wasanii wanatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kampeni za elimu kwa umma kuhusu utunzaji wa noti na sarafu, pamoja na uelewa wa masuala ya fedha.

BoT imeendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii kuhusu matumizi salama na sahihi ya fedha, huku ikisisitiza umuhimu wa wananchi kushirikiana katika kulinda ubora wa noti na sarafu ili ziweze kutumika kwa muda mrefu na kwa ufanisi.

Aidha,semina hiyo pia imekuwa fursa ya kutoa elimu kuhusu majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania katika kusimamia na kudhibiti sekta ya huduma za kifedha nchini.

BoT inasimamia na kudhibiti shughuli za benki na taasisi za fedha, taasisi za mikopo ya nyumba, kampuni za karadha, taasisi za taarifa za wakopaji pamoja na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazohusika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here