NA DIRAMAKINI
WIZARA ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefafanua kuwa,Kisiwa cha Lupita kilichopo Ziwa Tanganyika katika Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa ni miongoni mwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na kwamba kimepangishwa kwa Kampuni ya Firelight Safaris Ltd.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Agosti 31,2026 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Taarifa hiyo imetolewa kufuatia taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa mwekezaji, Bw. Tim Draper anakusudia kuuza ardhi katika kisiwa hicho.
Kwa mujibu wa wizara, Kisiwa cha Lupita ni miongoni mwa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji chini ya Mamlaka ya Uwekezaji na Usimamizi wa Maeneo ya Uwekezaji (TISEZA).
Wizara imesema, eneo hilo limepangishwa kwa kampuni ya Firelight Safaris Ltd ambayo Bw. Tim Draper, raia wa Marekani ni miongoni mwa wanahisa.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Sheria ya Ardhi, Sura ya 113 imeweka utaratibu unaowawezesha wawekezaji wa kigeni kupata ardhi kwa madhumuni ya uwekezaji kupitia TISEZA.
Wizara imeeleza kuwa, TISEZA ambayo ndiyo mmiliki wa eneo hilo kwa mujibu wa sheria, ililipangisha kwa Firelight Safaris Ltd na kuipa kampuni hiyo Hakimiliki Isiyo ya Asili (Derivative Right) kwa ajili ya matumizi ya kuendesha hoteli ya kitalii.
Kwa msingi huo, Wizara imesema Firelight Safaris Ltd ni mwekezaji halali katika eneo hilo na kwamba kampuni hiyo inaweza kuhamisha uwekezaji wake kwa mwekezaji mwingine kwa kuzingatia sheria na taratibu za Tanzania.

