DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua rasmi machapisho ya maandishi ya nukta nundu (Braille) kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa kuona ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhakikisha taarifa kuhusu masuala ya uchumi na fedha zinawafikia wananchi wote kwa urahisi na kwa usawa.
Akizungumza leo Agosti 20,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa machapisho hayo, Naibu Gavana wa BoT,Dkt.Rahma Salim Mahfoudh amesema,hatua hiyo inaonesha dhamira ya BoT ya kuhakikisha taarifa kuhusu uchumi, huduma za kifedha na majukumu ya Benki Kuu zinapatikana katika mifumo inayozingatia mahitaji ya makundi mbalimbali katika jamii.Amesisitiza kuwa, ujumuishi wa kifedha haupaswi kuishia kwenye kufungua akaunti za benki au kupata huduma za kifedha pekee, bali unapaswa pia kuhakikisha kila mwananchi anapata taarifa anazohitaji ili kufanya maamuzi sahihi ya kifedha.
“Upatikanaji wa taarifa unazidi kuwa muhimu katika dunia ambayo uelewa wa masuala ya kifedha una mchango mkubwa katika maamuzi kuhusu kuweka akiba, kuwekeza, kukopa, kutumia huduma za kifedha na kujilinda dhidi ya udanganyifu wa kifedha,”ameeleza.
Aidha, Dkt.Mahfoudh ametoa wito kwa taasisi za umma, sekta binafsi, taasisi za elimu na wadau wengine kutathmini namna wanavyotoa taarifa na kujihoji iwapo huduma na njia zao za mawasiliano zinazingatia mahitaji ya watu wenye aina mbalimbali za ulemavu.
"Taasisi zinapaswa kujiuliza kama taarifa wanazotoa zinawafikia watu wote, kama mtu mwenye ulemavu wa kuona anaweza kuzipata kwa urahisi, na kama huduma zao zimezingatia mahitaji ya watu wenye aina mbalimbali za ulemavu,” amesema Dkt. Mahfoudh.
Machapisho hayo yanahusu mada mbalimbali, zikiwemo uanzishwaji wa benki na taasisi za fedha, usimamizi wa fedha binafsi, uwekezaji, taarifa za mikopo, amana, mifumo ya malipo, utoaji wa leseni za biashara na miongozo kwa watoa huduma ndogo za kifedha, pamoja na historia na majukumu ya Benki Kuu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wasioona Zanzibar, Bi.Fatma Dijaa ameishukuru Benki Kuu kwa kuendelea kuwafikia wasiiona hapa nchini na kupitia machapisho haya ya Braille watanufaika kwa kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kifedha.
Naye, Katibu wa Jumuiya ya Wasioona Tanzania (TBA), Bw.Iddi Damka, ameipongeza BoT kwa kutengeneza machapisho hayo ambayo yatapanua wigo wa elimu kwa umma.
Uzinduzi huu uliofanyika leo umehudhuriwa pia na wafanyakazi na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Chuo Kishirikishi cha Elimu Dar es Salaam (DUCE) pamoja na viongozi na wafanyakazi wa BoT.
Tags
Benki Kuu ya Tanzania
Habari
Maandishi ya Nukta Nundu
Machapisho ya Braille
Nukta Nundu
Watu wenye Ulemavu
















