REDESO,VETA wawaandaa wakufunzi kueneza nishati safi

MOROGORO-Shirika la Relief to Development Society (REDESO) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) limeendesha mafunzo maalumu ya siku 10 kwa wakufunzi 12 kutoka vyuo vya VETA, kwa lengo la kuwaandaa kuwa Wakufunzi wa Wakufunzi (Trainers of Trainers-ToT) katika teknolojia za nishati safi.
Wakufunzi hao wanatoka VETA Dar es Salaam, Moshi, Mbeya, Mwanza, Pwani na Singida, ambapo wamepatiwa mafunzo ya nadharia na vitendo kuhusu matumizi ya nishati ya jua, majiko banifu na teknolojia za usafiri wa umeme.

Mradi huo unalenga kuwawezesha wanawake na vijana kupata maarifa na ujuzi wa nishati safi, huku ukijikita katika teknolojia tatu kuu ambazo ni umeme wa jua, majiko banifu yanayotumia nishati safi na usafiri wa umeme, ikiwamo magari, pikipiki na bajaji.

Mafunzo hayo yanayofanyika katika Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro, yamejikita pia katika kuwafundisha washiriki namna ya kufunga na kutunza mifumo ya umeme wa jua majumbani.

Mtaalamu wa teknolojia ya nishati ya jua, Mzumbe Musa, ndiye anayetoa mafunzo ya vitendo, akiwafundisha washiriki kuhusu ufungaji, matumizi na matengenezo ya mifumo ya umeme wa jua.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkufunzi wa VETA Moshi, Mhandisi Frank Kabipi, alisema mafunzo hayo yameongeza uelewa na ujuzi wake kuhusu nishati safi na sasa yuko tayari kuwafundisha wanafunzi.

“Mafunzo haya ni muhimu kwa maisha yangu binafsi na jamii yangu kwa kuwa dunia inahama kutoka kwenye nishati chafu kwenda kwenye nishati safi kwa ajili ya kutunza mazingira. Sasa tutawafundisha wanafunzi namna ya kufunga mifumo ya sola, majiko na vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi,” alisema.

Kwa upande wake, Mkufunzi wa VETA Dodoma, Bahati Kaniki, alisema amejifunza matumizi mbalimbali ya nishati ya jua, ikiwamo kupikia, usafiri na kupata mwanga.

“Nimejifunza kwa vitendo na sasa nitakwenda kuwafundisha wanafunzi wangu ili wakatumie teknolojia hizi na kusambaza maarifa hayo katika jamii,” alisema.
Naye Mkufunzi kutoka VETA Pwani alisema mafunzo hayo yatasaidia jamii kuondokana na matumizi ya nishati chafu ambayo yana madhara kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Kupitia sisi walimu, ninaamini tutaleta mtazamo chanya katika jamii zetu kwa kuwa tutawafundisha vijana na wanawake kuwa na maarifa kuhusu nishati safi na kuchukua hatua ya kutumia majiko ya nishati safi, vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati safi na umeme wa jua,” alisema.

Wakufunzi Philemon Julius kutoka VETA Dar es Salaam na Musa Doma kutoka VETA Mwanza walisema mafunzo hayo ni “game changer” katika matumizi ya nishati safi, wakieleza kuwa watakwenda kuwafundisha wanafunzi kwa nadharia na vitendo ili kuleta mabadiliko katika jamii.

Baada ya kukamilisha mafunzo hayo, wakufunzi hao 12 watapeleka ujuzi walioupata kwa wanafunzi wao. REDESO na VETA pia zimeandaa mtaala wa nishati safi ambao utaingizwa katika mitaala ya vyuo vya TVET, ili kuwapa wanafunzi ujuzi unaohitajika katika teknolojia hizo.
Mradi huo unaofadhiliwa na International Development Research Centre (IDRC) unalenga kuongeza uelewa na ujuzi wa jamii kuhusu nishati safi, kupunguza hewa ukaa na kuunga mkono juhudi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kwa mujibu wa Mzumbe Musa, mfumo wa mafunzo kwa wakufunzi unalenga kuleta matokeo makubwa zaidi kwa kuwa ujuzi unaotolewa kwa wakufunzi utafikishwa kwa wanafunzi, wanawake na vijana wengi zaidi, hivyo kuongeza matumizi ya nishati safi katika jamii.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here