BoT yazindua programu ya ulezi wa kiuongozi kwa wanawake ya She Rise

DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) tarehe 4 Agosti 2026 imezindua rasmi Programu ya Ulezi wa Kiuongozi kwa Wanawake inayojulikana kama ‘She Rise’, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Benki za kuwaendeleza wanawake na kuwaandaa kushika nafasi za uongozi ndani na nje ya taasisi.
Programu ya ‘She Rise’ inalenga kuwawezesha wanawake kujenga uwezo wa kiuongozi kupitia ushauri, mwongozo, kujifunza na kubadilishana uzoefu na viongozi wenye uzoefu katika maeneo mbalimbali ya kitaaluma na kiuongozi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa programu hiyo, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba amesema, 'She Rise’ inaonesha dhamira ya Benki Kuu ya kuwekeza katika maendeleo ya wanawake na kuwaandaa kwa majukumu makubwa zaidi ya kiuongozi.
“Kupitia programu hii, tunalenga kutoa fursa kwa wanawake kujifunza, kujenga uwezo, kunufaika na uzoefu wa viongozi waliowatangulia, na kujiandaa kwa nafasi za juu za uongozi ndani na nje ya Benki Kuu,” amesema Gavana Tutuba.

Gavana Tutuba aliongeza kuwa programu hiyo ni sehemu ya jitihada pana za Benki Kuu katika kuwaendeleza watumishi wake kupitia mafunzo, programu za kujenga uwezo na fursa mbalimbali za kujifunza, kwa lengo la kuhakikisha kila mtumishi anapata nafasi ya kukuza uwezo wake na kutoa mchango mkubwa zaidi katika kutekeleza majukumu ya Benki Kuu na kulihudumia taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Naibu Gavana wa Utawala na Udhibiti wa Ndani, Dkt. Rahma Mahfoudh, alisema Benki Kuu imeingia makubaliano ya miezi tisa na Uongozi Institute kwa ajili ya kusimamia na kuwezesha utekelezaji wa programu hiyo.

Alisema ushirikiano huo pia utasaidia katika kujenga uwezo na kurithisha ujuzi kwa Kamati Tendaji ya ndani ambayo itasimamia na kuendesha programu hiyo baada ya kipindi cha ushirikiano na Uongozi Institute.

“Programu hii itaendeshwa kwa muda wa miezi tisa. Katika awamu ya kwanza, tumepata walezi nane (8) (Mentors) na wanawake wanufaika kumi na mmoja (11) (Mentees) ambao wameweza kukidhi vigezo baada ya mchakato wa kuchakata na kutathmini maombi yaliyopokelewa,” amesema Dkt. Mahfoudh.
Hafla ya uzinduzi ilihudhuriwa pia na Afisa Mtendaji Mkuu wa Uongozi Institute, Bw. Kadari Singo, pamoja na viongozi na wawakilishi kutoka benki ya NMB, benki ya KCB, Women in Management Africa (WIMA) na MultiChoice Tanzania.

Viongozi na wawakilishi hao walishiriki katika mjadala uliofanyika baada ya uzinduzi, ambapo walibadilishana uzoefu na kutoa mtazamo kuhusu umuhimu wa ulezi, ujenzi wa uwezo na uwezeshaji wa wanawake katika kufikia nafasi za juu za uongozi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here