Cameroon gizani,Rais Biya atimiza miezi miwili mapumzikoni barani Ulaya

NA DIRAMAKINI

HALI ya sintofahamu za kisiasa zimeendelea kuitikisa nchini Cameroon baada ya Rais wa nchi hiyo, Paul Biya mwenye umri wa miaka 93, kukaa nje ya nchi kwa takribani miezi miwili bila kurejea nyumbani, hali inayozua maswali kuhusu mustakabali wa uongozi wa taifa hilo linaloongozwa na Biya kwa zaidi ya miongo minne.
Biya aliondoka Cameroon Juni 7, 2026 kuelekea barani Ulaya kwa kile kilichoelezwa na Serikali kuwa ni mapumziko binafsi ya muda mfupi.

Hata hivyo,kwa mujibu wa mashirika mbalimbali ya habari hadi sasa Rais huyo hajarejea nchini na muda wa safari yake umeendelea kuongeza wasiwasi miongoni mwa wananchi,wanasiasa wa upinzani na wadau wa uchumi.

Ingawa sheria za Cameroon hazijaweka kikomo cha muda ambao Rais anaweza kukaa nje ya nchi, kutokuwepo kwake kwa muda mrefu kumeibua mjadala mpana kuhusu namna Serikali inavyoendeshwa, hali ya Rais na suala la urithi wa madaraka.

HAKUNA MAKAMU WA RAIS

Moja ya mambo yanayofanya hali hiyo kuwa nyeti zaidi ni kwamba Cameroon haina nafasi ya Makamu wa Rais, hivyo hakuna mrithi wa moja kwa moja wa kikatiba anayeshikilia madaraka ya utendaji wakati Rais akiwa hayupo.

Hali hiyo imeongeza maswali kuhusu nani anayeongoza kikamilifu shughuli za Serikali endapo Rais atashindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu yoyote.

Aidha,vyama vya upinzani vimeanza kuelezea hali hiyo kama nchi inayojiendesha kwa kile walichokiita “autopilot”, huku vikitaka ufafanuzi zaidi kuhusu hali ya Rais na mwelekeo wa uongozi wa taifa.

Issa Tchiroma Bakary aliyewahi kuwa mshirika wa Rais Biya na ambaye alishika nafasi ya pili katika uchaguzi wa urais wa Oktoba, amesema kuna imani inayozidi kuenea nchini humo kwamba mambo hayako sawa kwa Rais huyo.

Bakary pia amesema, kukaa kwa muda mrefu kwa Biya nchini Uswisi kunadhoofisha uhalali wa uongozi na kunaonyesha jitihada za kuendelea kushikilia madaraka licha ya changamoto zinazomkabili.

BIYA AONGOZA KUTOKA NJE

Licha ya kutokuwepo nchini, Rais Biya ameendelea kutoa maagizo ya Serikali, ikiwemo mabadiliko katika uongozi wa kijeshi.

Wiki hii, amri tatu zilizotangazwa kupitia akaunti rasmi ya Rais katika mtandao wa X zilitangaza mabadiliko makubwa katika mfumo wa uongozi wa kijeshi wa Cameroon.

Mabadiliko hayo yamehusisha kumpandisha cheo Mkuu wa Walinzi wa Rais kuwa Brigedia Jenerali, kubadilisha makamanda katika maeneo manne kati ya matano ya kijeshi nchini humo na kumteua kamanda mpya wa kikosi maalumu cha Rapid Intervention Brigade.

Hatua hiyo imeongeza mjadala kuhusu namna mamlaka ya Rais yanavyotekelezwa akiwa nje ya nchi na kiwango cha ushawishi alichobaki nacho katika uendeshaji wa Serikali.

MABADILIKO YAONGOZA KWA MAOFISA WALEWALE

Profesa Wilson Tamfuh, mtaalamu wa Sheria za Umma na Kimataifa amesema,mabadiliko ya Baraza la Mawaziri na uongozi wa kijeshi yaliyofanyika katika kipindi cha miaka 15 iliyopita kwa kiasi kikubwa yamehusisha kuwahamisha maofisa wale wale kutoka nafasi moja kwenda nyingine.

Kauli hiyo imeongeza mjadala kuhusu ufanisi wa mabadiliko hayo katika kuleta sura mpya ya uongozi na taasisi za Serikali.

WAWEKEZAJI WAPIGA BREKI

Wakati mjadala wa kisiasa ukiendelea, hali hiyo pia imeanza kuonekana katika masoko ya fedha na mazingira ya uwekezaji.

Kwa mujibu wa taarifa ya Bloomberg, hati fungani za Cameroon zinazouzwa kwa dola ya Marekani zimekuwa miongoni mwa zilizofanya vibaya zaidi barani Afrika tangu mwanzoni mwa Juni, huku wawekezaji wakijaribu kutathmini iwapo kuna mchakato wa mpito wa kisiasa unaoendelea kimyakimya.

Cameroon ni miongoni mwa nchi zinazozalisha mafuta barani Afrika, hivyo utulivu wa kisiasa na mwendelezo wa sera za Serikali ni mambo muhimu kwa wawekezaji na washirika wa kimataifa.

Kutokuwepo kwa mpango wa wazi wa urithi wa madaraka kunazidi kuongeza sintofahamu kuhusu mwelekeo wa nchi hiyo endapo kutatokea mabadiliko ya ghafla katika uongozi.

NANI ATAONGOZA BAADA YA BIYA?

Rais Paul Biya ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40, ni miongoni mwa viongozi waliotawala kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.

Kutokuwepo kwake kwa muda mrefu kumeibua tena swali ambalo limekuwa likijadiliwa kwa miaka mingi nchini Cameroon, nani atarithi madaraka na mchakato huo utafanyikaje?.

Kwa sasa, Serikali inaendelea kufanya shughuli zake huku Rais akiendelea kutoa maagizo akiwa nje ya nchi.

Hata hivyo, kadiri kutokuwepo kwake kunavyoongezeka, ndivyo maswali kuhusu afya yake, uwezo wa kuendelea kuongoza, uthabiti wa taasisi za Serikali na mustakabali wa kisiasa yanavyozidi kupata uzito.

Vilevile, kwa wananchi, vyama vya siasa, wawekezaji na washirika wa kimataifa, suala kubwa si tu lini Rais Biya atarejea Cameroon, bali pia nchi hiyo imejiandaa kwa kiwango gani kwa kipindi kitakachofuata uongozi wake.(NA)

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here