DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema Kielelezo cha Faida Rejea ya Dhamana za Serikali (Tanzania Sovereign Yield Curve) kitaongeza uwazi, ushindani na ufanisi katika soko la Dhamana za Serikali.
Gavana Tutuba ameyasema hayo katika hafla ya uzinduzi wa Kielelezo hicho uliyofanyika tarehe 7 Agosti 2026 katika ofisi za Benki Kuu jijini Dar es Salaam.
Amesema Kielelezo hicho kinachotokana na miamala halisi katika soko la upili kitawawezesha wawekezaji kufuatilia mwenendo wa faida na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji.
Aidha, ameeleza kuwa Kielelezo hicho pia kitakuwa rejea muhimu katika kupanga bei za mikopo, mikopo ya nyumba na hatifungani za kampuni, kwa kutumia viwango rejea visivyo na hatari (risk-free benchmark rates).
Gavana Tutuba ameongeza kuwa kitasaidia kuvutia mitaji ya kigeni na kuongeza ushindani katika soko la dhamana za serikali, huku akisisitiza kuwa soko hilo lina mchango muhimu katika kuiwezesha Serikali kupata fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.
"Ushiriki wa wadau katika soko la Dhamana za Serikali ni muhimu katika kuiwezesha Serikali kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na hivyo kuchangia katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,” amesema.
Vilevile, alisisitiza kuwa Kielelezo hicho ni kioo kinachoakisi matarajio ya soko kuhusu mwelekeo wa ukuaji wa uchumi, mfumuko wa bei na sera ya fedha, huku kwa upande wa Benki Kuu kikitarajiwa kuimarisha utekelezaji wa sera ya fedha inayotegemea viwango vya riba (interest rate-based monetary policy transmission).
Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, ameeleza kuwa amesema Kielelezo hicho ni hatua muhimu na ya kihistoria katika kuendeleza soko la Dhamana za Serikali na kujenga miundombinu ya masoko inayokidhi viwango vya kimataifa.
Kamishna huyo alisisitiza kuwa Kilelezo hiki ni suluhsho la changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa taarifa za kutosha kuhusu viwango halisi vya faida vinavyotokana na mauzo na manunuzi ya Dhamana katika soko la upili, hali iliyokuwa ikifanya iwe vigumu kupanga bei sahihi za dhamana.
Awali, Naibu Gavana wa Sera za Uchumi na Fedha wa Benki Kuu ya Tanzania, Dkt. Yamungu Kayandabila, alitambua na kupongeza mchango wa wataalamu kutoka Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania, pamoja na utaalamu uliotolewa na Ofisi ya Hazina ya Marekani (U.S. Treasury Department), katika kufanikisha uundwaji wa Kielelezo hicho, akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano huo wa kitaalamu katika juhudi za kuendeleza na kuimarisha soko la Dhamana za Serikali nchini.
Hafla hiyo pia ilihudhuriwa, Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA. Nicodemas Mkama, Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela, viongozi na watumishi wa Wizara ya Fedha, Wawakilishi wa Idara ya Hazina ya Marekani na wadau wengine wa sekta ya fedha nchini.















