Chamwino walipwa fidia Shilingi bilioni 4.9 kupisha chanzo cha maji

DODOMA-Serikali imelipa fidia kiasi cha Shilingi bilioni 4.9 kwa wananchi wilayani Chamwino waliopisha eneo la hifadhi ya maji Chamwino.
Naibu Waziri wa Maji Mhe. Mhandisi Kundo Mathew (Mb) akikabidhi mfano wa hundi kwa wawakilishi wa wananchi hao amesema maji ni kichocheo cha maendeleo na kusisitiza, chanzo cha Chamwino ni muhimu kwa Jiji la Dodoma na maeneo jirani.

Amesema, fidia hiyo inalipwa kwa wananchi 880 ili kuhakikisha chanzo hicho kinalindwa kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.

Amesema bila kulinda vyanzo vya maji, upatikanaji wa maji wa uhakika hauwezi kufikiwa kwasababu mamlaka za maji zitakuwa na miundombinu isiyokuwa na faida kwa jamii.

Ameainisha kuwa Serikali imelipa wananchi jumla ya Shilingi bilioni 36.756 iliwa ni fidia katika maeneo mbalimbali ya hifadhi ya maji nchini.

Amezielekeza Bodi za Maji za Mabonde kuhakikisha vyanzo vya maji vinasimamiwa, vinawekewa mipaka na kutangazwa rasmi, na kuzitaka mamlaka za maji kushirikiana na mabonde kuhakikisha maeneo hayo yanapatiwa hati miliki na kuwekewa mikakati ya kudhibiti uvamizi na ushirikishwaji wa wananchi katika ulinzi wa miundombinu.
Amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Waziri amesema historia ya eneo hilo ni kuwa lilitangazwa kuwa eneo la hifadhi mwaka 1973, likiwa na ukubwa wa ekari 2,100, ambapo ekari 740 zilitengwa kwa ajili ya hifadhi.

Ameainisha wananchi 880 kutoka Vitongoji vya Mpera na Sokoine wanahusika katika zoezi la ulipaji fidia, na kuwataka wananchi kuepuka uvamizi wa eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wapokea fidia, Bi. Maina Elieza ameishukuru Serikali kwa wepesi wa mchakato wa ulipaji fidia ambao ulikwama tangu mwaka 1990.
Zoezi hilo ni sehemu ya hatua za Serikali za kulinda vyanzo vya maji nchini, kuhakikisha wananchi wanapatiwa haki ya stahiki na kuweka mazingira bora ya upatikanaji wa huduma ya maji katika Jiji la Dodoma.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here