Dar ipo tayari kupokea wageni wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika-RC Chalamila

NA GODFREY NNKO

MKOA wa Dar es Salaam umekamilisha maandalizi ya kuwa mwenyeji wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika (Africa50 General Shareholders’ Meeting-GSM and Infra for Africa Forum) unaotarajiwa kufanyika kesho Agosti 5 hadi 6, 2026 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa leo Agosti 4,2026 na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert John Chalamila wakati akizungumza na waandishi wa habari katika ukumbi wa JNICC.

Amesema kuwa, maandalizi yote muhimu yamekamilika ili kuhakikisha mkutano huo unafanyika kwa mafanikio na viwango vinavyokubalika kimataifa.

Mkutano huo unatarajiwa kuwa miongoni mwa mikutano mikubwa ya kimataifa inayofanyika nchini mwaka huu, ukiwaleta pamoja washiriki zaidi ya 1,200 kutoka ndani na nje ya Afrika, wakiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali.

Sambamba na viongozi wa taasisi za fedha za kimataifa, wanahisa wa Africa50, wawekezaji, viongozi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo.

Amesema, katika hafla ya ufunguzi, viongozi mbalimbali wa nchi wanatarajiwa kushiriki wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye atakuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Viongozi wengine wanaotarajiwa kushiriki ni Rais João Lourenço wa Angola, Rais Bassirou Diomaye Faye wa Senegal, Rais Daniel Francisco Chapo wa Msumbiji, Rais Bola Ahmed Tinubu wa Nigeria, Rais William Samoei Ruto wa Kenya na Rais Brice Clotaire Oligui Nguema wa Gabon.

Ushiriki wa viongozi hao unatarajiwa kuongeza uzito wa mkutano huo, ambao unalenga kujadili mikakati ya kuharakisha maendeleo ya miundombinu barani Afrika na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na taasisi za fedha.

RC Chalamila amesema, mkutano huo unatajwa kuwa jukwaa muhimu kwa Tanzania kuendelea kujitangaza kama kitovu cha biashara, uwekezaji na maendeleo ya miundombinu barani Afrika, huku ukitoa fursa ya kuwasilisha miradi mbalimbali ya kimkakati kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.

Miongoni mwa miradi inayotarajiwa kuwasilishwa ni Reli ya Kisasa (SGR), Bandari ya Dar es Salaam, miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme pamoja na miundombinu ya TEHAMA.

Uwasilishwaji wa miradi hiyo unalenga kuvutia mitaji na washirika wa kimataifa, sambamba na kuharakisha utekelezaji wa Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV) na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa Tanzania, fursa hiyo ni muhimu katika kuongeza uwekezaji katika miundombinu ambayo ni msingi wa ukuaji wa uchumi, kuongeza uzalishaji, kurahisisha usafirishaji wa bidhaa na watu na kuimarisha nafasi ya nchi katika biashara ya kikanda na kimataifa.

Africa50 ni taasisi ya uwekezaji wa miundombinu barani Afrika iliyoanzishwa kwa ushirikiano kati ya nchi za Afrika na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ikiwa na jukumu la kuandaa na kusaidia kufadhili miradi ya maendeleo yenye uwezo wa kuvutia uwekezaji.

Taasisi hiyo pia inalenga kuhamasisha ushiriki mkubwa wa sekta binafsi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu kupitia ubia kati ya Serikali na sekta binafsi (PPP).

Kwa msingi huo, mkutano wa Dar es Salaam unatarajiwa kuwa jukwaa la kubadilishana uzoefu na kutafuta njia mpya za kuongeza mitaji kwa ajili ya miradi mikubwa ya miundombinu barani Afrika.

RC Chalamila amesema,Serikali imejipanga kuhakikisha wageni wote watakaofika nchini kwa ajili ya mkutano huo wanapata huduma bora tangu wanapowasili hadi wanapoondoka.

Amesema, maandalizi yamefanyika kwa ushirikiano wa wizara, taasisi za Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wadau mbalimbali, kwa lengo la kuhakikisha mkutano unafanyika katika mazingira salama, tulivu na yenye viwango vya kimataifa.

Pia, amesema Mkoa wa Dar es Salaam umejipanga kuhakikisha mkutano huo unakuwa kielelezo cha uwezo wa Tanzania kuandaa mikutano mikubwa ya kimataifa na kuongeza taswira chanya ya nchi katika jumuiya ya kimataifa.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wananchi wa Dar es Salaam kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kuwapokea wageni kwa ukarimu, kudumisha usafi wa mazingira, kuheshimu sheria na taratibu za nchi na kutoa ushirikiano kwa mamlaka husika pale utakapohitajika.

Aidha, amewataka wafanyabiashara na watoa huduma kutumia fursa hiyo kwa kutoa huduma zenye weledi, uadilifu na viwango vya kimataifa, huku akiwataka kuepuka kupandisha bei kiholela au kutoa huduma zisizokidhi viwango kwa wageni.

RC Chalamila amesema tabia hizo zinaweza kuathiri taswira ya Tanzania na kupunguza manufaa yanayoweza kupatikana kutokana na mkutano huo.

Vilevile amevipongeza vyombo vya habari kwa ushirikiano wao na kuvitaka kuendelea kutoa taarifa sahihi, kwa wakati na zenye kujenga, ili kuutangaza mkutano huo pamoja na fursa zinazotokana nao.

Serikali inatarajia kuwa mafanikio ya Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika yatafungua fursa mpya za uwekezaji, biashara, ajira na maendeleo ya miundombinu, sambamba na kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na mataifa mengine ya Afrika na duniani.

Kwa Dar es Salaam, mkutano huo pia ni fursa ya kuimarisha nafasi yake kama kitovu cha mikutano ya kimataifa, biashara na uwekezaji katika Afrika Mashariki, huku Tanzania ikitumia jukwaa hilo kuwasilisha uwezo wake, fursa za uwekezaji na miradi ya kimkakati inayohitaji mitaji na teknolojia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here