DODOMA-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amekutana na kufanya mazungumzo na Mwakilishi Mkazi Mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) nchini Tanzania, Bi. Jana Bricco, katika Makao Makuu ya Benki Kuu jijini Dodoma, tarehe 26 Agosti 2026.
Katika kikao hicho, Gavana Tutuba alieleza hatua mbalimbali zinazoendelea kutekelezwa na Benki Kuu katika kusimamia ukuaji na ustahimilivu wa uchumi, ikiwemo kuimarisha uthabiti wa thamani ya Shilingi, kuongeza akiba ya fedha za kigeni kupitia programu ya ununuzi wa dhahabu, pamoja na kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za fedha.
Kwa upande wake, Bi. Bricco aliipongeza Tanzania kwa kukamilisha programu mbili za kifedha za IMF, ambazo ni Extended Credit Facility (ECF), inayolenga kusaidia nchi kuimarisha uchumi kupitia upatikanaji wa mikopo yenye masharti nafuu, na Resilience and Sustainability Facility (RSF), inayosaidia kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuimarisha ustahimilivu wa uchumi. Programu hizo zimeiwezesha Tanzania kupata jumla ya Dola za Marekani milioni 443.9.



