NA GODFREY NNKO
MWANASHERIA Mkuu wa Serikali,Mheshimiwa Hamza Johari amesema, kupoteza uanachama wa chama cha siasa kwa aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kulisababisha kupoteza sifa ya kushika nafasi hiyo na hivyo kufanya kiti cha Makamu wa Rais kuwa wazi kabla ya tarehe ya kujiuzulu iliyotajwa katika barua yake.
Akichangia hoja ya Waziri Mkuu,Dkt.Mwigulu Nchemba ya kumthibitisha Makamu wa Rais mteule,Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi, bungeni jijini Dodoma leo Agosti 28,2026, Mheshimiwa Johari amesema,suala hilo linapaswa kutazamwa kwa kuzingatia Katiba kwa ujumla na si kifungu kimoja pekee.
Mheshimiwa Johari amesema,awali kulikuwa na uwezekano wa kiti hicho kuwa wazi kuanzia Septemba 4, 2026 kutokana na taarifa ya kujiuzulu iliyowasilishwa na aliyekuwa Makamu wa Rais na kukubaliwa na Rais.
Hata hivyo, amesema kabla ya tarehe hiyo kufika kulitokea jambo jingine la kikatiba, la kupoteza uanachama wa chama cha siasa ambalo lilisababisha kupoteza sifa ya kushika kiti hicho kwa mujibu wa Ibara ya 47(4)(c) ya Katiba, ikisomwa pamoja na Ibara ya 50(2)(h).
“Kwa kifupi, ni kwamba taarifa ya kujiuzulu ingeweza kusababisha nafasi ya Makamu wa Rais kuwa wazi kuanzia tarehe 4 Septemba, 2026. Lakini kabla ya tarehe hiyo kufika, limetokea suala la kupoteza uanachama na limesababisha kupoteza sifa ya kushika kiti kwa mujibu wa Ibara ya 47(4)(c) ya Katiba, ikisomwa pamoja na Ibara ya 50(2)(h),”amesema.
Kwa mujibu wa Mwanasheria Mkuu, Ibara ya 50(2)(h) inatoa msingi wa kikatiba wa kuzingatia mazingira mengine yanayoweza kumfanya Makamu wa Rais asiendelee kushika nafasi hiyo.
Amesema,Serikali haina changamoto yoyote ya kikatiba katika hatua iliyochukuliwa na kwamba itaendelea kuhakikisha maamuzi yake yanafanyika kwa kuzingatia Katiba.
“Kwa hiyo, Mheshimiwa Spika, ninaomba nilijulishe Bunge lako Tukufu kwamba hakuna changamoto yoyote ya Kikatiba na kama Serikali, tutaendelea kuhakikisha kwamba tunazingatia Katiba katika maamuzi mbalimbali tunayoyafanya,”amesema.
Ufafanuzi wa AG
Mheshimiwa Johari amesema,baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais kuwasilisha barua ya kujiuzulu, tarehe iliyotajwa katika barua hiyo ilikuwa Septemba 4, 2026 na Rais aliikubali.
Amesema,hali hiyo ingeifanya Septemba 4 kuwa tarehe rasmi ya kujiuzulu kwa mujibu wa Ibara ya 149(2) ya Katiba, ambayo inatambua tarehe ya kujiuzulu kuwa tarehe ambayo taarifa ya kujiuzulu imepokelewa au tarehe nyingine iliyotajwa katika barua hiyo.
“Kwa hiyo, hiyo ndiyo scenario, kwa maana kwamba ataendelea kuwepo madarakani mpaka tarehe 4 Septemba 2026. Sasa tunakuja kusema kwamba, kwa kuwa maisha yanaendelea, je, ni zuio? Yanapotokea mambo mengine ya Kikatiba yanayomfanya apoteze sifa, kwamba tunaendelea kusubiri tarehe hiyo, ndiyo ufafanuzi ninataka kuutoa,”amesema.
Mwanasheria Mkuu amesema,baadhi ya hoja zilizotolewa kuhusu suala hilo zimejikita katika Ibara ya 50(4), ambayo inaweka utaratibu wa kujaza nafasi ya Makamu wa Rais inapokuwa wazi.
Amesema, Ibara hiyo inataja mazingira kama kuondolewa madarakani kwa Makamu wa Rais na Bunge, kifo au mazingira mengine yaliyowekwa katika Katiba na inaelekeza Rais kumteua mtu mwingine ambaye uteuzi wake unapaswa kuthibitishwa na Bunge ndani ya muda uliowekwa.
Hata hivyo, amesema kutotajwa moja kwa moja kuhusu kupoteza uanachama katika Ibara hiyo, hakumaanishi kwamba tukio hilo haliwezi kusababisha nafasi hiyo kuwa wazi.
Amesema,katika kutafsiri Katiba na sheria, vifungu mbalimbali vinapaswa kusomwa kwa pamoja ili kutoa tafsiri yenye mantiki na inayozingatia madhumuni ya Katiba.
Kwa lugha ya kisheria amesema, kuna kanuni ya harmonious construction, inayolenga kuhakikisha vifungu mbalimbali vya sheria au Katiba vinatafsiriwa kwa namna inayopatana badala ya kutafsiri kifungu kimoja kwa kujitenga na vifungu vingine.
Akifafanua zaidi,Mheshimiwa Johari amerejea Ibara ya 47(4) inayoweka sifa za mtu anayestahili kuteuliwa, kugombea au kushika nafasi ya Makamu wa Rais.
Amesema,miongoni mwa sifa hizo ni kuwa raia wa kuzaliwa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mujibu wa sheria za uraia, kutimiza umri wa miaka 40, kuwa mwanachama wa chama cha siasa na kuwa mgombea aliyependekezwa na chama cha siasa.
Sifa nyingine amesema, ni kuwa na sifa za kumwezesha mtu kuwa Mbunge au Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi na kutokuwa ametiwa hatiani na mahakama kwa kosa la kukwepa kulipa kodi ya Serikali katika kipindi cha miaka mitano kabla ya tarehe ya uchaguzi.
Pia,amesema sifa hizo haziwezi kutazamwa kuwa ni za wakati wa kugombea pekee, kwa kuwa Katiba inazitaja pia kwa mtu anayeshika nafasi hiyo.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Johari, tafsiri inayodai kwamba sifa hizo zinahusu mgombea pekee inaweza kuleta matokeo yasiyokuwa na mantiki katika uendeshaji wa Serikali.
Ametoa mfano kwamba, endapo sifa hizo zisingehusika kwa mtu anayeteuliwa kushika nafasi ya Makamu wa Rais, kinadharia mtu mwenye umri chini ya miaka 40 au mtu ambaye si raia wa Tanzania angeweza kuteuliwa, jambo ambalo haliwezi kuwa lengo la Katiba.
Mheshimiwa Johari amesema,Ibara ya 50(4) na Ibara ya 47 zinapaswa kutafsiriwa kwa pamoja ili kuleta maana inayopatana na mantiki ya Katiba.
Amesema,si sahihi kudai kwamba kwa kuwa Ibara ya 50(4) haikutaja wazi kupoteza uanachama wa chama cha siasa kama moja ya mazingira ya kufanya kiti kuwa wazi, basi tukio hilo haliwezi kuwa na athari kwa nafasi ya Makamu wa Rais.
Pia,amesema Katiba haiwezi kuorodhesha kila tukio linaloweza kujitokeza katika maisha ya mtu anayeshika nafasi ya juu ya uongozi wa nchi. “Hatupaswi kuleta vihoja katika tafsiri; tunatakiwa kutafsiri kuleta logic na mantiki,” amesema.
Ameongeza kuwa, Ibara ya 50(2)(h), inayohusu mazingira ambayo Makamu wa Rais anaacha kushika kiti “vinginevyo kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii”, ndiyo inayoweza kubeba mazingira mengine yanayosababisha mtu kupoteza sifa za kuendelea kushika nafasi hiyo.
Katika kuimarisha hoja yake,Mheshimiwa Johari alirejea tukio la mwaka 2021 wakati Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan alipowasilisha jina la Dkt.Philip Isdory Mpango bungeni kwa ajili ya kuthibitishwa kuwa Makamu wa Rais.
Amesema,utaratibu huo ulifanyika chini ya Ibara ya 50(4), licha ya mazingira ya wakati huo kutokuwa yameandikwa kwa maneno yale yale katika kifungu hicho.
Mheshimiwa Johari amesema, Dkt.Mpango alithibitishwa na Bunge Machi 30, 2021 na kuapishwa siku iliyofuata, Machi 31, 2021, jambo alilolitumia kueleza umuhimu wa kutafsiri Katiba kwa kuzingatia mazingira halisi na uhusiano wa vifungu vyake.
Kwa maelezo yake, mfano huo unaonesha kwamba tafsiri ya Katiba haiwezi kutegemea maneno ya kifungu kimoja pekee bila kuangalia vifungu vingine vinavyohusiana na jambo husika.
Mheshimiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia ameeleza sababu ya Katiba kuhitaji Bunge kuthibitisha mtu anayeteuliwa kushika nafasi ya Makamu wa Rais pale nafasi hiyo inapokuwa wazi.
Amesema,katika mazingira ya kawaida, Makamu wa Rais huchaguliwa pamoja na Rais katika Uchaguzi Mkuu na huingia madarakani pamoja na Rais, hivyo huwa amepata ridhaa ya wananchi kupitia uchaguzi.
Hata hivyo, nafasi inapokuwa wazi katikati ya kipindi cha uongozi, mtu anayeteuliwa kushika nafasi hiyo huwa hajachaguliwa moja kwa moja na wananchi.
Kwa sababu hiyo, amesema Katiba imeweka utaratibu wa uteuzi huo kuthibitishwa na Bunge, ambalo linawakilisha wananchi.
“Katika mazingira hayo anakuwa amepata ridhaa ya wananchi. Lakini nafasi inapokuwa wazi katika kipindi, mtu anayeteuliwa hajachaguliwa moja kwa moja na wananchi. Ndiyo maana Katiba imeweka uthibitisho katika Bunge hili, kwa wawakilishi wa wananchi wote, ili hiyo ridhaa itoke kwa niaba yao,”amesema.
Ampongeza Ndejembi
Wakati huo huo, Mheshimiwa Johari pia amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kumteua Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu wa Rais mteule.
Amesema anamfahamu Ndejembi na amewahi kufanya naye kazi katika utekelezaji wa miradi mbalimbali mikubwa ya kitaifa.
Pia,amemtaja kuwa ni mtu mwenye uwezo mkubwa, weledi, nidhamu na utii, akiongeza kuwa pia ni miongoni mwa watu wenye upendo na huruma.
Hatua ya Bunge kujadili na kuthibitisha uteuzi huo imekuja katika mazingira ya mjadala mpana wa kikatiba kuhusu tafsiri ya vifungu vinavyohusu nafasi ya Makamu wa Rais, hasa baada ya aliyekuwa Makamu wa Rais kuwasilisha taarifa ya kujiuzulu na baadaye kupoteza uanachama wa chama cha siasa.
Mheshimiwa Johari amewataka Watanzania, hususan wanaojadili masuala hayo, kutegemea tafsiri ya Katiba inayozingatia vifungu vyake kwa pamoja badala ya kutegemea hoja zinazotolewa bila kuzingatia misingi ya tafsiri ya sheria.
Hata hivyo,wabunge 324 wamepiga kura za ndio kumthibitisha Makamu wa Rais mteule, Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi katika mchakato ambao umefanyika leo bungeni jijini Dodoma.
Tags
Bunge la Tanzania
Bungeni Leo
Habari
Makamu wa Rais
Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Ofisi ya Makamu wa Rais Tanzania









