BoT yaikabidhi HESLB jukumu la kuratibu zoezi la upatikanaji wa wanufaika Mfuko wa Mwalimu Julius Nyerere

NA GODFREY NNKO

BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imeikabidhi Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) jukumu la kuratibu mchakato wa maombi na uteuzi wa wanufaika wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hatua inayolenga kuongeza uwazi, usawa na ufanisi katika utoaji wa ufadhili kwa wanufaika wa elimu ya juu nchini.
Uamuzi huo umeanza kutumika katika udahili wa mwaka wa masomo 2026/27 baada ya Bodi ya Usimamizi wa Mfuko huo kuridhia kutumia mifumo ya HESLB katika mchakato wa kutangaza, kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi wanaostahili kupata ufadhili.

Hayo yamesemwa leo Agosti 28,2026 jijini Dar es Salaam na Gavana wa BoT, Bw.Emmanuel Tutuba wakati akizindua Mwongozo Mpya wa Utoaji Ufadhili kwa Wanafunzi wanaonufaika na Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Gavana Tutuba amesema, uamuzi huo ulifikiwa na Bodi ya Mfuko katika kikao chake kilichofanyika Mei,mwaka huu, baada ya kubaini umuhimu wa kutumia mifumo iliyopo serikalini ili kurahisisha mchakato wa kuwapata wanafunzi wenye sifa.
Amesema hapo awali, tangu mfuko huo ulipoanzishwa mwaka 2009, nafasi za ufadhili zilitangazwa kupitia vyombo vya habari, vikiwamo televisheni, magazeti na mitandao ya kijamii, ambapo wanafunzi wenye sifa waliwasilisha maombi yao na kuchambuliwa na timu ya wataalamu wa BoT.

“Tumekubaliana sasa kutumia mifumo inayoratibiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu. Mfumo huo una uwezo wa kutumia taarifa za ufaulu kutoka Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), hivyo kutuwezesha kupata wanafunzi wenye sifa kwa utaratibu wenye ufanisi zaidi,” amesema Gavana Tutuba.

Amesema,mabadiliko hayo yanaendana na msisitizo wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu umuhimu wa mifumo ya Serikali kusomana ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Gavana huyo, badala ya kuendelea na utaratibu wa kutangaza nafasi na kusubiri maombi, HESLB itaweza kutumia mifumo yake iliyopo kuchakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaokidhi vigezo vya ufadhili.
"Kwa kuwa mfumo wa Bodi ya Mikopo tayari unachakata taarifa za wanafunzi na kubaini wanaostahili kupata mikopo, tumeona ni jambo jema kutumia utaratibu huo huo katika kupata wanufaika wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere,” amesema

Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulianzishwa Oktoba 12, 2009 ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi mchango wa Baba wa Taifa katika kuendeleza elimu na rasilimali watu nchini.

Gavana Tutuba amesema,Mwalimu Nyerere alikuwa mtetezi mkubwa wa haki ya Watanzania kupata elimu na alikuwa mwasisi wa programu mbalimbali za elimu, kuanzia elimu ya awali, msingi na sekondari hadi elimu ya vyuo vya kati na vyuo vikuu.

Amesema,watumishi wa BoT waliokuwepo wakati huo waliona umuhimu wa kuanzisha mfuko huo kwa kutumia michango yao wenyewe ili kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuendeleza elimu ya juu na kuenzi misingi iliyoachwa na Mwalimu Nyerere.

“Watumishi walijichanga, wakapata fedha na kuanzisha mfuko huu. Ndio chimbuko la mfuko huu kuwa chini ya Benki Kuu ya Tanzania,” amesema.
Tangu kuanzishwa kwake, Gavana Tutuba amesema,mfuko huo umekuwa ukitoa ufadhili kwa wanafunzi Watanzania wenye ufaulu wa juu wanaosoma katika vyuo vikuu vinavyotambuliwa nchini.

Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, mfuko huo umekuwa ukitoa ufadhili kwa makundi mawili makuu ya wanafunzi. Amesema,kundi la kwanza ni wanafunzi wa shahada ya kwanza, likiwa na programu maalumu inayolenga wanafunzi wa kike wanaosoma Hisabati na Sayansi.

Kundi jingine ndani ya ngazi ya shahada ya kwanza linahusisha wanafunzi wa kike na wa kiume wanaosoma fani za Hisabati, Sayansi, Uchumi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Uhasibu na Fedha.

Gavana Tutuba amesema, kundi la pili ni wanafunzi wa shahada ya uzamili wanaochaguliwa kutokana na ufaulu wao wa juu katika fani hizo.

Amesema, ufadhili huo unahusisha gharama mbalimbali za masomo ikiwa ni pamoja na ada kulingana na viwango vya vyuo husika, fedha za kujikimu, mafunzo kwa vitendo, utafiti, ukusanyaji wa takwimu kwa ajili ya tasnifu pamoja na vifaa vya kujifunzia.

Pia,amesema kila mwanafunzi anayepata ufadhili huo hupewa kompyuta mpakato kwa ajili ya kurahisisha masomo yake.

Takwimu zinaonesha kuwa,hadi mwaka wa masomo 2025/26, mfuko huo ulikuwa umeshafadhili jumla ya wanafunzi 100.

Kwa mwaka wa masomo 2026/27, nafasi 10 za ufadhili zimetengwa, ambapo saba ni kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza na tatu kwa wanafunzi wa shahada ya uzamili.

Gavana Tutuba amesema, uwezekano wa kuongeza idadi ya wanufaika upo endapo mfuko utaendelea kuimarishwa kifedha na kupata vyanzo zaidi vya mapato.

Amesema,sehemu ya fedha zinazotumika kugharamia ufadhili huo hutokana na mapato yanayopatikana kupitia uwekezaji wa fedha za mfuko katika hati fungani.

HESLB YAPEWA JUKUMU

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt.Bill Kiwia amesema, jukumu la kusimamia mchakato wa ufadhili huo ni heshima kubwa kwa taasisi hiyo na ni ishara ya imani iliyowekwa na BoT katika uwezo wa HESLB.

Dkt.Kiwia amesema, ushirikiano huo unaonesha namna taasisi za Serikali zinavyoweza kutumia mifumo na uwezo wao kwa pamoja ili kuboresha huduma kwa Watanzania.

“Leo historia inaandikwa. Bodi ya Mikopo imekabidhiwa jukumu la kutangaza na kupokea maombi ya ufadhili kwa ajili ya vijana wetu wa Kitanzania,”amesema.
Amesema,HESLB imewekeza zaidi ya dola milioni tano katika kujenga na kuimarisha mifumo yake ya kidijitali inayowezesha usimamizi wa mchakato mzima wa mikopo na ufadhili wa wanafunzi.

Miongoni mwa mifumo hiyo ni Mfumo wa Usimamizi wa Maombi Mtandaoni (OLAMS), unaotumika kupokea na kuchakata maombi ya wanafunzi.

Dkt.Kiwia amesema,mfumo mwingine ni Integrated Loan Management System (ILMS), unaowezesha kufuatilia mwanafunzi kuanzia anapoanza masomo, anapoendelea na masomo hadi anapohitimu na kuanza kurejesha mkopo.

Amesema,HESLB pia imejenga mfumo wa kidijitali wa utoaji fedha kwa wanufaika pamoja na mfumo wa malipo ya marejesho unaounganishwa na Serikali e-Payment Gateway (GePG).

Pia,amesema taasisi hiyo imefikia kiwango cha takribani asilimia 98 cha matumizi ya mifumo isiyohitaji karatasi katika shughuli zake, jambo linalorahisisha utunzaji wa nyaraka na uchakataji wa taarifa.

Dkt.Kiwia amesema,HESLB imewezesha zaidi ya Watanzania milioni moja kupata elimu ya juu kupitia mikopo, huku zaidi ya Shilingi trilioni 9 zikitolewa kwa wanufaika.

Amesema,bodi hiyo pia imeendelea kusimamia programu nyingine za ufadhili, ikiwemo Samia Scholarship ambayo tangu ilipoanzishwa mwaka 2022 imewanufaisha zaidi ya wanafunzi 2,000 katika fani za Sayansi, Tiba, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati.

Kwa upande wa Mfuko wa Mwalimu Nyerere, amesema,unalenga kuwatambua na kuwaendeleza wanafunzi mahiri wa Kitanzania katika fani ambazo zina umuhimu katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchi.

Amesema,wanafunzi watakaokidhi vigezo watapata ufadhili kamili wa masomo na kwamba maombi yatafanyika kwa njia ya mtandao kupitia mfumo wa OLAMS.

Kwa mujibu wa HESLB, mfumo huo umeunganishwa na mifumo mbalimbali ya Serikali ikiwemo ya Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), NECTA, NAPA na DAWASA, hatua inayolenga kuwezesha uhakiki wa taarifa za waombaji kwa ufanisi zaidi.

MAOMBI KUANZA SEPTEMBA

HESLB imetangaza kuwa,dirisha la maombi ya ufadhili wa Mfuko wa Udhamini wa Kumbukumbu ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa mwaka wa masomo 2026/27 litafunguliwa Septemba 5, 2026 na kufungwa Oktoba 5,2026.

Mfuko huo unatarajiwa kuendelea kuwa sehemu ya jitihada za kukuza vipaji, maarifa na rasilimali watu nchini, huku mabadiliko ya mfumo wa uteuzi yakilenga kuhakikisha fursa za ufadhili zinawafikia wanafunzi wenye sifa kwa njia ya uwazi, usawa na ufanisi ambapo pia utaendelea kusimamiwa na BoT.
Wakati huo huo,Gavana Tutuba amesema,BoT iko tayari kuendelea kuboresha mwongozo huo kulingana na uzoefu utakaopatikana wakati wa utekelezaji pamoja na mahitaji ya jamii na uwezo wa mfuko kuendelea kukua.

Amesisitiza kuwa, lengo kuu ni kuendeleza juhudi za kumuenzi Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kuwekeza katika elimu na kuwaandaa vijana wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya Taifa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here