KILIMANJARO-Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa wa Kilimanjaro imewaokoa watoto wanne wa familia moja wenye umri kati ya miaka 10 na 11 baada ya kubainika kuwa walikuwa wakiishi bila uangalizi wa wazazi tangu Februari,mwaka huu katika Mtaa wa Relini uliopo Kata ya Bomambuzi ndani ya Manispaa ya Moshi.
Watoto hao walikutwa Agosti 14,2026 wakiishi katika mazingira magumu na kutegemea msaada wa chakula kutoka kwa majirani ambapo wawili kati yao, wanafunzi wa darasa la tatu walikuwa wameacha shule.
Aidha,kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa, wazazi wa watoto hao waliondoka kwenda kufanya shughuli za kilimo Simanjiro mkoani Manyara na kuwaacha watoto hao bila uangalizi wa mzazi.
Wakili wa Serikali Mkoa wa Kilimanjaro na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria Mkoa huo, Bi.Tamari Mndeme amesema, kamati hiyo ilibaini kuwa watoto hao walikuwa wakiishi katika mazingira magumu na yasiyo salama.
“Watoto hawa bado wanahitaji kulelewa na kuelekezwa, lakini wameachwa wanajisimamia wenyewe, wazazi wameacha kutekeleza wajibu na majukumu yao ya msingi kwa watoto jambo ambalo ni kinyume cha sheria,"amesema Bi. Tamari Mndeme.
Naye Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Kilimanjaro, Sajenti Mwajabu Mzee amesema,mtoto hawezi kujisimamia mwenyewe na kwamba wazazi wana wajibu wa kuhakikisha watoto wanapata malezi na ulinzi unaostahili.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Kilimanjaro, Bi. Scolastica Swai ametoa wito kwa wazazi kutekeleza wajibu wao wa malezi na kuhakikisha watoto wanapata ulinzi na usalama, akisisitiza kuwa jamii haiwezi kuchukua nafasi ya mzazi katika kumlea mtoto wake.
Watoto hao wamechukuliwa na kupelekwa katika eneo salama huku ufuatiliaji wa wazazi wao ukiendelea.
Tags
Habari
Kamati ya Ushauri wa Kisheria
Kamati Yaokoa Watoto
Kilimanjaro
Malezi kwa Watoto Tanzania
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
