DODOMA-Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wameshiriki katika bonanza maalumu la uzinduzi wa michezo ya SHIMIWI lililofanyika Agosti 15,2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari John Merlin jijini Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Katibu wa Michezo,Bw.Abdallah Mohamed ameushukuru uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuwawezesha Watumishi kushiriki katika bonanza hilo na michezo kwa ujumla.“Tunaushukuru Uongozi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutuwezesha na kutupa nafasi ya kuweza kushiriki Bonanza na michezo ya SHIMIWI kwa ujumla,"amesema Bw. Abdallah.
Aidha,bonanza hilo la uzinduzi wa Michezo ya SHIMIWI limehusisha mbio nyepesi, mpira wa miguu, mpira wa pete na kuvuta Kamba.
Mgeni rasmi katika bonanza hilo alikuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi,Bw.Juma Mkomi akimuwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Balozi, Dkt. Moses Mpogole Kusiluka.
Bonanza hilo ni kiashiria cha maandalizi ya Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) inayotarajiwa kufanyika kuanzia Septemba 20,2026 mkoani Kilimanjaro.








