PWANI-Wilaya ya Kisarawe inaendelea kujijenga kuwa kitovu cha uzalishaji wa baruti na vilipuzi nchini, kufuatia kuanzishwa kwa viwanda viwili vinavyolenga kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo ndani ya nchi na kupunguza utegemezi wa uagizaji kutoka nje.
Viwanda hivyo ni Ideal Detonators Tanzania Limited, kinachotarajiwa kuwa miongoni mwa viwanda vikubwa vya aina hiyo katika Ukanda wa Afrika Mashariki, na Solar Intracom Chemicals Limited.Ideal kina uwezo wa kuzalisha tani 84,000 za baruti na vipande 50,000 vya vilipuzi kwa mwaka, huku Solar kikiwa na uwezo wa kuzalisha tani 25,000 za baruti na vipande 15,000 vya vilipuzi kwa mwaka.
Akizungumza wakati wa ziara yake wilayani Kisarawe iliyolenga kukagua shughuli za madini, kufahamu changamoto za wawekezaji na kufuatilia utekelezaji wa miradi, Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, alisema uwepo wa viwanda hivyo utasaidia kuongeza upatikanaji wa baruti na vilipuzi vinavyohitajika katika shughuli za migodi na matumizi mengine nchini.
Alisema mahitaji ya baruti nchini yanakadiriwa kufikia wastani wa tani 79,548.22 kwa mwaka, pamoja na vipande 29,663.17 vya vilipuzi, hivyo uwekezaji huo ni muhimu kwa kuwa utaongeza uzalishaji wa ndani.
Dkt. Kiruswa alisema uwekezaji huo unaonesha utekelezaji wa dhana ya uongezaji thamani madini, kwa kuwa Tanzania inalenga siyo tu kuchimba madini, bali pia kuzalisha bidhaa zinazohitajika katika shughuli za uchimbaji hapa nchini.
“Baruti ni miongoni mwa bidhaa muhimu katika shughuli za madini, kwani huwezesha wachimbaji kuyafikia madini. Uzalishaji wa bidhaa hizi hapa nchini utaongeza upatikanaji wake na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje,” alisema Dkt. Kiruswa.
Kuhusu changamoto ya soko la ndani iliyowasilishwa na Solar Intracom Chemicals, Dkt. Kiruswa alisema Wizara inalichukua suala hilo kwa uzito na italishughulikia kwa kushirikiana na wadau, ili kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinapata soko na viwanda vinaendelea kuzalisha.
Alisema ikiwa Serikali imeweza kushughulikia changamoto zilizowahi kujitokeza katika sekta nyingine za uzalishaji ikiwemo chumvi, hivyo ina imani kuwa changamoto zinazokabili uzalishaji wa baruti na vilipuzi nazo zitapatiwa ufumbuzi.
Vilevile, kuhusu changamoto ya vifaa kukaa bandarini kwa muda mredu iliyowasilishwa na kampuni ya Ideal Detonators, Dkt. Kiruswa alisema Serikali italifanyia kazi suala hilo kwa kushirikiana na mamlaka husika.
Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Lameck Gabote, alisema Tanzania ina jumla ya viwanda vinane (8) vidogo na vya kati vinavyozalisha wastani wa tani 49,000 za baruti na vipande 950,000 vya vilipuzi kwa mwaka.
"Pamoja na uzalishaji huo, bado haukidhi mahitaji ya matumizi ya baruti katika migodi nchini kwa mwaka. Kwa Mkoa wa Pwani una jumla ya viwanda vinne (4) vya kuzalisha baruti, ambapo viwili (2) kati yake vipo Wilaya ya Kisarawe," alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Mhe. Petro Maguti, alisema wilaya hiyo iko tayari kwa mapinduzi makubwa ya viwanda, akibainisha kuwa Ideal Detonators ni miongoni mwa viwanda vikubwa vya aina hiyo katika Ukanda wa Afrika Mashariki, kikiwa na uwekezaji wa zaidi ya Shilingi bilioni 15.
Alisema Kisarawe inatarajia kupokea viwanda vingine vinne vinavyolenga kuzalisha bidhaa mbalimbali, ikiwemo nondo, spika na viwanda vya kutotolesha kuku.
“Kisarawe ina madini ya viwandani na ujenzi, maeneo ya kujenga viwanda, umeme, maji na miundombinu wezeshi ya usafirishaji. Tuko tayari kupokea uwekezaji zaidi,” alisema Mhe. Maguti.Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na viwanda hivyo, kila kimoja tayari kimetoa ajira kwa takribani Watanzania 250, hivyo kuongeza fursa za ajira na shughuli za kiuchumi Wilayani Kisarawe.
Kiwanda cha Solar Intracom Chemicals Limited kilizinduliwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, na kuanza uzalishaji Agosti 14, 2026, huku Kiwanda cha Ideal Detonators Tanzania Limited kikitarajiwa kuanza uzalishaji Septemba 2026.






