Kwa nini,Mwinjilisti Temba alitabiri kujiuzulu kwa Makamu wa Rais na Yanga kutwaa ubingwa tena?

NA DIRAMAKINI

MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt. Alphonce Boniface Temba amevuta hisia za umma baada ya utabiri alioutoa Julai 21,2026 kuhusu kuondoka madarakani kwa mmoja wa Makamu wa Rais katika nchi za Afrika Mashariki, ambao umeibuka tena baada ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi, kutangaza kujiuzulu Agosti 25,2026.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Balozi Dkt.Emmanuel John Nchimbi ambaye ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Septemba, mwaka huu.

Katika video aliyorekodi usiku wa Julai 21, 2026 akiwa katika chumba chake cha maombi jijini Dar es Salaam, Dkt.Temba alisema,amepokea ujumbe wa kiroho kuhusu kuondoka kwa mmoja wa Makamu wa Rais katika nchi ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa maelezo yake, Dkt.Temba alichokiona hakikumaanisha moja kwa moja kwamba kiongozi huyo angejiuzulu, bali angeweza pia kutofautiana na Serikali au kuamua kwenda kivyake tofauti na kiongozi wa nchi pamoja na Baraza la Mawaziri.

“Roho wa Mungu amenionesha kwamba kuna Makamu wa Rais katika nchi ya Afrika Mashariki anaondoka katika uwepo. Mimi nimeoneshwa na Mungu akiondoka katika uwepo wa Serikali,”alisema Dkt.Temba katika video hiyo.

Aliongeza kuwa, hali hiyo ingeweza kutokea kutokana na kutofautiana kati ya Makamu huyo wa Rais na Serikali yake, huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kuombea amani katika nchi za Afrika Mashariki. "Inawezekana hasitoke katika Serikali kwa maana ya kujiuzulu, labda akawa ametofautiana na Serikali,” alisema.

Hata hivyo, baada ya Balozi Dkt. Nchimbi kutangaza kujiuzulu Agosti 25, 2026, kauli hiyo ya Dkt.Temba imeanza kusambaa na kujadiliwa upya kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na ukweli kwamba utabiri huo ulitolewa zaidi ya mwezi mmoja kabla ya tangazo la kujiuzulu.

Ninaendelea kuombea amani

Katika utabiri wake, Dkt. Temba hakutaja jina la nchi wala jina la Makamu wa Rais aliyekuwa akimzungumzia. Badala yake, alitumia maelezo ya jumla akisema ni nchi mojawapo ya Afrika Mashariki.

Alisema,licha ya mabadiliko hayo, alichooneshwa kilihusisha kuendelea kuwepo kwa amani, huku akitoa wito kwa waumini na Watanzania kuendelea kuliombea eneo hilo.“Lakini, kutakuwa na amani na amani itaendelea kuwepo,” alisema.

Kwa mtazamo huo, ujumbe wake uliwasilishwa zaidi kama wito wa maombi kuliko tangazo la kisiasa, huku akisisitiza kwamba lengo lake lilikuwa kuhakikisha tukio lolote litakalotokea halisababishi athari kwa amani ya Tanzania au mataifa mengine ya Afrika Mashariki.

Yanga kutwaa ubingwa tena

Mbali na suala la Makamu wa Rais, Dkt.Temba alitumia ujumbe huo huo kuelezea jambo lingine alilodai kuoneshwa kiroho kuhusu hatima ya mbio za ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2026/2027.

Katika kauli yake, Dkt. Temba alitabiri kuwa Yanga SC itatwaa tena ubingwa wa Ligi Kuu, licha ya yeye kujitambulisha kuwa shabiki wa Simba SC.

“Mimi ni mpenzi wa Simba, si yale mapenzi sana ya kindakindaki, lakini nimeoneshwa na roho wa Mungu kuwa timu ya Yanga inaenda kushinda tena kombe ambalo wanalo sasa hivi,” alisema.

Dkt. Temba alidai kuwa utabiri huo unatokana na kile alichokiona kupitia Roho Mtakatifu na akasisitiza kwamba alikuwa akisema jambo hilo mapema kabla ya msimu mpya kuanza.

Kwa namna hiyo, alitoa utabiri ambao unagusa moja kwa moja ushindani mkubwa wa soka nchini kati ya Yanga na Simba, huku akiwaacha mashabiki wa timu hizo kusubiri kama kile alichokisema kitatimia mwishoni mwa msimu.

Kwa nini Yanga?

Katika sehemu nyingine ya ujumbe wake, Dkt. Temba alikiri kwamba hata kwake ilikuwa vigumu kueleza kwa nini alioneshwa Yanga badala ya timu nyingine.

“Kwa nini Yanga? Mungu anaweza kuzungumza chochote,” alisema. Alitumia mifano mbalimbali ya kibiblia kueleza kwamba, kwa mtazamo wa imani, njia za Mungu haziwezi kutabirika kwa mantiki ya kibinadamu.

Alirejea simulizi ya Mfalme Nebukadneza katika Biblia, ambaye alielezwa kuwa aligeuzwa na kuishi kama mnyama kwa kipindi cha miaka saba, pamoja na simulizi ya Musa na tukio la maji kutoka mwambani, akitumia mifano hiyo kusisitiza kwamba mambo ya kiroho yanaweza kutokea kwa namna ambayo mwanadamu hawezi kuyatabiri kwa urahisi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here