Makachero wamnasa Msomalia jijini Nairobi akisafirisha Drone kwenda nchini Somalia

NA DIRAMAKINI

POLISI nchini Kenya wamemkamata mwanaume mmoja jijini Nairobi baada ya kubaini kifurushi kilichokuwa na ndege isiyo na rubani (drone) iliyovunjwavunjwa pamoja na vifaa vyake katika kampuni ya usafirishaji mizigo eneo la Eastleigh.
PICHA NA MTANDAO.

Kwa mujibu wa Hiraan Online, mamlaka zimeanza uchunguzi kuhusu kifurushi hicho, ambacho kwa mujibu wa taarifa za awali kinadaiwa kuwa kilikuwa kikisafirishwa kuelekea nchini Somalia kupitia maeneo ya mpakani.

Mtuhumiwa,Mohamud Hared alikamatwa Ijumaa baada ya kufika katika kampuni hiyo ya usafirishaji kuchukua kifurushi kilichodaiwa kutumwa kutoka China na mtu aliyetajwa kwa jina la Abdi Kafi.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, kampuni hiyo ilianza kuwa na mashaka baada ya kubaini kuwa kifurushi hicho kilikuwa kimefungwa kwa umakini mkubwa, huku mtumaji akiwa hajataja aina ya bidhaa zilizokuwa ndani yake.

Hared anadaiwa kulipia gharama za usafirishaji kupitia huduma ya M-Pesa, kabla ya kuwaomba wafanyakazi wa kampuni hiyo kufungua kifurushi hicho.

Baada ya kufunguliwa, walibaini kuwa ndani kulikuwa na drone iliyokuwa imevunjwavunjwa pamoja na vifaa mbalimbali vinavyohusiana na matumizi yake.

Kampuni hiyo ilitoa taarifa kwa polisi, ambao walifika eneo la tukio na kumkamata Hared kabla ya kumpeleka katika Kituo cha Polisi cha Pangani kwa ajili ya mahojiano na uchunguzi zaidi.

Polisi wameeleza kuwa,wakati wa mahojiano ya awali, Hared aliwaambia wachunguzi kuwa drone hiyo ilikuwa ikipelekwa Balad Hawo, mji uliopo mpakani mwa Kenya na Somalia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kifurushi hicho kilitarajiwa kusafirishwa kupitia Mandera, kabla ya kuchukuliwa na mtu aliyetajwa kwa jina la Yussuf Abdi Abdille anayedaiwa kuwa mkazi wa eneo la mpakani.

Hata hivyo, polisi hawajatoa uthibitisho kuhusu matumizi yaliyokusudiwa ya drone hiyo wala iwapo kifaa hicho kilikuwa na uhusiano na shughuli yoyote ya uhalifu.

Hared anaendelea kushikiliwa na polisi wakati uchunguzi ukiendelea kuhusu chanzo cha kifurushi hicho, waliohusika katika usafirishaji wake, mpokeaji aliyekusudiwa na matumizi ambayo drone hiyo ilipaswa kufanyiwa.

Tukio hilo limeibua wasiwasi zaidi kuhusu usafirishaji wa vifaa vya kiteknolojia kupitia njia zisizo rasmi, hasa katika maeneo ya karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.

Mamlaka za Kenya zimeendelea kuimarisha udhibiti wa uingizaji na usafirishaji haramu wa vifaa vinavyoweza kutumika katika mashambulizi au shughuli nyingine za uhalifu.

Hata hivyo, polisi hawajasema iwapo kifurushi hicho kinahusishwa na kundi lolote la wapiganaji au mpango wowote wa shambulio.

Uchunguzi unaendelea ili kubaini madhumuni halisi ya usafirishaji wa drone hiyo, pamoja na watu wengine wanaoweza kuwa sehemu ya mtandao wa usafirishaji huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here