NA DIRAMAKINI
SHIRIKA la Marekani la Biashara na Maendeleo (USTDA) linatarajia kuandaa ziara ya ujumbe wa viongozi na wataalamu wa sekta ya umeme kutoka Angola, Botswana, Msumbiji na Zambia nchini Marekani ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga ushirikiano wa kimkakati katika kulinda na kuboresha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme Kusini mwa Afrika.
Ujumbe huo unatarajiwa kuwa na takribani wawakilishi 15 kutoka serikalini na sekta binafsi, ambapo utakuwa nchini Marekani kuanzia Agosti 29 hadi Septemba 5, 2026 na utatembelea miji ya Denver,Colorado,Austin na Texas.
Ziara hiyo inalenga kuwaunganisha watoa maamuzi wa sekta ya nishati kutoka nchi hizo na kampuni za Marekani, pamoja na kuwawezesha kuona na kujifunza kuhusu teknolojia za kisasa zinazoweza kutumika kuboresha mifumo ya usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Pia,katika ziara hiyo, wajumbe watakutana na kampuni mbalimbali za Marekani na kushuhudia maonesho ya teknolojia za kisasa zinazoweza kusaidia kuboresha mitandao ya usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Kwa mujibu wa USTDA, teknolojia hizo zinajumuisha mifumo ya udhibiti wa gridi inayotumia akili unde (AI) ambayo inaweza kusaidia katika kuimarisha ufanisi, uthabiti na usalama wa mifumo ya umeme.
Aidha, ujumbe huo unatarajiwa kukutana na mashirika ya huduma za umeme yanayomilikiwa na Serikali pamoja na yale ya sekta binafsi pamoja na taasisi za udhibiti wa nishati.
Miongoni mwa taasisi zitakazokutana na ujumbe huo ni Tume ya Huduma za Umma ya Colorado (Colorado Public Utilities Commission) na Baraza la Uaminifu wa Usambazaji Umeme la Texas (Electric Reliability Council of Texas).
USTDA pia inapanga kuandaa mkutano wa wazi wa kibiashara mjini Denver siku ya Septemba 1, 2026, utakaowapa kampuni za Marekani fursa ya kupata taarifa moja kwa moja kutoka kwa wajumbe hao kuhusu fursa zinazotarajiwa katika miradi ya nishati katika nchi zao.
Mkutano huo pia utatoa nafasi kwa kampuni hizo kukutana ana kwa ana na wajumbe kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara na kuwasilisha suluhisho zao za kiteknolojia zinazolenga kuimarisha usalama wa mifumo ya gridi za umeme.
Kwa USTDA, ushirikiano huo unaweza kufungua milango kwa kampuni za Marekani kushiriki katika miradi ya miundombinu ya nishati inayotarajiwa kutekelezwa katika eneo hilo.
Mahitaji ya miundombinu ya umeme katika Kusini mwa Afrika yanaendelea kuongezeka kutokana na kasi ya ukuaji wa idadi ya watu, ukuaji wa miji na kuongezeka kwa uzalishaji wa viwandani.
Ukuaji wa sekta ya uchimbaji wa madini muhimu kwa uchumi wa dunia pia unaongeza mahitaji ya nishati, hali inayoweka msukumo zaidi kwa nchi za eneo hilo kuwekeza katika mifumo ya kisasa, salama na yenye uwezo wa kusafirisha na kusambaza umeme kwa ufanisi.
Wapangaji wa nishati na taasisi za umeme katika eneo hilo wanaendelea kuweka kipaumbele katika miradi mikubwa ya kuunganisha mifumo ya umeme ya nchi mbalimbali pamoja na kufanya maboresho ya miundombinu iliyopo.
Hatua hizo zina umuhimu katika kuongeza uwezo wa nchi kuzalisha, kusafirisha na kusambaza umeme, huku pia zikisaidia kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa nishati katika maeneo yenye mahitaji makubwa ya kiuchumi.
Kwa mujibu wa USTDA, sekta binafsi ya Marekani iko katika nafasi nzuri ya kushiriki katika juhudi hizo kwa kutoa teknolojia, utaalamu wa uhandisi na vifaa vya kisasa vinavyoweza kusaidia kuboresha mifumo ya gridi za umeme katika eneo la Kusini mwa Afrika.
Vilevile,Marekani inajiona kuwa miongoni mwa vinara katika teknolojia za kisasa za usambazaji wa nishati, ambazo zina nafasi muhimu katika kufanya mifumo ya umeme kuwa thabiti, yenye ufanisi na salama zaidi.
Ziara hiyo ya ujumbe kutoka Angola, Botswana, Msumbiji na Zambia inatarajiwa kuwa jukwaa la kuimarisha uhusiano kati ya taasisi za nishati za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na sekta binafsi ya Marekani, sambamba na kutengeneza fursa mpya za uwekezaji na biashara katika miundombinu ya umeme.
Tags
Angola
Botswana
Habari
Kimataifa
Marekani
Msumbiji
Sekta ya Umeme
USTDA
Wataalamu wa Nishati
Wataalamu wa Umeme
Zambia
