PWANI-Kutokana na kuongezeka kwa Kasi ya uwekezaji ya shughuli za uongezaji thamani madini nchini huku ikizidi kujifungamanisha zaidi na sekta nyingine za uchumi, Sekta ya Madini imeendelea kuweka Msingi wa kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ya kujenga uchumi wa Dola Trilioni 1, kupitia viwanda.
Hayo yalibainishwa Agosti 19, 2026 wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, Wilayani Mkuranga iliyolenga kufuatilia shughuli za madini, kubaini changamoto na kutoa maelekezo muhimu.
Katika ziara hiyo , Dkt. Kiruswa alitembelea viwanda vikubwa vya KEDA Tanzania Float Glass kinachozalisha vioo kwa ajili ya maghorofa, magari na matumizi mbalimbali, pamoja na Kiwanda cha GoodWill Ceramic Co.Ltd kinachozalisha vigae vya sakafu na ukutani pamoja na vifaa vya usafi wa majumbani na vyooni na kueleza kuwa, ni jambo la kujivunia kuona Tanzania inaweza kuzalisha bidhaa zinazoweza kuuzwa kwenye mataifa makubwa duniani kama Marekani.
Dkt.Kiruswa alisisitiza uzingatiaji wa bei elekezi zinazotolewa na Serikali kwa madini yanayotumika viwandani, pamoja na kumuagiza Afisa Madini Mkazi Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kwa kushirikiana na Wilaya hiyo kuandaa semina kwa wamiliki wa viwanda na leseni za uchimbaji kuhusu uwajibikaji kwa jamii, utunzaji wa mazingira na masuala mengine ya msingi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mkuranga, Mhe. Hadija Nasri Ally, alisema Wilaya hiyo inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa uwekezaji, ikiwemo kutenga ekari 15 kwa ajili ya ujenzi wa Bandari Kavu itakayorahisisha uhifadhi na usafirishaji wa bidhaa zinazozalishwa wilayani humo,
Alisema,Mkuranga ina viwanda 275, ambapo 39 vinatumia madini kuzalisha bidhaa mbalimbali, huku shughuli za madini zikichangia shilingi bilioni 3.2 katika mwaka wa fedha 2025/26.
Naye, Meneja Biashara wa KEDA Tanzania, Ruby Zhu, alieleza kuwa, asilimia 98 ya malighafi ya kiwanda hicho inatoka Mkuranga, huku kiwanda kikizalisha takribani tani 600 za vioo kwa siku, vinavyosafirishwa katika masoko mbalimbali duniani ikiwemo Marekani.
Kwa upande wake, Meneja Biashara wa GoodWill, Justin Xie alieleza kwamba, asilimia 90 ya malighafi zinazotumiwa na kiwanda hicho zinatoka Tanzania na kuongeza kuwa, kampuni hiyo imepanua uzalishaji wa bidhaa za majumbani, ikiwemo sinki za kunawia, vifaa vya vyooni na bafu huku bidhaa zao zikiuzwa mataifa mbalimbali ikiwemo nchi za Ulaya na Marekani.
Kuhusu ajira, Xie alisema kiwanda kimetoa ajira za moja kwa moja kwa watanzania zipatazo 3,000 na zisizo za moja kwa moja 12,000.
"Tumeweka mizizi nchini Tanzania, tunaweza kujitolea kubadilisha rasilimali za madini za ndani kuwa bidhaa za usafirishaji nje zenye thamani kubwa, na kuleta ajira zaidi na kodi na kushiriki na idara zote kuzungumzia vizuizi katika mnyororo wa usambazaji wa madini, na kwa pamoja kuendeleza ujenzi wa viwanda nchini Tanzania," alisema Justin Xie.
Kwa mujibu wa Afisa Madini wa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Lameck Gabote, Mkuranga ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa madini ya ujenzi na viwandani yanayohudumia kwa kiasi kikubwa Mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani.
Tags
Dr Steven Kiruswa
GoodWill Ceramic Co.Ltd
Habari
KEDA Tanzania
Sekta ya Madini Tanzania
Wizara ya Madini Tanzania











