DAR-Mkurugenzi wa Kitengo cha Diaspora, Ushirikishwaji na Fursa,Bw. Salvator Marcus Mbilinyi amefanya mazungumzo na Uongozi wa TIB Rasilimali uliowakilishwa na Bw.Lameck Mavipya, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo.
Mazungumzo hayo yalifanyika jijini Dar Es Salaam hivi karibuni yalilenga kuitambulisha Kampuni ya TIB Rasilimali kwa ambayo ndio wakala pekee wa serikali katika uwekezaji wa Mitaji ya umma pamoja na Hati Fungani katika soko la Hisa DSE.
Kwa upande wa TIB Rasilimali iliwasilisha huduma na bidhaa mbalimbali inayojihusisha nazo kwa niaba ya Serikali, lengo likiwa ni kufikia soko la Diaspora wa Tanzania duniani ambao ni moja ya wadau muhimu katika sekta ya uwekezaji katika soko la hisa.
Kwa upande wa Wizara, Bw. Mbilinyi alitoa maelezo ya masuala mbalimbali ya kisera na kisheria kuhusu diaspora na kuonesha fursa ambazo mashirika ya umma na binafsi wanaweza kuzipata kupitia diaspora wa Tanzania duniani.
Bw. Mbilinyi amewahakikishia ushirikiano TIB Rasilimali huku akitoa wito kwa Kampuni hiyo kutafuta fursa zaidi za kuelimisha jamii kuhusu kazi zao na masuala mazima ya uwekezaji katika soko la hisa, elimu ambayo bado haijatiliwa mkazo wa kutosha kwa watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje pamoja na Diaspora kwa ujumla wao.
Bw. Mavipya aliongozana na ujumbe wake ambao ni Bw. James M Manyama - Mkuu wa Huduma Mbadala za Kifedha, na Bw. Peter Msafiri ni Afisa Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano.
