NA DIRAMAKINI
MAMLAKA nchini Iraq zimetangaza kukamata fedha taslimu zenye thamani ya zaidi ya Dola milioni 26 za Marekani (zaidi ya Shilingi bilioni 67 za Tanzania) pamoja na zaidi ya kilo 60 za dhahabu.
Ni katika operesheni ya kupambana na rushwa inayowalenga maafisa wakuu wa serikali wanaotuhumiwa kuhusika na ubadhirifu wa fedha za umma.
Kwa mujibu wa tovuti ya The National, mali hizo zilinaswa katika uchunguzi unaomhusu aliyekuwa Naibu Waziri wa Mafuta anayeshughulikia masuala ya usafishaji wa mafuta, Adnan Al Jumaili ambaye pia aliwahi kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Northern Refineries.
Imeelezwa kuwa, dola milioni 20.34 taslimu, kilo 60 za dhahabu pamoja na magari saba vilikamatwa kama sehemu ya mali zinazohusishwa na Al Jumaili.
Al Jumaili alikamatwa mwezi Mei,mwaka huu katika uchunguzi unaohusu tuhuma za ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha katika miradi ya ujenzi na uboreshaji wa mitambo ya kusafisha mafuta iliyokuwa chini ya Wizara ya Mafuta.
Baraza Kuu la Mahakama nchini Iraq limesema, Jaji wa Uchunguzi wa Mahakama Kuu ya Jinai ya Kupambana na Rushwa aliratibu operesheni hiyo kwa kushirikiana na mamlaka katika eneo la Kurdistan,Kaskazini mwa Iraq.
Mahakama hiyo haikutoa maelezo zaidi kuhusu mahali mali hizo zilipatikana, lakini imeeleza kuwa,uchunguzi unaendelea ili kubaini wahusika wengine wanaodaiwa kuhusika katika mtandao huo.
Jaji anayesimamia uchunguzi amesema hatua za ufuatiliaji na uchunguzi zilizochukuliwa kwa lengo la kukamata mapato yanayodaiwa kutokana na ubadhirifu katika miradi iliyotekelezwa na watuhumiwa na washirika wao zilisababisha kupatikana kwa fedha, vito vya dhahabu na magari hayo
Amesema,uchunguzi na msako dhidi ya watu wengine wanaodaiwa kuhusika unaendelea hadi taratibu zote za kisheria zitakapokamilika.
Pia,waendesha mashtaka wanadai kuwa,baadhi ya mikataba na fedha zilizotengwa kwa ajili ya kuboresha na kuendesha mitambo ya kusafisha mafuta zilielekezwa kinyume cha madhumuni kupitia mtandao wa kampuni na watu waliokuwa wakifanya kazi kama wasuluhishi.
Kukamatwa kwa fedha na dhahabu katika maeneo mbalimbali ya Baghdad na Erbil kunaashiria kuwa wachunguzi wanafuatilia mali zinazodaiwa kuhamishwa kati ya Serikali Kuu ya Iraq na eneo linalojitawala la Kurdistan.
Al Jumaili aliondolewa katika wadhifa wake baada ya tuhuma za rushwa dhidi yake kuwekwa hadharani na kwa sasa anaendelea kushikiliwa akisubiri hatua zaidi za kisheria na kesi yake.
Naibu Waziri wa Umeme naye akamatwa
Katika tukio jingine lililotangazwa siku hiyo hiyo, Tume ya Uadilifu ya Iraq imesema imefanikiwa kurejesha takribani dola milioni 5.84 taslimu pamoja na dinari bilioni 1.175 za Iraq sawa na karibu dola 770,000.
Mali hizo, ambazo pia zilijumuisha dhahabu, zilikutwa nyumbani kwa Khalid Khazaie Attiyah, aliyekuwa Naibu Waziri wa Umeme anayeshughulikia usafirishaji na usambazaji wa umeme.
Attiyah alikamatwa Ijumaa katika hatua nyingine ya kampeni hiyo ya kupambana na rushwa.
Mfululizo huo wa operesheni unaonesha kuongezeka kwa msako wa serikali dhidi ya maafisa wanaotuhumiwa kutumia vibaya madaraka yao na kuhusika katika ubadhirifu wa mali za umma.
Hatua hizo zinakuja wakati serikali ya Waziri Mkuu Ali Al Zaidi ikiongeza kasi katika kampeni yake ya kupambana na rushwa, ambayo imepewa nafasi kubwa katika juhudi za kurejesha imani ya wananchi na kulinda rasilimali za taifa.
Tangu kuingia madarakani mwezi Mei, Al Zaidi ameagiza mfululizo wa misako, kukamatwa kwa maafisa wakuu na kuzuiwa kwa mali zinazodaiwa kupatikana kwa njia zisizo halali katika wizara mbalimbali ikiwemo Wizara ya Mafuta na Wizara ya Umeme.
Serikali imekuwa ikiwasilisha kampeni hiyo kama mtihani wa uwezo wa dola kusimamia rasilimali na taasisi zake, hasa katika sekta ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikihusishwa na ushawishi wa vyama vya kisiasa na mitandao yenye nguvu kiuchumi.
Mahakama za Iraq, ambazo tayari zimeanzisha mahakama maalumu za kushughulikia kesi za rushwa, zimesema zinaimarisha ushirikiano na Tume ya Uadilifu, vitengo vya ujasusi wa kifedha pamoja na mamlaka za kikanda katika kufuatilia fedha zinazodaiwa kupatikana kwa njia haramu.
Kwa mujibu wa maafisa wa serikali, lengo la kampeni hiyo si kuwafikisha tu watuhumiwa mbele ya sheria, bali pia kurejesha fedha na mali zilizopatikana kwa njia haramu na kuzirudisha katika mfuko wa serikali.
Hatua hiyo ina umuhimu mkubwa kwa taifa linalokabili shinikizo la kifedha katika kugharamia huduma za umma na miradi ya maendeleo.
Sekta ya mafuta imeendelea kuwa kitovu cha kampeni hiyo kwa sababu ndiyo chanzo kikuu cha mapato ya Iraq. Sekta hiyo imekuwa ikikabiliwa mara kwa mara na tuhuma zinazohusu upotevu wa mapato, magendo, pamoja na mikataba yenye gharama zilizopandishwa isivyo halali.
Suala la usafishaji wa mafuta ni nyeti zaidi kutokana na ukweli kwamba Iraq, licha ya kuwa na akiba kubwa ya mafuta ghafi, bado huagiza kiasi kikubwa cha mafuta yaliyosafishwa kutoka nje.
Hali hiyo imeifanya miradi ya ujenzi, uboreshaji na uendeshaji wa mitambo ya kusafisha mafuta kuwa na uzito mkubwa kisiasa na kiuchumi.
Kwa serikali, kufanikisha hukumu dhidi ya wahusika na kurejesha fedha zinazodaiwa kupotezwa ni muhimu katika kudumisha kasi ya kampeni hiyo na kuonesha kwamba mapambano dhidi ya rushwa yana matokeo yanayoonekana.(NA)
Tags
Dhahabu Kilo 60
Dola Milioni 20.34
Habari
Iraq
Kimataifa
Mafisadi Serikalini
Naibu Waziri wa Mafuta
Naibu Waziri wa Umeme
Wizi Fedha za Umma

