Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kufanya ziara ya kikazi nchini Tanzania

NA DIRAMAKINI

KUFUATIA mwaliko wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) atafanya ziara ya kikazi nchini tarehe 17 na 18 Agosti 2026.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wakati wa ziara hiyo, Mhe. Rais Félix Antoine Tshisekedi Tshilombo atafanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Zanzibar.

Mazungumzo yao yanatarajiwa kujikita katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano ikiwemo biashara na uwekezaji, kilimo, madini, nishati, miundombinu na usafirishaji, afya, mawasiliano ya kidijitali, pamoja na masuala ya amani, usalama na mtangamano wa kikanda.

Mara baada ya mazungumzo rasmi, viongozi hao wawili wanatarajiwa kuzungumza na waandishi wa habari katika mkutano wa pamoja kuelezea maazimio yaliyofikiwa katika kuimarisha zaidi uhusiano wa uwili kati ya Tanzania na DRC.

Ziara hii itakuwa ni ziara ya tatu kwa Mhe. Rais Tshisekedi nchini Tanzania, kufuatia ziara zake za awali alizofanya mwaka 2019 na 2022 ambazo zilisaidia kuweka misingi imara ya ushirikiano katika sekta za miundombinu, matumizi ya bandari, biashara na uwekezaji.

Aidha, ziara ya sasa ya Mhe. Rais Tshisekedi inalenga kuimarisha uhusiano wa kihistoria, ya kindugu na ya kidiplomasia kati ya Tanzania na DRC.

Sambamba na kutathmini masuala ya maendeleo, amani, usalama na mtangamano wa kikanda, maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati ya pamoja na hatua zinazochukuliwa kuondoa vikwazo vinavyoathiri biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here