Mwinjilisti Temba aweka wazi unabii kuhusu Makamu wa Rais Dkt.Nchimbi kujiuzulu,atoa tahadhari kuhusu hoteli inayoanza na "S" kuwaka moto Masaki

NA DIRAMAKINI

MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt. Alphonce Boniface Temba amefafanua kauli yake ya kinabii iliyohusu kuondoka kwa Makamu wa Rais ndani ya Afrika Mashariki, akisema maono hayo yalikuwa yakimlenga Makamu wa Rais wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi.
Ameyasema hayo leo Agosti 26,2026 jijini Dar es Salaam katika mahojiano maalum na DIRAMAKINI, baada ya kutaka kufahamu kwa kina kuhusu unabii wake wa mmoja wa Makamu wa Rais kujiuzulu kwa moja ya nchi za Afrika Mashariki alioutoa Julai 21,2026.

Dkt.Temba amesema,awali alitoa unabii huo kwa lugha ya mafumbo bila kutaja moja kwa moja nchi au jina la kiongozi aliyekuwa akimlenga, akieleza kuwa alifanya hivyo kwa kuzingatia namna ambavyo baadhi ya unabii unavyowasilishwa katika maandiko ya Biblia.

Kwa mujibu wa Dkt. Temba, maono hayo yalianza kumjia mara kwa mara tangu mwezi Mei, hali iliyomsukuma kuyaeleza hadharani kwa namna ambayo, kwa mtazamo wake, isingesababisha taharuki au kuonekana kama alikuwa akieleza matukio kwa kuzingatia taarifa za kawaida za kibinadamu.

Amesema,baada ya taarifa kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kujiuzulu na kustaafu siasa kwa Dkt. Nchimbi, alifafanua kuwa kiongozi aliyekuwa akimlenga katika unabii wake alikuwa ni Makamu wa Rais wa Tanzania.

“Kuondoka” alikosema katika unabii huo, Dkt. Temba amefafanua kuwa,hakumaanisha lazima Dkt. Nchimbi angeondoka katika Chama Cha Mapinduzi (CCM) au kujiunga na chama kingine cha siasa, bali alimaanisha kuondoka katika nafasi ya Umakamu wa Rais.

Kwa maana hiyo, amesema Dkt. Nchimbi anaweza kuendelea kuwa mwanachama wa CCM, raia wa Tanzania na kushiriki maisha ya kawaida ya kitaifa, huku akiwa ameondoka katika nafasi ya Umakamu wa Rais.

Dkt. Temba amesema, jambo lililomvutia zaidi ni namna ambavyo mabadiliko hayo yalivyotokea kwa utulivu na bila kusababisha misukosuko mikubwa ya kisiasa, licha ya ukubwa wa nafasi aliyokuwa akiishikilia Dkt. Nchimbi.

Ameilinganisha hali hiyo na matukio yaliyowahi kutokea katika baadhi ya nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, akitaja Malawi na Kenya.

Kwa upande wa Malawi, Dkt. Temba amerejea mgogoro wa kisiasa uliowahi kujitokeza kati ya aliyekuwa Rais Peter Mutharika na aliyekuwa Makamu wa Rais Joyce Banda, akieleza kuwa kuondolewa madarakani kwa Makamu wa Rais kulifuatwa na mvutano wa kisiasa ambao baadaye ulihusisha kuanzishwa kwa chama kingine na safari ya Banda ya kuwania urais.

Aidha, ametaja Kenya, ambako amesema uhusiano kati ya Rais William Ruto na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua uliingia katika mvutano mkubwa kabla ya Gachagua kuondolewa madarakani kupitia mchakato wa kisiasa na kisheria.

Kwa mujibu wa Dkt. Temba, tofauti hiyo inaonekana wazi ikilinganishwa na Tanzania, ambako kuondoka kwa Dkt. Nchimbi katika nafasi ya Umakamu wa Rais kumefanyika bila kiwango cha mvutano kilichoshuhudiwa katika baadhi ya nchi nyingine.

Amesema hali hiyo, kwa mtazamo wake, inaendana na sehemu ya maono aliyoyatoa awali kuhusu “kuondoka” kwa Makamu wa Rais huku amani ikiendelea kutawala nchini.

Dkt. Temba amesisitiza kuwa, lugha ya mafumbo katika unabii wake haikuwa na lengo la kuficha ukweli kwa nia nyingine, bali ilitokana na namna alivyodai kupokea na kutafsiri maono hayo ya kiroho.

Amesema,hata katika Biblia, baadhi ya mafundisho na unabii uliwasilishwa kwa njia ya mifano na mafumbo, akitaja mfano wa Yesu Kristo ambaye mara kadhaa alitumia lugha ya mifano katika kufikisha ujumbe wake.

Atoa wito wa kuendeleza amani

Pamoja na kufafanua unabii huo, Dkt. Temba amesema,kwa sasa anaendelea kuliombea Taifa la Tanzania liendelee kuwa na amani, umoja na mshikamano.
Amesema,anaunga mkono maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan akieleza kuwa, anaona umuhimu wa kuendelea kumuombea Rais katika kutekeleza mipango yenye lengo la kukuza uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania.

Ametoa mfano wa mradi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere kilichopo Rufiji Mkoa wa Pwani, akisema kukamilika na kuanza kwa mradi huo ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu unalenga kuongeza upatikanaji wa umeme nchini.

Kwa mujibu wa Dkt. Temba, upatikanaji wa umeme wa uhakika una umuhimu pia kwa shughuli za taasisi za dini, ambazo zinatumia nishati hiyo katika shughuli mbalimbali za kiroho na uenezaji wa injili.

Amesema,anaendelea kumuombea Rais Samia kutokana na kile alichokiita maono makubwa yenye lengo la kuimarisha ustawi wa Taifa kiuchumi.

Atoa tahadhari kuhusu hoteli Masaki

Katika hatua nyingine, Dkt. Temba amesema amepata maono kuhusu uwezekano wa kutokea kwa moto katika hoteli moja ya kimataifa iliyopo Masaki, Dar es Salaam.

Amesema, katika maono hayo ameiona hoteli hiyo ikiteketea kwa moto, akieleza kuwa jina la hoteli hiyo, kwa mujibu wa maono yake, linaanza kwa herufi “S”.

Dkt. Temba amesema, jengo kubwa la hoteli hiyo, ambalo kwa mujibu wa maelezo yake linaelekea au kugusa eneo la bahari, linaweza kuathiriwa kwa kiwango kikubwa endapo tukio hilo litatokea.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa lengo la kutoa taarifa hiyo si kutangaza kwamba janga hilo lazima litokee, bali kutoa tahadhari ili hatua za kinga zichukuliwe mapema.

Ameutaka uongozi wa hoteli hiyo kukagua mifumo yote ya umeme, hasa nyaya na vifaa vya umeme vinavyoweza kuwa vimechakaa, na kufanya matengenezo au mabadiliko yanayohitajika.

“Ndiyo maana ninawaambia wazi kwamba wajitahidi kuangalia mifumo yao ya umeme na wajitahidi kurekebisha ili kadhia hiyo isitokee,” amesema.

Dkt. Temba amesema, ametoa tahadhari hiyo kutokana na umuhimu wa hoteli hiyo katika uchumi wa Taifa, akieleza kuwa hoteli za kimataifa zina mchango katika kutoa ajira, kuhudumia wageni kutoka nje ya nchi na kuchangia upatikanaji wa fedha za kigeni.

Amesema, iwapo mifumo ya umeme itakaguliwa na hitilafu zinazoweza kusababisha madhara zikarekebishwa mapema, anaamini hatua hiyo inaweza kusaidia kuzuia madhara yanayoweza kujitokeza.

Hata hivyo, tahadhari hiyo ya kinabii inapaswa kuchukuliwa kama wito wa jumla wa kuimarisha usalama wa majengo, hususan ukaguzi wa kitaalamu wa mifumo ya umeme, badala ya kutafsiriwa kama uthibitisho kwamba tukio la moto litatokea.

Dkt. Temba amesisitiza pia umuhimu wa viongozi wa dini na jamii kwa ujumla kuendelea kuliombea Taifa, huku akitoa wito wa kuwepo kwa amani, umoja na mshikamano kwa ajili ya maendeleo ya Tanzania.

Vilevile, Dkt.Temba ameweka wazi kuwa,Mungu ameendelea kumuonesha mara kadhaa kwamba aendelee kumuombea Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini kwani, kuna kusudi maalum aliloliweka ndani yake kwa ajili ya Taifa na Watanzania kwa ujumla.

Wananchi wampongeza Mwinjilisti Temba

Mbali na hayo, wananchi mbalimbali wamempongeza Mwinjilisti wa Kimataifa, Dkt. Alphonce Boniface Temba kwa kazi yake ya kuhubiri Injili, kuombea watu na mataifa, pamoja na ujumbe wa kinabii anaoutoa katika huduma yake, wakisema mchango wake katika masuala ya kiroho unastahili kutambuliwa na kuungwa mkono.

Kwa mujibu wa maoni ya wananchi hao, Dkt. Temba amekuwa akitumia kipawa na wito wake wa kiroho kuwahudumia watu ndani na nje ya Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa kumtegemea Mungu, kuombea jamii na kuendeleza maadili mema katika Taifa.

Wananchi hao,Prosper Justin mkazi wa Ilala, Halima Musa mkazi wa Tegeta, Yusuf Said, Sadick John wa jijini Dar es Salaam wamesema, kazi hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa katika kuwafariji, kuwaunganisha na kuwajengea matumaini watu wanaopitia changamoto mbalimbali za maisha.

Wameeleza pia kuwa huduma za kiroho zinazolenga amani, matumaini na maadili zina nafasi muhimu katika kujenga jamii yenye mshikamano.

Baadhi yao wamependekeza kuwa Serikali na taasisi husika ziangalie namna bora ya kushirikiana na viongozi wa dini na watu wenye huduma za kiroho, akiwemo Dkt. Temba katika maeneo yanayohusu amani, maadili, mshikamano wa kitaifa na ustawi wa jamii.

Wakielezea mtazamo wao, wananchi hao wamesema Serikali inaweza kutumia kwa busara uzoefu na ushawishi wa viongozi wa dini katika kuhamasisha amani, upendo, umoja na maadili miongoni mwa wananchi. Kwa mtazamo wao, ushirikiano huo unaweza kuwa nyenzo ya kuongeza nguvu katika juhudi za kulijenga Taifa.

Aidha, wameeleza kuwa Dkt. Temba amekuwa akifanya huduma za kiinjilisti na maombi katika mataifa mbalimbali barani Afrika, jambo ambalo, kwa maoni yao, linaonesha wigo mpana wa huduma yake na uwezo wa kufikia watu kutoka jamii na mataifa tofauti.

“Tunampongeza kwa kazi anayoifanya kwa ajili ya Mungu na kwa kuendelea kuwahudumia watu kupitia mahubiri, maombi na mafundisho ya kiroho. Tunatamani kuona viongozi wa dini na Serikali wakishirikiana zaidi katika kujenga Taifa lenye amani, maadili na mshikamano,” amesema Halima.

Wananchi hao pia wametoa wito kwa jamii kuendelea kuheshimu na kuthamini mchango wa viongozi wa dini katika malezi ya kiroho na kimaadili, huku wakisisitiza umuhimu wa kutofautisha masuala ya imani na majukumu ya kikatiba ya Serikali.

Kwa upande mwingine, wameeleza kuwa, ujumbe wa kinabii unapaswa kupokelewa kwa busara na kuzingatia misingi ya imani, huku mamlaka za Serikali zikiendelea kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi.

Wameongeza kuwa, endapo kutakuwa na ushirikiano unaozingatia taratibu na misingi ya nchi, viongozi wa dini wanaweza kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kuhamasisha wananchi kuombea Taifa, kudumisha amani na kuendeleza mshikamano wa kitaifa.

Aidha, pongezi hizo zinaakisi mtazamo wa baadhi ya wananchi wanaoona umuhimu wa huduma za kiroho katika jamii na wanataka mchango wa viongozi wa dini, wakiwemo wahubiri wa kimataifa kama Dkt. Alphonce Boniface Temba, uendelee kutumika katika kuhamasisha matumaini, amani, maadili na upendo kwa Taifa na watu wake.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here