ARUSHA-Kamanda wa Polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU) Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Simon Pasua amesema kuwa, watuhumiwa 21 wamekamatwa katika Wilaya ya Longido mkoani Arusha wakitorosha jumla ya mifugo 1,955 kwenda nchi jirani kwa njia za magendo.
Akizungumza leo Agosti 26, 2026 Kamanda huyo amesema kuwa katika kipindi cha mwezi Juni 2026, hadi sasa kikosi hicho katika kwa kushirikiana na Maafisa wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika doria ya pamoja walifanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao ambao walikuwa wakitorosha mifugo kwenda nchi jirani bila ya kuikatia vibali.
Aidha Kamanda huyo amesema kuwa kwa kipindi hicho pia jumla ya watuhumiwa 42 wamekamatwa kwa makosa ya wizi wa mifugo, ambapo watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani huku mmoja akihukumiwa kufungwa miaka mitano jela, wengine kesi zikiwa katika hatua mbalimbali.
Sambamba na hayo (SACP) Pasua amesema kuwa kikosi kimeendelea kutoa elimu ya ushirikishwaji jamii kupitia mikutano ya hadhara na minada ya mifugo, ambapo kwa kipindi hicho wamefanya jumla ya mikutano 305 kote nchini, huku lengo likiwa ni kujenga miundombinu ya amani mapema kabla ya uhalifu haujatokea.
