RUKWA-Timu ya Polisi Mkoa wa Songwe imefanikiwa kutinga hatua ya fainali ya Bonanza la Polisi Jamii Kanda ya Kwanza baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Timu ya Polisi Katavi katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Agosti 09, 2026, katika Viwanja vya Kantalamba, Sumbawanga mkoani Rukwa.
Ushindi huo umeiwezesha Timu ya Polisi Songwe kukutana na Timu ya Polisi Mbeya katika hatua ya fainali, ambapo bonanza hilo linalenga kuandaa timu itakayoiwakilisha Polisi Kanda ya Kwanza katika Mashindano ya Polisi Jamii Cup Kitaifa yanayotarajiwa kufanyika Mkoani Mbeya Agosti 25, 2026.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Mkuu wa Polisi Jamii Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi ( ACP), Maria Kway ameipongeza timu hiyo kwa ushiriki na mafanikio iliyoyapata, huku akiwasisitiza wachezaji hao kuendelea kufanya mazoezi na kudumisha nidhamu, akibainisha kuwa michezo ni muhimu kwa afya, kujenga mshikamano na kuimarisha ushirikiano miongoni mwa askari katika ngazi ya Mkoa,kanda na kitaifa.
Mwisho, ACP Kway aliwasisitiza wachezaji hao kushinda mchezo wa fainali dhidi ya Polisi Mbeya, na hivyo kuendeleza heshima na mafanikio ya Timu ya Polisi Mkoa wa Songwe katika michezo.



