NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Makamu wa Rais mpya,Deogratius John Ndejembi kutekeleza majukumu yake kwa utii, uaminifu, uzalendo, utu, busara, hekima na maarifa, akitanguliza maslahi ya Taifa na ustawi wa Watanzania.
Ameyasema hayo leo Agosti 29,2026 katika hafla ya kumuapisha Ndejembi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyofanyika Ikulu ya Chamwino,Dodoma.
Katika hotuba yake baada ya kiapo hicho, Rais Dkt.Samia amesema,nafasi ya Makamu wa Rais si cheo cha kujivunia bali ni dhamana kubwa inayotolewa kwa ajili ya kuwatumikia wananchi na kulinda maslahi mapana ya Taifa.
Amemtaka Ndejembi kutumia dhamana hiyo kwa kuwatumikia Watanzania wote bila kujali tofauti zao, huku akihakikisha kila jukumu atakalokabidhiwa linatekelezwa kwa ufanisi na kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
“Cheo ni dhamana, cheo hiki tulichokupa si ufalme, ni dhamana.Ni dhamana uliyopewa na Watanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi, lakini pia kupitia Bunge,”amesema Rais Dkt.Samia.
Amesema,uteuzi wa Ndejembi umezingatia sifa na vigezo alivyonavyo, ikiwemo uzoefu wake katika uongozi wa Serikali na sekta binafsi, pamoja na uwezo wake wa kujituma katika utekelezaji wa majukumu ya umma.
Rais Dkt.Samia amesema,umri wa Ndejembi, ambaye bado ni kijana, ni miongoni mwa mambo yaliyotazamwa katika kumpa dhamana hiyo, akieleza kuwa ana nguvu,ari na kasi ya kutekeleza majukumu ya Serikali.
“Nivishukuru vikao vya Chama Cha Mapinduzi vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu kwa kupendekeza na kuridhia jina la Deogratius Ndejembi katika nafasi ya Makamu wa Rais,” amesema.
Kwa mujibu wa Rais Samia, uamuzi wa kumpa kijana nafasi hiyo ulilenga kuendeleza utamaduni wa kuwalea vijana katika uongozi ili kupata uzoefu na kukua kiakili na kiuongozi, hususan katika majukumu yenye uzito wa kitaifa.
Amesisitiza kuwa,hakuna shule maalumu inayofundisha mtu kuwa Makamu wa Rais, hivyo Ndejembi atalazimika kuwa na bidii, nidhamu,weledi na utayari wa kujifunza kila siku ili kumudu majukumu yake.
Rais Dkt.Samia amesema,kujifunza huko kunapaswa kwenda sambamba na kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali, pamoja na kujifunza kutoka kwa viongozi na watendaji wengine anaofanya nao kazi.
Amesema,utekelezaji wa majukumu ya Serikali unahitaji umoja,mshikamano,ushirikiano, utulivu na uongozi bora ili kufikia malengo ya maendeleo na kutimiza matarajio ya wananchi.
Kwa msingi huo,amemtaka Ndejembi kushirikiana kwa karibu na viongozi wengine wa Serikali katika kuhakikisha majukumu yanatekelezwa ipasavyo na malengo ya maendeleo ya Taifa yanafikiwa kwa maslahi na usawa wa wananchi.
Rais Dkt.Samia pia amesisitiza umuhimu wa Ndejembi kuelewa kuwa,dhamana aliyopewa inahitaji uadilifu na uwajibikaji, akimtaka kuendelea kuitumikia Tanzania kwa uaminifu na kuweka maslahi ya Taifa mbele.
Aidha, amesema matarajio ya Watanzania ni kumuona Makamu huyo wa Rais akilitumikia Taifa kwa utii, uaminifu, utu, busara, hekima, uzalendo na maarifa.
Amemtaka pia kushirikiana katika utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030 pamoja na kufanikisha malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa kwa miaka 25 ijayo.
NDEJEMBI: “MAMA SITAMZINGUA”
Kwa upande wake, Makamu wa Rais Deogratius Ndejembi, baada ya kuapishwa amemshukuru Rais Dkt.Samia kwa kumwamini na kumpa dhamana ya kuwa msaidizi wake wa kwanza katika uongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ndejembi ameahidi kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, utii, uzalendo, bidii na kuzingatia maslahi mapana ya Taifa, akisema dhamira yake ni kumsaidia Rais katika kuharakisha maendeleo ya Tanzania.Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chamwino waliojitokeza kumpokea nje ya Ikulu ya Chamwino, Ndejembi amesema,ataendelea kufanya kazi kwa bidii na kuwatumikia Watanzania wote bila kujali tofauti zao.
Amesema pia ataendelea kuwa mwakilishi mzuri wa vijana nchini na kutumia nafasi hiyo kushirikiana katika juhudi za kuhakikisha Tanzania inapiga hatua zaidi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
“Nitafanya kazi ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kwa uadilifu na kuwatumikia Watanzania wote ili kuharakisha maendeleo,”amesema.
Katika salamu zake kwa wananchi, Ndejembi amesisitiza dhamira yake ya kutekeleza majukumu mapya kwa uaminifu, bidii na kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.
Kwa msisitizo, amesema: “Wana sitawazingua, na Mama sitamzingua,” akieleza dhamira yake ya kuwa mwaminifu katika kutekeleza wajibu aliopewa na Rais na Taifa kwa ujumla.
Ndejembi amewasalimia wananchi wa Chamwino, jimbo alilolitumikia kabla ya kuteuliwa kushika nafasi ya Makamu wa Rais.MABALOZI WASHUHUDIA UAPISHO
Katika hafla hiyo, Rais Dkt.Samia pia aliwashukuru mabalozi na wakuu wa mashirika ya kimataifa waliohudhuria, akisema uwepo wao ni ishara ya urafiki, udugu na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa.
Amesema, tukio hilo pia ni ushahidi wa uwezo wa Tanzania wa kufanya mabadiliko ya kiuongozi kwa njia ya amani, utulivu na kufuata taratibu za kikatiba.
Uapisho wa Ndejembi unafungua ukurasa mpya katika safari yake ya uongozi wa kitaifa, huku akibeba jukumu la kushirikiana na Rais Samia katika kusimamia utekelezaji wa majukumu ya Serikali na kufanikisha ajenda za maendeleo kwa kipindi kijacho.
Tags
Deogratius Ndejembi
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Maagizo ya Rais Samia
Makamu wa Rais wa Tanzania
Uapisho




























