NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Uganda na Amiri Jeshi Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF), Yoweri Kaguta Museveni amewaaga rasmi maafisa wakuu 19 wa jeshi hilo waliostaafu, huku akiwaasa kutumia kwa busara mafao na akiba zao ili kujenga maisha yenye usalama wa kifedha baada ya kustaafu.
Ameongoza hafla ya kuwaaga maafisa hao iliyofanyika katika Ikulu ya Entebbe, akiwapongeza kwa mchango wao katika ujenzi wa UPDF na kuimarisha usalama wa Uganda wakati wa utumishi wao wa kijeshi.
Katika hotuba yake, Rais Museveni amewapongeza majenerali hao kwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi ya nidhamu, uzalendo, uadilifu na kujitolea kwa taifa.
“Kwanza, nawapongeza Majenerali kwa mchango mkubwa walioutoa kwa UPDF. UPDF na NRM wameweza kujenga usalama,” amesema Museveni.
Rais Museveni alitumia sehemu kubwa ya hotuba yake kuwaelekeza wastaafu hao namna ya kusimamia fedha watakazopata baada ya kumaliza utumishi wa kijeshi.
Amewataka kuepuka kufanya maamuzi ya haraka ya kuwekeza mitaji mikubwa katika miradi yenye hatari, badala yake wakaanze na maeneo salama yanayoweza kuzalisha mapato ya uhakika bila kuhitaji usimamizi mkubwa wa kila siku.
Kwa mfano, aliwashauri kuwekeza katika hati fungani za Serikali, akisema uwekezaji huo unaweza kuwapatia mapato ya riba bila kuhitaji kushiriki moja kwa moja katika uendeshaji wa biashara.
“Ukiweka Shilingi milioni 600 na ukapata asilimia 15, mwishoni mwa mwaka hiyo ni faida ya Shilingi milioni 90,”amesema.
Kwa mujibu wa Rais huyo, wastaafu wanapaswa kuweka kipaumbele katika uwekezaji unaolinda mtaji wao huku ukiwawezesha kupata mapato ya kudumu.
“Kilicho salama zaidi ni kuweka tu fedha mahali zitakapozalisha riba,”amesema.
Mbali na uwekezaji wa kifedha, Rais Museveni amewashauri maafisa hao kutumia ardhi waliyonayo kuanzisha shughuli za uzalishaji, akitaja ufugaji wa mbuzi kama moja ya fursa rahisi na yenye soko.
Amesema,mbuzi wana soko la uhakika, huzaliana kwa haraka na hawahitaji gharama kubwa za chakula cha viwandani, hivyo wanaweza kufugwa kwa kiwango kidogo na kuendelezwa hatua kwa hatua.
“Mnaweza kufuga mbuzi. Mnawezaje kukosa wanunuzi? Hawahitaji chakula cha viwandani. Mnaweza kuanza kwa kiwango kidogo, kitu rahisi, salama na endelevu,”amesema.
Rais Museveni pia amependekeza wastaafu kuweka sehemu ya akiba zao katika akaunti za muda maalumu na kutumia mapato yatokanayo na akiba hizo kufadhili miradi mingine, ikiwemo ufugaji wa samaki na ujenzi wa nyumba za kupangisha.
“Kwanza panda mbegu mahali zitakapoota, kisha tumia mavuno katika miradi mingine,” amesema.
Pamoja na masuala ya uchumi, Rais Museveni amewataka maafisa hao kutokuchukulia kustaafu kama mwisho wa jukumu lao kwa taifa.
Amewahimiza kuendelea kuwa karibu na familia zao na jamii kwa ujumla, huku wakitumia uzoefu walioupata katika miaka yao ya utumishi wa kijeshi kusaidia maendeleo ya jamii na taifa.
Naibu Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Luteni Jenerali Sam Okiding amesema, maafisa hao wamekuwa na mchango mkubwa katika mageuzi ya UPDF pamoja na juhudi za kulinda amani na usalama nchini Uganda.
Amesema,nidhamu na kujitolea kwao kwa muda mrefu vimechangia katika kujenga taasisi yenye uwezo wa kutekeleza majukumu yake ya ulinzi na usalama.
Waziri wa Ulinzi na Masuala ya Wastaafu, Kiryowa Kiwanuka amewataka majenerali hao kuendelea kuitumikia Uganda hata baada ya kustaafu rasmi kutoka katika utumishi wa kijeshi.
Kiwanuka amesema,kustaafu kwao kunamaanisha kumalizika kwa utumishi wa kijeshi wa moja kwa moja, lakini si kumalizika kwa wajibu wao wa kuiwakilisha taasisi hiyo na taifa.
“Kustaafu kunaashiria mwisho wa utumishi wa kijeshi wa moja kwa moja kwa Majenerali baada ya miaka ya kulitumikia UPDF katika nyadhifa mbalimbali. Ninyi ni mabalozi wetu huko nje, hivyo endeleeni kutuwakilisha,” amesema.
Waziri huyo pia aliwataka kutumia maarifa waliyopata katika mafunzo ya usimamizi wa fedha kuwa chachu ya kuhamasisha utajiri na ujasiriamali miongoni mwa jamii.
Aliwapongeza kwa kufikia hatua hiyo ya maisha na kuwatakia mafanikio katika kipindi chao cha kustaafu.
“Hongereni. Ondokeni mkiwa mmeinua vichwa vyenu na mkaiwakilishe Uganda. Mungu awabariki na aibariki Uganda,”amesema.
Akizungumza kwa niaba ya maafisa waliostaafu, Jenerali Edward Katumba Wamala amesema,wanakabidhi taasisi yenye nidhamu na heshima, iliyojengwa kupitia miaka ya kujitolea na kujitoa kwa wanajeshi wake.
Katumba amewataka viongozi na wanajeshi waliobaki katika utumishi kuhakikisha wanaulinda urithi huo kwa kuendeleza uzalendo, weledi na uadilifu.
Amesisitiza pia umuhimu wa kulinda uhusiano kati ya UPDF na wananchi, akisema jeshi haliwezi kutenganishwa na jamii inayolihudumia.
“Tunawakabidhi taasisi yenye nidhamu na heshima iliyojengwa kupitia kujitolea. Tafadhali lindeni urithi huu kwa kuzingatia uzalendo, weledi na uadilifu na, muhimu zaidi, kuwaheshimu raia,”amesema.
Katumba pia alisisitiza umuhimu wa kuendelea kulinda uhusiano kati ya jeshi na wananchi pamoja na kuheshimu Katiba ya Uganda.
“Kuna uhusiano wa karibu kati ya UPDF na wananchi, tafadhali ulindeni na, bila shaka, endeleeni kuwa waaminifu kwa Katiba,”amesema.
Miongoni mwa maafisa wakuu waliostaafu ni Jenerali Edward Katumba Wamala, Luteni Jenerali Charles Otema Awany, Luteni Jenerali Charles Angina, Meja Jenerali Abel Kandiho, Meja Jenerali Geoffrey Tumusiime Katsigazi, Meja Jenerali Apollo Kasiita Gowa na Meja Jenerali Leopold Kyanda.
Wengine ni Brigedia Jenerali E. Muhanguzi, Brigedia Jenerali S. Omara, Brigedia Jenerali F. Zakye, Brigedia Jenerali F.R. Akiiki, Brigedia Jenerali M.S. Kisame, Brigedia Jenerali P.B. Mwesigwe, Brigedia Jenerali S.T. Kashure, Brigedia Jenerali S.N. Ocan, Brigedia Jenerali M.K. Bitimbika, Brigedia Jenerali C. Bakahumura, Brigedia Jenerali C.K. Asiimwe na Brigedia Jenerali C.M. Muhindo.
Maafisa hao wamehudumu katika nafasi mbalimbali za uongozi wa kijeshi, operesheni, utawala na mipango ya kimkakati, wakishiriki katika maendeleo ya UPDF na majukumu ya ulinzi na usalama wa Uganda.
Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Waziri wa Nchi wa Ulinzi na Masuala ya Wastaafu anayeshughulikia Ulinzi, Akifeza Grace Ngabirano, Waziri wa Nchi anayeshughulikia Wastaafu, Huda Abason Oleru pamoja na maafisa wengine wa UPDF.
Tags
Habari
Kimataifa
Majenerali wa UPDF
Majenerali Wastaafu Uganda
Retirement Ceremony Of UPDF Generals
UPDF
Wanajeshi Wastaafu
Yoweri Kaguta Museveni


