RC Chalamila atoa maagizo mazito kudhibiti maegesho holela ya malori Temeke

DAR-Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila ametoa maagizo mazito kwa mamlaka za usalama na uongozi wa Wilaya ya Temeke kuchukua hatua dhidi ya madereva wa malori wanaokiuka sheria kwa kuegesha magari yao katika maeneo yasiyoruhusiwa, hususan hifadhi za barabara.
Mhe. Chalamila amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Temeke kwa kushirikiana na Kamanda wa Polisi wa Wilaya hiyo kuunda kikosi kazi maalumu kitakachokuwa na jukumu la kuwakamata na kuwahoji madereva wa malori wanaoegesha katika maeneo yasiyo rasmi, hatua inayolenga kurejesha nidhamu na usalama katika matumizi ya barabara.

Mkuu huyo wa Mkoa ametoa maagizo hayo Agosti 17,2026 wakati wa ziara ya kimkakati katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Temeke, ambapo alikagua hali ya maegesho ya malori katika maeneo ya Barabara ya Mandela, Sandali na maeneo mengine.

Katika ziara hiyo, Mhe.Chalamila alishuhudia idadi kubwa ya malori yakiwa yameegeshwa kwenye hifadhi za barabara huku baadhi yakiziba sehemu za barabara na kuathiri matumizi salama ya miundombinu hiyo kwa watumiaji wengine.

Kutokana na hali hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema hatua za kisheria dhidi ya madereva wanaokiuka maagizo ya Serikali sasa zitaanza kuchukuliwa, akisisitiza kuwa uholela katika matumizi ya barabara na maeneo ya umma hauwezi kuvumiliwa katika Jiji la Dar es Salaam.
Aidha, Mhe.Chalamila amerejea maagizo yake kwa wamiliki wa bandari kavu kuhakikisha wanaweka maeneo maalumu ya maegesho ya malori ndani ya maeneo yao, badala ya kuyaacha magari hayo yakiingia kwenye hifadhi za barabara au kuziba barabara za umma.

Ametoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya ya Temeke kuwaita wamiliki wa bandari kavu katika kikao maalumu na Mkuu wa Mkoa, kinachotarajiwa kufanyika Agosti 19,2026 kwa ajili ya kuwapatia maelekezo ya utekelezaji wa hatua hizo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chalamila alitembelea daraja linalounganisha Kata ya Toangoma na Kata ya Kibondemaji hususan maeneo ya Mtaa wa Golani B na Mtaa wa Kichangani na kujionea hali ya daraja hilo ambalo limejengwa na wananchi kwa nguvu zao wenyewe miaka michache iliyopita.

Baada ya kukagua daraja hilo, Mkuu wa Mkoa alieleza kutoridhishwa na ubora na hali ya miundombinu hiyo, akisema haikidhi mahitaji ya wananchi wanaolitumia kila siku.

Kwa msingi huo, ameiagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kufanya tathmini ya kina ya daraja hilo na kuandaa upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa daraja la kudumu.
Amesema, hatua hiyo inalenga kupata suluhisho la kudumu kwa changamoto ambayo imekuwa ikiathiri wananchi wa maeneo hayo kwa muda mrefu, hususan katika usafiri na shughuli za kiuchumi.

Mhe.Chalamila pia amesisitiza utekelezaji wa maagizo ya mabasi yote ya mikoani na yanayokwenda nchi jirani kutumia Kituo cha Mabasi cha Magufuli, badala ya kuendelea kuegesha katika eneo la Shekilango na maeneo mengine yasiyo rasmi.

Amesema,utekelezaji wa hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Mkoa wa Dar es Salaam wa kupunguza msongamano wa magari, kuongeza ufanisi wa matumizi ya miundombinu ya usafiri na kuhakikisha shughuli za usafirishaji zinafanyika katika maeneo yaliyotengwa rasmi.

Katika ziara hiyo, wananchi wa Kata ya Sandali pamoja na madereva wa malori waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili, zikiwemo ukosefu wa maeneo rasmi ya maegesho ya malori, uharibifu wa mazingira unaodaiwa kusababishwa na salfa inayotoka katika bandari kavu iliyopo eneo hilo, pamoja na ukosefu wa barabara za ndani zinazokidhi mahitaji ya wakazi.

Changamoto hizo ziliwasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa kwa lengo la kupata hatua za haraka na za kudumu kutoka kwa mamlaka zinazohusika.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Jomaary Mrisho Satura amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa,changamoto zilizowasilishwa na wananchi pamoja na maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi na mamlaka husika.

Ziara hiyo ya Mhe. Chalamila inaelezwa kuwa sehemu ya juhudi za Serikali za Mkoa wa Dar es Salaam katika kuimarisha usimamizi wa miundombinu,kudhibiti matumizi holela ya maeneo ya umma, kupunguza msongamano wa magari na kuhakikisha wananchi wanapata huduma na miundombinu salama na yenye viwango vinavyokidhi mahitaji yao.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here