WAZIRI wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ujenzi, Mhe. Abdallah Ulega (Mb) pamoja na Timu ya Wataalamu wa Wizara ya Ujenzi katika hatua ya kuimarisha utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya barabara na madaraja nchini.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika ofisi za Wizara ya Fedha jijini Dodoma, ambapo yamelenga kujadili namna ya kuhakikisha upatikanaji wa fedha na kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu inayotekelezwa na Serikali.Kikao hicho ni sehemu ya hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuboresha mfumo wa upatikanaji na matumizi ya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo mageuzi ya kimfumo ambapo asilimia 70 ya mapato yanayokusanywa kupitia mifuko maalum yataelekezwa moja kwa moja kwenye mifuko hiyo bila kupita Hazina.
Katika mwezi Julai pekee, Serikali ilitoa jumla ya shilingi bilioni 325 kwa mifuko mbalimbali ya maendeleo, ambapo shilingi bilioni 76 zilipelekwa moja kwa moja kwenye Mfuko wa Barabara.Utaratibu huo utaendelea kutekelezwa katika mwaka mzima wa fedha, ukiwa na lengo la kuhakikisha kuwa miradi ya miundombinu inaendelea kutekelezwa kwa kasi na kwa wakati bila kukwamishwa na changamoto ya upatikanaji wa fedha.
Aidha, Waziri wa Fedha na Waziri wa Ujenzi walijadili uwezekano wa kutumia fursa zinazotolewa na sekta ya fedha katika kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kwa ajili ya miradi mikubwa ya miundombinu kama vile matumizi ya hati fungani za miundombinu (infrastructure bonds).
Ni ambazo zinaweza kusaidia Serikali kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja na hivyo kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa bila kusubiri mapato ya ndani kukusanywa hatua kwa hatua.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwezo wa Serikali kutekeleza miradi ya kimkakati ya barabara na madaraja kwa wakati, huku ikiendelea kuhakikisha matumizi ya fedha za umma yanafanyika kwa ufanisi, uwajibikaji na kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Taifa.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhe. Godfrey Kasekenya,Naibu Makatibu Wakuu wa Wizara ya Fedha, Bw. Nsubili Joshua na Bw. Elijah Mwandumba; Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde; Kamishna wa Kituo cha Ubia Kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP Centre), Bw.David Kafulila pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka Wizara ya Fedha, Wizara ya Ujenzi na taasisi zake.
Tags
Abdallah Ulega
Balozi Khamis Mussa Omary
Habari
PPP Tanzania
Ujenzi wa Barabara na Madaraja
Wizara ya Fedha Tanzania
Wizara ya Ujenzi Tanzania
