NA DIRAMAKINI
RAIS wa Simba Sports Club, Mohammed Dewji amewataka wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kudumisha umoja na mshikamano, akisisitiza kuwa mafanikio ya Simba hayawezi kutegemea mtu mmoja bali nguvu ya familia nzima ya WanaSimba.
Dewji ametoa kauli hiyo leo Agosti 8,2026 katika kilele cha maadhimisho ya Simba Day yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, ambapo klabu hiyo ilisherehekea kutimiza miaka 90 tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dewji amesema, Simba imepitia safari ndefu yenye mafanikio na changamoto, huku akieleza kuwa msingi wa mafanikio ya klabu hiyo umejengwa na vizazi mbalimbali vya viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki.
Alianza hotuba yake kwa kumshukuru Mungu, Serikali, wadhamini, wafadhili, washirika na Wanasimba wote kwa mchango wao katika kuiwezesha klabu hiyo kufikia hatua iliyonayo sasa.
Dewji pia amewaomba waliohudhuria kusimama kwa dakika moja kuwaenzi WanaSimba waliotangulia mbele ya haki, wakiwemo waanzilishi wa klabu, viongozi, wachezaji, wanachama na mashabiki waliochangia kuijenga Simba kwa miongo kadhaa.
MABADILIKO YA KLABU
Katika hotuba hiyo, Dewji amegusia mchakato wa mabadiliko ya mfumo wa uendeshaji wa Simba, akisema ulianza baada ya wanachama kuridhia mabadiliko hayo mwaka 2017 na kuanza kutekelezwa rasmi mwaka 2018.
Amesema,katika kipindi hicho, bajeti ya klabu imeongezeka kutoka takribani Shilingi bilioni 3 hadi zaidi ya Sh20 bilioni kwa mwaka, akieleza kuwa ongezeko hilo ni moja ya viashiria vya hatua ambazo Simba imepiga katika kujenga uwezo wake wa kifedha na kiushindani.
Hata hivyo, amesema mchakato wa mabadiliko hayo bado haujakamilika kutokana na changamoto mbalimbali za kiutendaji na kiidhini.
“Kama ninyi wenyewe mliridhia mabadiliko, kwa nini baada ya karibu miaka kumi bado tunakwama?” amehoji Dewji, huku akitaka wanachama kupata majibu kuhusu vikwazo vinavyochelewesha kukamilika kwa mchakato huo.
Amesema,amekuwa akikosolewa kuhusu baadhi ya masuala ya klabu, lakini amechagua kutanguliza maslahi ya Simba badala ya maslahi yake binafsi.
Dewji pia amekanusha madai kwamba anazuia utoaji wa kadi za uanachama, akisema suala hilo halipo chini ya upande wa mwekezaji.
DIRA YA SIMBA YA BAADAYE
Rais huyo wa Simba amesema,maono yake ni kuona klabu hiyo ikiendelea kujenga uwezo wa kifedha, miundombinu na ushindani ili iweze kufikia kiwango cha vilabu vikubwa barani Afrika.
Amesema,anatamani kuona Simba ikiwa na uwanja wake wa kisasa pamoja na kituo cha biashara katika eneo linalofikika kwa urahisi jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Dewji, uwekezaji huo unapaswa kwenda sambamba na kuimarisha timu, kukuza vipaji na kujenga uchumi wa klabu utakaoifanya iwe na uwezo wa kushindana kwa muda mrefu.
Amesisitiza kuwa,ataendelea kutekeleza wajibu wake, ikiwemo kuwekeza katika usajili na kuimarisha kikosi cha Simba.
BIMA YA AFYA KWA WANACHAMA
Katika hatua nyingine, Dewji ameeleza kuwa, amepokea maombi kutoka kwa baadhi ya WanaSimba wenye changamoto za kiafya, hali iliyomsukuma kufikiria namna klabu inavyoweza kuwasaidia wanachama wake nje ya shughuli za soka.
Amesema,yuko tayari kugharamia bima ya afya kwa wanachama wa Simba, lakini utekelezaji wa mpango huo unahitaji kwanza kupatikana kwa orodha sahihi na kamili ya wanachama wa klabu.
“Kama klabu yetu inapaswa kushinda uwanjani, lakini pia isimame na watu wake nje ya uwanja,”amesema.
Ametoa wito kwa viongozi kuhakikisha taarifa za wanachama zinakamilishwa ili kuwezesha mpango huo kuanza kutekelezwa.
SIMBA SI YA MO
Dewji amesisitiza kuwa,Simba si mali ya mtu mmoja, bali ni klabu ya wanachama na mashabiki wake, hivyo akawataka WanaSimba kuepuka migawanyiko na badala yake kujenga utamaduni wa kuuliza, kujadili na kutafuta ukweli kuhusu masuala yanayohusu klabu.
“Simba si ya Mo. Simba ni yetu sote,”amesema, akiwataka wanachama kutumia mikutano yao kwa kuuliza maswali na kuwawajibisha viongozi waliowapa dhamana pale wanapoona kuna jambo linalohitaji ufafanuzi.
Amesema,tofauti za kimtazamo zisigeuke kuwa chanzo cha kuigawa klabu, akisisitiza kuwa maendeleo ya Simba yanahitaji umoja na mshikamano wa WanaSimba wote.LENGO NI UBINGWA WA AFRIKA
Dewji amesema, pamoja na changamoto ambazo klabu imepitia, ndoto yake bado ni kuiona Simba ikitwaa ubingwa wa Afrika.
Amesema,safari hiyo inahitaji maandalizi ya muda mrefu, uwekezaji endelevu, miundombinu imara, usimamizi bora na umoja miongoni mwa wanachama na mashabiki.
“Ndoto yetu bado ni ile ile kuiona Simba ikiwa Bingwa wa Afrika. Na ninaamini kabisa, tutafika,”amesema.
Akihitimisha hotuba yake, Dewji amewataka WanaSimba kutokata tamaa na kuendelea kuiunga mkono timu, akisema Simba ni kubwa kuliko changamoto zinazokabili klabu hiyo kwa sasa.Amesema,miaka 90 iliyopita waliotangulia waliweka msingi wa Simba ya leo, hivyo kizazi cha sasa kina wajibu wa kuandika historia mpya na kuijenga klabu hiyo kuwa kubwa, imara na yenye ushindani zaidi barani Afrika.









































