NA DIRAMAKINI
SERIKALI ya Singapore imetangaza kutoa malipo ya fedha taslimu kati ya dola za Singapore 400 na 600 kwa zaidi ya raia milioni 2.4 wenye umri wa miaka 21 na zaidi, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuwasaidia wananchi kukabiliana na gharama za maisha.
Malipo hayo yanayojulikana kama Cost-of-Living Special Payment ambapo yataanza kutolewa kuanzia Septemba 9, 2026 kwa raia wanaokidhi vigezo vilivyowekwa na Serikali.
Kwa mujibu wa Wizara ya Fedha ya Singapore, malipo hayo yatatolewa kwa raia wanaoishi nchini humo, wenye mapato yanayokadiriwa kutotoa zaidi ya dola za Singapore 100,000 kwa mwaka wa tathmini wa 2025, pamoja na wale wanaomiliki si zaidi ya nyumba moja.
Kiasi cha fedha atakachopokea mwananchi kitategemea kiwango cha mapato yake pamoja na thamani ya nyumba anayomiliki.
Aidha,wananchi wenye mapato yasiyozidi dola za Singapore 22,000 na wanaoishi katika nyumba yenye thamani ya mwaka isiyozidi dola 15,000 watapata kiwango cha juu cha dola 600.
Serikali imesema,malipo hayo yanalenga zaidi kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini kukabiliana na ongezeko la gharama za maisha.
Awali, mpango huo ulitangazwa katika Bajeti ya Taifa ya Singapore ya mwaka 2026, ambapo wananchi waliostahili walitarajiwa kupata kati ya dola 200 na 400.
Hata hivyo, Serikali iliongeza dola nyingine 200 mwezi Aprili kama sehemu ya hatua za kupunguza athari za ongezeko la bei lililohusishwa na mzozo wa Mashariki ya Kati.
Mbali na malipo hayo, Serikali pia imetangaza mpango mwingine wa msaada unaojumuisha vocha za Community Development Council (CDC) zenye thamani ya dola 300 kwa kila kaya.
Vocha hizo zinatarajiwa kutolewa Januari,2027 na zitatumika katika maduka makubwa, wafanyabiashara na wachuuzi wanaoshiriki katika mpango huo.
Wakati huo huo, takribani raia milioni 1.5 wa Singapore wanaostahili wameanza pia kupokea malipo ya kati ya dola 450 na 850 kupitia mpango wa kudumu wa Goods and Services Tax (GST) Voucher, unaolenga kuwasaidia wananchi wenye kipato cha chini na cha kati kukabiliana na kodi ya bidhaa na huduma pamoja na gharama za kila siku.
Hatua hizo zinaonesha jitihada zinazoendelea za Serikali ya Singapore kupunguza mzigo wa gharama za maisha kwa wananchi, huku ikielekeza sehemu kubwa ya msaada kwa kaya na watu wenye kipato cha chini.
Tags
Gharama za Maisha
Habari
Kimataifa
Malipo kwa Raia Singapore
Singapore
Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi
