NA DIRAMAKINI
MUHUBIRI na Mwinjilisti wa Kimataifa,Dkt.Alphonce Temba ameitaka Serikali kuharakisha matumizi rasmi ya Bandari Kavu ya Kwala, Vigwaza mkoani Pwani akisema hatua hiyo ni miongoni mwa suluhisho la kudumu la kukabiliana na msongamano wa malori na shughuli za mizigo katika Jiji la Dar es Salaam.

Dkt.Temba amesema amekuwa akitetea na kuhamasisha utekelezaji wa mradi huo kwa zaidi ya miaka 12, akisisitiza kuwa Kwala inaweza kuwa kitovu muhimu cha kuhifadhi na kusafirisha mizigo, hivyo kupunguza idadi ya malori yanayoingia katikati ya jiji na kuacha barabara zikitumika kwa shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa Dkt.Temba, alianza kuzungumzia umuhimu wa Kwala tangu Agosti 2014, wakati aliposhiriki mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV, ambako alieleza kuwa uamuzi wa Serikali kuichagua Vigwaza kuwa eneo la kimkakati kwa ajili ya bandari kavu ulikuwa wa busara na wenye manufaa kwa Taifa.
Amesema,eneo hilo lina faida kadhaa za kimkakati, ikiwemo kumilikiwa na Serikali pamoja na kuwepo kwa miundombinu ya reli, hali inayoweza kupunguza gharama za ujenzi na kurahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda Kwala.
“Ni kweli kabisa kwamba kijografia ukiliangalia eneo la Vigwaza linaweza kuwa na faida zaidi ya tatu kuwa bandari kavu,” amesema Dkt. Temba.
Ahoji kuendelea kuunda kamati
Akizungumza katika kipindi cha Kipima Joto cha ITV hivi karibuni, Dkt.Temba amesema,suluhisho la changamoto ya foleni za Dar es Salaam si kuendelea kuunda kamati za ushauri, bali ni kutekeleza mipango ya muda mrefu ambayo tayari imeainishwa na Serikali.
Amesema,Tanzania inapaswa kuacha kujadili mara kwa mara tatizo ambalo limekuwa likifahamika kwa muda mrefu na badala yake kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa mipango ya kimkakati ya matumizi ya ardhi na maendeleo ya miji.
Kwa mujibu wake, tangu mwaka 2008 na 2009 kulikuwa na mipango ya kuanzisha mzani katika eneo la Vigwaza na kuliendeleza Kwala kuwa kitovu cha shughuli za bandari kavu, kwa lengo la kupunguza msongamano wa malori katikati ya Dar es Salaam.
Amedai kuwa, baadhi ya mipango hiyo pia imejumuishwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo ya 2050, lakini utekelezaji wake haujafikia kiwango kinachotarajiwa.
“Tunapaswa kunyoosha mambo. Hii nchi ni yetu sote. Haiwezekani tuendelee kuzungumza kila siku kuhusu foleni wakati suluhisho lipo wazi. Kwala ilipangwa kwa kazi hiyo muda mrefu,” amesema.
Aonya kuhusu mgongano wa maslahi
Dkt.Temba pia ameibua hoja kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mgongano wa maslahi katika baadhi ya ushauri unaotolewa kuhusu namna ya kukabiliana na msongamano wa malori jijini.
Amesema,baadhi ya watu wanaoshiriki katika kutoa ushauri wanaweza kuwa na maslahi katika biashara ya maghala na yadi za kuhifadhi makontena ndani ya Jiji la Dar es Salaam, jambo ambalo kwa mtazamo wake linaweza kuathiri mapendekezo yanayotolewa.
“Ukimpa mtu mwenye yadi ya makontena jukumu la kushauri namna ya kuondoa malori mjini, unategemea atashauri nini? Atakuwa analinda biashara yake,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa upangaji bora wa miji, Dkt.Temba amesema,Tanzania inapaswa kuharakisha uendelezaji wa maeneo mapya kama Kwala, Vigwaza, Chalinze na Morogoro ili kupunguza mkusanyiko wa shughuli za kiuchumi na usafirishaji ndani ya Dar es Salaam.
Ametoa mfano wa Afrika Kusini, ambako amesema miundombinu ya kisasa ya reli na barabara imewezesha kuunganisha miji mikubwa na kupunguza changamoto za usafiri.
Kwa mtazamo wake, uwekezaji katika miji ya satelaiti pamoja na usafiri wa reli unaweza kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kupunguza msongamano katika miji mikubwa na kusambaza fursa za kiuchumi katika maeneo mbalimbali.
Dkt.Temba pia amekosoa hali ya baadhi ya maeneo ya Dar es Salaam yaliyokuwa yakitumika kwa shughuli za kijamii kugeuzwa kuwa maeneo ya kuhifadhi makontena na magari.
Ametaja eneo la Jangwani, ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitumika kwa mikutano mbalimbali ya kitaifa, kisiasa na kidini, pamoja na eneo la Biafra, akisema matumizi hayo yanaibua maswali kuhusu utekelezaji wa mipango ya matumizi ya ardhi jijini.
Amesisitiza kuwa,shughuli za bandari kavu na uhifadhi wa mizigo zinapaswa kuelekezwa katika maeneo yaliyopangwa kwa ajili hiyo nje ya katikati ya jiji.
Dkt.Temba amesema Serikali tayari imewekeza zaidi ya Shilingi bilioni 90 katika maendeleo ya Kwala, hivyo akataka uwekezaji huo uendelezwe kwa kuhakikisha eneo hilo linatumika kikamilifu kama kituo muhimu cha kuhudumia mizigo.
Aidha, amesema nchi jirani, zikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Zambia na Sudan, zinaonesha nia ya kutumia Kwala kama kitovu cha shughuli za usafirishaji wa mizigo, jambo ambalo linaweza kuongeza nafasi ya Tanzania kuwa kitovu cha biashara katika Afrika Mashariki na Kati.
Kwa mujibu wa taarifa za hivi karibuni, DRC imetenga takribani dola milioni 291.3 za Marekani kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa bandari kavu ya Kwala kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.
Mradi huo unatarajiwa kujengwa katika eneo la Kwala, takribani kilomita 60 kutoka Bandari ya Dar es Salaam, huku DRC ikipewa eneo la hekta 45 kwa ajili ya shughuli zake za usafirishaji wa mizigo.
Inatarajiwa kuwa, mradi huo utapunguza muda wa usafirishaji wa mizigo ya DRC kupitia Bandari ya Dar es Salaam kutoka wastani wa siku 15-16 hadi siku tano hadi sita, sambamba na kupunguza gharama za usafirishaji.
Kwala kulenga kuhudumia makasha zaidi ya 300,000 kwa mwaka
Taarifa ya Serikali iliyowasilishwa Machi 16,2025 kwa waaandishi wa habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ilieleza kuwa, Bandari Kavu ya Kwala ni mradi wa kimkakati unaolenga kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza msongamano wa mizigo bandarini.
Msigwa alisema,Kwala inatarajiwa kuhudumia takribani makasha 823 kwa siku, sawa na hadi makasha 300,395 kwa mwaka, ambayo ni takribani asilimia 30 ya makasha yote yanayopita katika Bandari ya Dar es Salaam.
Serikali pia imewekeza katika miundombinu inayounganisha Kwala na mtandao wa reli wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), pamoja na barabara za zege, umeme, maji na miundombinu mingine muhimu.
Kupitia reli, mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam inaweza kusafirishwa moja kwa moja hadi Kwala, hatua ambayo inalenga kupunguza utegemezi wa malori katika usafirishaji wa mizigo, kupunguza msongamano na kupunguza uchakavu wa barabara.
Mbali na shughuli za bandari kavu, Serikali imeeleza kuwa eneo hilo lina mpango wa kuwa kitovu cha shughuli za viwanda. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kwala inatarajiwa kuwa na viwanda vikubwa na vya kati 200 pamoja na viwanda vidogo 300 vitakavyohusika na sekta mbalimbali, ikiwemo usindikaji wa chakula, utengenezaji wa vifaa, dawa, vifaa vya ujenzi, nguo na viatu pamoja na kemikali.
Kongani ya viwanda ya SINO-TAN nayo imetajwa kuwa sehemu ya mradi huo, huku ikitarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira 100,000 za moja kwa moja na ajira 500,000 zisizo za moja kwa moja.
Aidha, utekelezaji kamili wa Kwala unaweza kuwa na manufaa zaidi ya kupunguza foleni za malori, kwa kuwa unaweza pia kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam, kupunguza gharama za usafirishaji, kuchochea uwekezaji na kuifanya Tanzania kuwa kiungo muhimu cha biashara na usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika Mashariki, Kati na Kusini.
Rais Dkt.Samia azindua Bandari Kavu ya Kwala
jJulai 31,2025 Serikali ilizindua rasmi Kituo cha Kimataifa cha Lojistiki cha Kwala (Kwala International Logistics Centre), mradi wa kimkakati utakaopunguza gharama za usafirishaji, kuondoa msongamano wa malori jijini Dar es Salaam, na kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi mkoani Pwani, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema,Kituo hicho ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto ya ongezeko la mizigo na meli bandarini.
“Ni wazi kuwa Kituo hiki ni jibu la kiu ya muda mrefu ya Tanzania kuwa na bandari kavu ya kisasa nje ya jiji la Dar es Salaam, hiyo kina umuhimu mkubwa,”alisema Rais Dkt. Samia.
Akieleza takwimu za matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam, Rais Dkt. Samia alidokeza ongezeko la matumizi ya bandari hiyo kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30 kila mwaka na kukua kwa shehena za mizigo kutoka tani milioni 23.69 mwaka 2023 hadi tani milioni 27.76 mwaka 2024, huku idadi ya meli ikiongezeka kutoka 1,860 hadi 1,990.
Ukuaji huu wa shughuli za bandari alisema, umeongeza msongamano mkubwa wa malori jijini Dar es Salaam na mrundikano wa makasha bandarini, kwa kuwa usafirishaji mwingi wa mizigo hufanyika kwa njia ya barabara, hali inayopunguza ufanisi na ushindani wa Bandari ya Dar es Salaam kwa ujumla.
Rais Dkt. Samia alieleza uwekezaji katika kituo cha Kwala kama sehemu ya kupanua bandari kwa kuhamishia shughuli kadhaa kutoka Dar es Salaam kwenda Kwala, hatua itakayoongeza wigo wa huduma na kuboresha kasi ya upakuaji na usafirishaji wa mizigo.
“Kituo hiki kitarahisisha upatikanaji wa huduma zote hapa Kwala na maboresho haya yataepusha gharama zilizokuwa zinasababishwa na ucheleweshaji wa mizigo,”alisema.
Kituo hicho kilichounganishwa na barabara kuu pamoja na reli ya kisasa ya SGR kipo kwenye mpango wa kuunganishwa na Bandari za Bagamoyo na Tanga, hatua inayolenga kuimarisha huduma za bandari na kuongeza mvuto wa Tanzania kama kitovu cha biashara ya kikanda na kimataifa.