NA DIRAMAKINI
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewaagiza wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya na viongozi wa taasisi mbalimbali za Serikali kuchukua hatua za mapema kukabiliana na mvua kubwa zinazotabiriwa kunyesha nchini, akisisitiza kuwa maandalizi ya haraka ni muhimu katika kuzuia maafa na kupunguza madhara kwa wananchi.

Ametoa agizo hilo leo Agosti 22,2026 wakati akizungumza na wananchi wa Mkoa wa Pwani muda mfupi baada ya uzinduzi wa Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) Megawati 2,115 kilichopo Rufiji mkoani humo.
Mheshimiwa Rais amesema,taarifa za utabiri zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) zinaashiria uwezekano wa kuwepo kwa mvua kubwa zinazohusishwa na hali ya El Niño, hivyo viongozi katika ngazi mbalimbali za Serikali hawapaswi kusubiri athari zijitokeze kabla ya kuchukua hatua.
“Niwaombe nendeni mkajitayarishe,mkaweke mazingira sawa ili mvua hizo zitakapoanza zisilete maafa makubwa kwa wananchi wetu."
Amesisitiza kuwa, tahadhari zinazotolewa na TMA zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito na viongozi kuhakikisha maeneo yao yanaandaliwa mapema, hususan katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mafuriko ili kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza.
“Kwa hiyo niwaombe sana, tahadhari zimeanza kutolewa, hatua zichukuliwe ili mvua hizi zisilete madhara kwa wananchi wetu."
TMA yatabiri
Kauli ya Rais Dkt.Samia imekuja wakati TMA ikiwa imetoa utabiri wa msimu wa mvua za Vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba,2026 huku ukionya kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa hali ya El Niño yenye nguvu kubwa.
Kwa mujibu wa utabiri huo, mvua za Juu ya Wastani hadi Wastani zinatarajiwa katika maeneo mbalimbali nchini, yakiwamo Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Ziwa Victoria na kaskazini mwa Mkoa wa Kigoma.
Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a amesema,mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya Septemba hadi Oktoba 2026, huku ongezeko kubwa la mvua likitarajiwa mwezi Novemba.
Aidha, amesema mvua za nje ya msimu zinaweza kuendelea hadi Januari 2027, hali inayohitaji maandalizi ya mapema kutoka kwa Serikali, sekta binafsi na wananchi.
Dkt.Chang’a ameeleza kuwa, ongezeko la mvua linaweza kusababisha unyevu uliokithiri kwenye udongo na kuongeza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko katika maeneo mbalimbali.
Kwa mujibu wa tahadhari hiyo, mafuriko yanaweza kuathiri miundombinu ya kilimo, kuongeza kina cha maji katika mabwawa na mito, pamoja na kusababisha uchafuzi wa vyanzo vya maji na hivyo kuongeza hatari ya milipuko ya magonjwa.
Mabadiliko hayo ya hali ya hewa pia yanaweza kuathiri uzalishaji wa mazao kutokana na kuongezeka kwa magonjwa ya mimea.
Miongoni mwa mazao yanayotajwa kuwa katika hatari ya kuathiriwa ni viazi mviringo, alizeti, maharage, ufuta na mbogamboga.
Athari hizo hazitarajiwi kuishia katika sekta ya kilimo pekee. TMA imeonya kuwa,mvua kubwa zinaweza pia kuathiri shughuli za usafiri, ujenzi na utalii kutokana na mmomonyoko wa barabara, uharibifu wa madaraja na changamoto nyingine zinazoweza kujitokeza kutokana na mafuriko.
Katika maeneo yenye shughuli za uhifadhi na utalii, mabadiliko ya mazingira yanayoweza kusababishwa na mvua nyingi yanaweza pia kuathiri mienendo na uhamaji wa wanyamapori.
Kufuatia utabiri huo, TMA imezitaka sekta mbalimbali za kiuchumi na kijamii kutumia taarifa za hali ya hewa katika kupanga shughuli zao mapema, kwa lengo la kupunguza athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.
Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni kuvuna na kuhifadhi maji ya mvua, kuimarisha miundombinu inayoweza kuathiriwa na mafuriko, pamoja na kuhakikisha mifumo ya tahadhari za mapema inafanya kazi kwa ufanisi.
TMA pia imesisitiza umuhimu wa kudhibiti mazalia ya mbu na kuchukua hatua za kuzuia milipuko ya magonjwa ambayo inaweza kuongezeka kutokana na maji yaliyotuama na uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Kwa upande wa Serikali za Mitaa na mamlaka nyingine zinazohusika na usimamizi wa majanga, maandalizi hayo yanahusisha kutambua maeneo hatarishi, kuimarisha mifumo ya utoaji wa taarifa kwa wananchi na kuwa tayari kuchukua hatua za uokoaji endapo mafuriko au majanga mengine yatatokea.
Aidha,kwa kutoa agizo hilo, Rais Dkt.Samia ameweka msisitizo katika umuhimu wa viongozi kutumia taarifa za kisayansi za utabiri wa hali ya hewa kama msingi wa maandalizi na hatua za kuzuia majanga.
Ujumbe huo unalenga kuhakikisha kuwa tahadhari zinazotolewa kabla ya msimu wa mvua zinatafsiriwa kuwa hatua halisi katika ngazi za mikoa, wilaya na taasisi, badala ya kusubiri maafa yatokee.
Tags
Dr Samia Suluhu Hassan
El Niño
Habari
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA)
Tanzania Meteorological Agency (TMA)
Utabiri wa Hali ya Hewa Tanzania