Tanzania na Italia zaimarisha ushirikiano wa kiteknolojia katika Sekta ya Reli

ROME-Serikali ya Tanzania imeimarisha ushirikiano wa kimkakati na Italia katika sekta ya reli baada ya kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), kampuni ya FS Engineering S.p.A. na ITS Engineering S.r.l., hatua inayolenga kuhamisha teknolojia za kisasa, kuongeza uwezo wa kitaalamu na kuboresha usimamizi wa miradi ya reli nchini.
Makubaliano hayo yalishuhudiwa na Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa wakati wa ziara rasmi nchini Italia kufuatia mwaliko wa Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia.

Ziara hiyo pia ilihusisha kujifunza matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa miundombinu ya reli na kutembelea miradi mikubwa ya kimkakati inayotekelezwa nchini humo.

Kwa upande wa Tanzania, Hati ya Makubaliano ilisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya M. Shiwa huku FS Engineering ikiwakilishwa na Dario Lo Bosco na ITS Engineering ikiwakilishwa na Michele Titton.
Makubaliano hayo yanaweka msingi wa ushirikiano wa muda mrefu katika kubadilishana utaalamu wa kihandisi, kuendeleza mafunzo kwa wataalamu wa TRC, kuimarisha uwezo wa kitaasisi na kuendeleza matumizi ya teknolojia za kisasa katika kubuni, kupanga, kusimamia na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya reli.

Aidha, ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza uwezo wa TRC katika kubuni miradi mipya ya reli, kuboresha mifumo ya uendeshaji wa miundombinu, kuimarisha huduma za ushauri wa kihandisi na kuongeza ufanisi wa biashara ya reli kupitia matumizi ya suluhisho bunifu.

Katika ziara hiyo, ujumbe wa Tanzania ulitembelea Kituo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Uendeshaji wa Reli (National Control Room) cha Rete Ferroviaria Italiana (RFI), ambapo ulijifunza namna mtandao wa reli wa Italia unavyosimamiwa kwa wakati halisi kupitia mifumo ya kidijitali inayoratibu usafiri wa abiria na mizigo, shughuli za matengenezo na udhibiti wa usalama.
Vilevile, ujumbe ulitembelea mradi mkubwa wa miundombinu jijini Florence unaosimamiwa na FS Engineering na kujionea matumizi ya teknolojia za kisasa kama Building Information Modelling (BIM), LiDAR Survey, Akili Unde (Artificial Intelligence-AI) pamoja na Digital Control Room, ambazo huwezesha kufuatilia maendeleo ya miradi, kutathmini ubora wa kazi, kubaini changamoto mapema na kufanya maamuzi kwa kutumia taarifa za wakati halisi.

Wataalamu wa FS Engineering pia walifanya majadiliano ya kiufundi na ujumbe wa Tanzania kuhusu mbinu bora za usimamizi wa miradi na namna teknolojia hizo zinavyoweza kutumika kuboresha utekelezaji wa miradi ya reli nchini.
Ziara hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiufundi kati ya Tanzania na Italia, huku ikitarajiwa kuiwezesha TRC kunufaika na uhamishaji wa teknolojia, kuongeza uwezo wa wataalamu wake na kuimarisha kitengo chake cha ushauri wa kihandisi kupitia ushirikiano na taasisi zenye uzoefu wa kimataifa.

Hatua hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuendelea kuimarisha sekta ya reli kwa kutumia teknolojia za kisasa, kuongeza ufanisi wa usimamizi wa miradi ya kimkakati, kujenga uwezo wa wataalamu na kuhakikisha miundombinu ya reli inachangia kikamilifu maendeleo ya uchumi wa Taifa pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here