Rais Dkt.Samia azindua Tume ya Jaji Lila

DAR-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua Tume ya Rais ya Uchunguzi ya Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria Katika Matukio ya Ghasia Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ikiwa na jukumu la kuchunguza kwa kina chanzo cha matukio hayo, wahusika pamoja na waliowezesha kutokea kwake.
Akizungumza leo Ijumaa Agosti 7, 2026 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Tume hiyo, Rais Samia amesema ameunda Tume hiyo kwa kuzingatia mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Tume ya Uchunguzi, Sura ya 32, ili kuwezesha uchunguzi wa kina kuhusu matukio ya ghasia na ukiukwaji wa sheria yaliyotokea.

Amesema Tume hiyo itaongozwa na Jaji Shabani Ally Lila na itakuwa na jumla ya makamishna sita, ambapo mmoja anatoka Uganda na mwingine Namibia, hatua inayolenga kuongeza mtazamo mpana katika utekelezaji wa jukumu hilo.

“Katika Tume hii tumeamua kuwashirikisha wenzetu kutoka nje ya Tanzania ili kupata maono mapana,” amesema Rais Samia.
Rais Samia amesema Tume hiyo itaingia kwa undani zaidi kubaini waliowachochea, waliohusika pamoja na waliotoa fedha ili matukio ya uvunjifu wa amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 yatokee ndani ya nchi.

Ameeleza kuwa,Tume imepewa hadidu za rejea zitakazoongoza utekelezaji wa majukumu yake na itawasilisha ripoti pamoja na mapendekezo yake kwa mujibu wa sheria.

“Nina imani majaji hawa watakwenda kutumia taaluma, uzoefu na viapo vyao kutekeleza kazi kwa weledi, umakini na uadilifu mkubwa,” amesema Rais Samia.
Amesema,licha ya kutambua uzito wa jukumu hilo, Tume imepewa muda wa miezi mitano kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti rasmi.

Aidha, Rais Samia amewataka Watanzania wote kutoa ushirikiano unaohitajika kwa Tume hiyo ili iweze kutekeleza kazi yake kwa ufanisi bila kuingiliwa.

“Niwasihi sana Watanzania wote kutoa ushirikiano unaohitajika na Tume katika kutekeleza majukumu yao. Tusaidie Tume hii ili iweze kufanya kazi yake na tusiisumbue katika kufanya kazi zake,”amesema Rais Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here