NA DIRAMAKINI
RASILIMALI za maji, hili sio neno geni masikioni mwa wengi katika jamii yetu. Kwa uchache neno rasilimali linasimama kumaanisha kitu chochote chenye thamani na kinachoweza kutumika kufanikisha jambo fulani, iwe fedha,watu,au muda. Ni uwezo unaoweza kutumika kufanikisha mahitaji au lengo.
Kazi ya ukaguzi wa maji chini ya ardhi mara kwa mara ni muhimu kwa usalama wa wateja, pamoja na mazingira. Jukumu la kupima ubora wa maji hayo sharti lifanywe na wataalamu wa rasilimali za maji kwa vifaa vya kisasa. Utafiti uliochapishwa katika Atlasi ya Maji Afrika umeainisha kuwa uendelevu wa maji chini ya ardhi unahitaji uelewa mkubwa wa haidrolojia na maji, kwa usalama wa chakula, uchumi na huduma ya maji kwa sasa na siku zijazo.
Rasilimali za maji, inajumuisha vyanzo vya maji kama mito, maziwa, bahari, chemchemi na maji ya chini ya ardhi, vinavyotumika kwa matumizi ya binadamu, kilimo, viwanda na mazingira.
Hivyo tunapoongea kuhusu masuala ya rasilimali za maji ni bayana kuwa tunagusa moja kwa moja umuhimu wa maji katika majukumu mbalimbali kwa maendeleo ya jamii na uchumi ikiwamo kilimo,mifugo, nishati ya kuzalisha umeme na matumizi ya majumbani na viwandani.
Pia hifadhi ya bioanuai na kudhibiti mmomonyoko wa ardhi katika vyanzo vya maji bila kusahau vyanzo vya maji chini ya ardhi.
Kwa lugha nyepesi, maji chini ya ardhi ni maji yanayopatikana chini ya uso wa ardhi ambayo hujikusanya kwenye nafasi na mwamba wenye uwezo wa kuhifadhi na kupitisha maji unayojulikana kama mwambamaji (aquifer).
Maji chini ya ardhi hayakai eneo moja, hutembea polepole kupitia udongo na miamba na chanzo chake kikuu ikiwa ni mvua ambayo maji yake hujikusanya na kupenya ardhini.
Tafiti za kitaalam za Wizara ya Maji katika kuandaa mipango shirikishi ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji nchini, zinaonesha inakadiriwa kuwa rasilimali za maji zinazopatikana na zinazofaa kwa matumizi mbalimbali nchini ni mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka.
Kiasi hicho kinahusisha maji juu ya ardhi mita za ujazo bilioni 105 na maji chini ya ardhi mita za ujazo bilioni 21 kwa mwaka, kwa mujibu wa Atlasi ya Rasilimali za Maji, Tanzania 2019.
Wizara ya Maji kupitia Idara ya Rasilimali za Maji yenye dhamana ya kushughulikia masuala yote yanayohusu maji juu ya ardhi na maji chini ya ardhi inaratibu suala hili kwa manufaa ya nchi, na wadau wengine nje ya mipaka ya nchi
Ili kukidhi mahitaji ya wananchi hususan maji chini ya ardhi, hili limewezeshwa kikamilifu na serikali ya awamu ya sita kwa kununua seti 25 za mitambo ya kuchimba visima na seti tano (5) za mitambo ya ujenzi wa mabwawa.
Ni jitihada ya kuwatumia wataalam walioajiriwa na Serikali kwa kuwapatia vifaa vya kisasa kufanikisha huduma ya maji katika jamii.
Kazi ya kuchimba maji chini ya ardhi sio “holela”, zipo taratibu mahsusi za kitaalam kabla ya kufanya kazi hiyo.
Jukumu hili linawahitaji wataalam wenye vifaa vya kisasa ilikuweza kupata matokeo yenye ufanisi kuanzia hatua ya utafiti hadi kupatikana kwa maji.
Kabla ya kuchimba kisima au ujenzi wa bwawa, eneo husika lililochaguliwa na jamii hufanyiwa uchunguzi ili kutambua sehemu yenye uwezekano mkubwa wa kupata maji kupitia vifaa vya kisasa vyenye teknolojia kubwa na uwezo wa kuchunguza hali ya udongo na miamba chini ya ardhi bila kuchimba kwanza.
Hatua hii husaidia kutambua, mabadiliko ya tabaka za miamba na maeneo yenye uwezekano mkubwa wa kuwa na maji.
Ipo imani kuwa maji yanayopatikana chini ya ardhi yamechujwa na udongo hivyo ni safi na salama, huu ni mtazamo usio sawa kitaalam.
Taarifa kuhusu tafiti za kihaidrojeolojia na kihaidrometolojia na uzoefu wa kitaalamu imethibitisha upimaji wa wingi na ubora wa maji katika maendeleo na usimamizi wa maji chini ya ardhi ni moja ya hatua muhimu kabisa kabla ya kufanya matumizi yoyote.
Hivyo wadau wote, ikiwamo kampuni zinazojihusha na utafiti na uchimbaji wa maji chini ya ardhi ni lazima kuzingatia utaratibu wa kuwa na nyaraka halali za Sheria, leseni na kukidhi viwango vya kitaalamu ili kulinda rasilimali za maji ambayo ni muhimu kwa maendeleo na usalama wa taifa.
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) hivi karibuni amenukuliwa akiongea na wadau wa maji chini ya ardhi kuwa katika kufanikisha huduma ya maji kwa jamii kwa kushirikiana na serikali ni muhimu kuzingatia taratibu za sheria za ukitaalam na sio kufanya kazi holela kwa kuangalia faida bila kujali mazingira na afya ya jamii katika kupata maji.
Uchimbaji holela wa visima unahatarisha ubora na uendelevu wa rasilimali za maji, hivyo Serikali inaendelea kuimarisha ukaguzi, utoaji wa leseni na matumizi ya teknolojia ya kisasa katika usimamizi wa sekta ya maji, pamoja na kutoa elimu katika jamii kuhusu uchimbaji ambao ni salama.
Alisema utaratibu wa kuchimba maji lazima ufanyike kitaalamu kwa kuzingatia uendelevu wa huduma na utunzaji wa mazingira, ikiwamo miamba inayotunza maji.
Hadi sasa katika eneo la uchimbaji, Idadi ya leseni 45 za kampuni zinazojihusisha na kazi ya kuchimba visima; leseni 45 za wachimbaji na leseni 15 za utafiti wa maji chini ya ardhi zimehuishwa.
Hatua hiyo inafanya jumla ya leseni 93 za kampuni za uchimbaji; leseni 106 za wachimbaji; na leseni 20 za taasisi na makampuni ya utafiti wa maji chini ya ardhi. Vilevile, jumla ya vibali 630 vya kuchimba visima vya maji katika maeneo mbalimbali nchini vimetolewa na kufanya kuwa na jumla ya vibali 4,519 vya kuchimba visima.
Eneo la maji chini ya ardhi linapoongelewa, halikomei ndani ya mipaka ya nchi ya Tanzania peke yake, bali pia linahusu ushirikiano na nchi jirani katika miradi ya usimamizi wa maji chini ya ardhi miongoni mwa nchi hizo ni zile zilizopo katika Kamisheni ya Bonde la mto Nile (Burundi, Rwanda na Uganda).
Tafiti za maji chini ya ardhi zinaonyesha kuwa endapo nchi moja itakuwa na tamaa ya kusukuma maji chini toka chini ya ardhi, itamaliza rasilimali hiyo kwa nchi jirani.
Haidrojia imeweka bayana kuwa miamba inayotunza maji inavuka mipaka ya nchi katika baadhi ya maeneo, hivyo inatumika kunufaisha wananchi katika nchi zaidi ya moja.
Mfano mzuri wa ushirikishwaji ni katika mkoa wa Kagera kupitia mradi wa usimamizi wa maji chini ya ardhi ambao umekamilika kwa gharama ya Dola za Marekani milioni 5,329,452.
Mradi huo umetekelezwa katika Wilaya za Muleba, Bukoba, Misenyi, Karagwe na Kyerwa. Vilevile, kupitia mradi huo Wizara ya Maji imenufaika kwa kupata vifaa vya kisasa vya kupima wingi na ubora wa maji, hivyo kuimarisha upatikanaji wa taarifa sahihi za hali ya mwenendo wa wingi na ubora wa maji chini ya ardhi.
Kuelewa maji chini ya ardhi ni kuelewa maji yanatoka wapi, yanahifadhiwa wapi, yanatiririka vipi, yanapatikanaje, yapo wingi wa kiasi gani, yana ubora gani na yanawezaje kutumika bila kuharibu rasilimali nyingine ili kuweza kutumika kwa kiwango endelevu.
Maji chini ya ardhi yanaweza kuchafuliwa na shughuli zinazofanyika juu ya ardhi ikiwamo shughuli za binadamu kama vile ujenzi usiobora wa vyoo na matanki ya majitaka (septic tanks), taka, mbolea, dawa zinazotumika katika kilimo, mafuta, viwanda na maji machafu, haya yote yanaweza kusababisha uchafu kupenya ardhini na kufika kwenye mwamba ambao maji yanatoka (aquifer) na hatimaye kwenye kisima kinachotumika kutoa huduma yam aji katika jamii.
Hivyo, maji chini ya ardhi inaweza kuonekana kwa macho ni safi lakini kupitia vipimo vya ubora yasiwe salama kwa matumizi ya binadamu.
Kutokana na mwenendo wa kuongezeka kwa mahitaji ya maji kunakotokana na ongezeko la watu, Serikali inaendelea kuwekeza katika utunzaji wa vyanzo vya maji, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha ufanisi katika matumizi ya maji kwa lengo la kuepusha nchi yetu kuwa na uhaba wa maji.
Ambapo hili pia limewekwa katika Dira ya maendeleo ya Taifa 2050. Kutimiza hilo Sekta ya Maji inaenda kwa agenda ‘Wizara ya Maji 1-5-7-5 tuko site kikazi zaidi’ kufikisha miundombinu rasmi ya maji katika idadi ya vijiji 1,575 vilivyosalia ambapo tiyari idadi ya vijiji 10,758 vina majisafi.
Wakati Dunia inakumbwa na misuko misuko mbalimbali ya mazingira, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi yayosababisha pamoja na mengine, kuongezeka kwa joto na kusababisha tabia ya mabadiliko ya maji juu ya ardhi ya mito, maziwa na mabwawa ambapo kiasi cha maji kinapotea kwa mvuke au kuwa na mvua zinazopitiliza.
Maji ni muhimu sana kwa maisha ya viumbe hai pamoja na mazingira. Mabadiliko ya tabianchi yanasababisha athari kubwa katika upatikanaji wa maji.
Bara la Afrika nalo linakabiliwa na mabadiliko hayo ambapo idadi ya watu Milioni 400 wanakosa huduma ya uhakika ya maji, kwa mujibu wa tafiti ya Umoja wa Mataifa.
Hata hivyo, habari njema ni kuwa Afrika imebarikiwa kuwa na maji chini ya ardhi mita za ujazo milioni 0.66, kiasi ambacho ni zaidi ya mara 20 ya maji yote kwa ujumla katika maziwa makuu yanayopatikana barani Afrika.
Maji chini ya ardhi ni mkombozi mkubwa pale eneo linapokumbwa na ukame au upungufu wa maji kwa sababu maji chini ya ardhi yanatoa uhakika wa huduma ya maji kuendela kuwepo, hata hivyo wataalam wa maji, wakiwemo Wahaidrolojia wanalo jukumu la kuhakikisha ni eneo gani muafaka kwa kazi ya kubaini eneo litakalotobolewa na kupatapa maji bila kuhatarisha uendelevu wa miamba inayotunza maji.
Kuvuta maji chini ya ardhi inategema wingi wa maji yaliyopatikana chini na mwamba unayoyatunza.
Uchimbaji wa maji usiokuwa wa kitaalam unatishia kupoteza mimba inayotunza maji kwa asilimia 70 Duniani, pia kutishia baadhi ya makazi katika miji mikubwa kuzama.
Bara la Afrika lina wakazi wapatao milioni 94 katika maeneo ya vijijini ambapo maji chini ya ardhi yanaweza kutumika kutoa huduma bora ya majisafi na salama.
Jarida la MaongeziAfrika katika eneo la utafiti limeonesha kuwa idadi ya watu Milioni 333 wanaishi katika maeneo ambapo maji chini ya ardhi yanaweza kutumika kwa kazi ya kilimo cha umwagiliaji ikiwamo Tanzania.Umoja wa mataifa katika
Hata hivyo, idadi ya watu Milioni 535 wameweka makazi ambapo shughuli wanazofanya zinatishia usalama wa maji chini ya ardhi ambapo maji hayo kabla ya kutumika lazima wataalam wayachunguze kwa kina.
