Tanzania yasaini makubaliano ya miradi ya afya,umeme na gesi

NA DIRAMAKINI

SERIKALI ya Tanzania imesaini makubaliano mbalimbali ya ushirikiano katika sekta za afya, umeme na gesi asilia, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuongeza uwekezaji na kuimarisha miundombinu nchini.
Makubaliano hayo yamesainiwa Agosti 5,2026 wakati wa Mkutano Mkuu wa Wanahisa wa Africa50 na Jukwaa la Miundombinu Afrika unaofanyika jijini Dar es Salaam kwa siku mbili.

Aidha,mkutano huo umefunguliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan ambapo amesema, Bara la Afrika limekuwa na maono na mipango mbalimbali ya maendeleo kwa muda mrefu, lakini sasa kinachohitajika ni utekelezaji wa miradi yenye matokeo yanayoonekana katika maisha ya wananchi.

Rais Dkt.Samia amesema, wananchi hawapimi maendeleo kwa ahadi au matamko, bali kwa uwepo wa miundombinu bora kama barabara, reli, bandari, nishati ya uhakika na mifumo ya kidijitali inayochochea biashara, kuvutia uwekezaji na kuboresha huduma za kijamii.

"Ni wakati wa kugeuza mawazo kuwa miradi, ushirikiano kuwa uwekezaji na fursa za Afrika kuwa ustawi wa watu wetu," amesema.
Hata hivyo,kwa mujibu wa makubaliano hayo, Tanzania itashirikiana na wadau katika kupanua huduma za matibabu ya figo, kuongeza uwekezaji wa sekta binafsi katika miundombinu ya usafirishaji wa umeme, pamoja na kuongeza matumizi ya gesi asilia katika shughuli za viwanda.

Washirika walioshiriki katika makubaliano hayo ni Africa50, Wizara ya Afya, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na TAQA Arabia.

Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwekezaji katika miundombinu muhimu, kuboresha huduma za afya, kuimarisha upatikanaji wa umeme na kukuza matumizi ya gesi asilia katika uzalishaji wa viwandani, hatua inayolenga kuchochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here