TMA yawataka wananchi kupuuza taarifa potofu kuhusu baridi kali kutokana na Aphelion

NA DIRAMAKINI

MAMLAKA ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imekanusha taarifa inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikidai kuwa,Tanzania inatarajiwa kukumbwa na baridi kali isiyo ya kawaida kutokana na tukio la kiasili la Aphelion.
TMA imesema taarifa hiyo inayodai kuwa kuanzia saa 11:00 alfajiri kwa muda wa saa 27 kutatokea tukio la Aphelion litakaloambatana na baridi kali, mafua,kikohozi na matatizo ya kupumua,si sahihi.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa na TMA leo Agosti 9,2026. Mamlaka hiyo imeeleza kuwa,Aphelion ni tukio la kawaida katika mzunguko wa Dunia kwenye mfumo wa Jua, ambapo Dunia hufikia hatua ya kuwa katika umbali mkubwa zaidi kutoka kwenye Jua.

Hata hivyo, TMA imefafanua kuwa tukio hilo lina mchango mdogo sana katika kusababisha mabadiliko ya baridi kutoka msimu mmoja hadi mwingine katika maeneo ya Tanzania, kutokana na nchi kuwa karibu na Ikweta.

Kipupwe cha Juni hadi Agosti

Kwa mujibu wa TMA, kipindi cha Juni hadi Agosti kila mwaka ni majira ya Kipupwe katika maeneo mengi nchini, ambapo mifumo ya hali ya hewa hutawaliwa na hali ya baridi pamoja na upepo mkali.

Mamlaka hiyo imesema, utabiri wa msimu wa Kipupwe uliotolewa Mei 25, 2026 ulionesha kuwa hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi ilitarajiwa katika maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kusini, Nyanda za Juu Kusini Magharibi pamoja na Mkoa wa Singida.

Kwa upande mwingine, hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani ilitarajiwa katika maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini na maeneo ya nchi kavu, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki, Ukanda wa Pwani ya Kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma.

TMA ilitabiri pia kuwa vipindi vya baridi zaidi vilitarajiwa kujitokeza katika mwezi Julai 2026.
Viwango vya joto. Mamlaka hiyo imeeleza kuwa, viwango vya joto la chini vilitarajiwa kutofautiana kulingana na maeneo.

Katika Nyanda za Juu Kusini Magharibi, joto la chini lilitarajiwa kuwa kati ya nyuzi joto 6°C na 21°C, wakati katika Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki lilitarajiwa kuwa kati ya 10°C na 20°C.

Aidha,katika maeneo ya Kanda ya Kusini, joto la chini lilitarajiwa kuwa kati ya 8°C na 22°C, huku maeneo mengine ya nchi yakitarajiwa kuwa na joto la chini kati ya 10°C na 25°C.

TMA imesisitiza kuwa,hali hiyo ni sehemu ya mwenendo wa kawaida wa msimu wa Kipupwe na haihusiani na madai yanayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu Aphelion.

Vilevile, TMA imewakumbusha wananchi kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania Na. 2 ya Mwaka 2019, mamlaka hiyo ndiyo taasisi yenye jukumu na mamlaka ya kutoa taarifa rasmi za utabiri na tahadhari za hali ya hewa kwa umma.

TMA imeonya kuwa kutoa au kusambaza taarifa zisizo rasmi kuhusu utabiri na tahadhari za hali ya hewa ni kosa kisheria kwa mujibu wa vifungu vya 27, 31(5) na 46(1) vya sheria hiyo.

Mamlaka hiyo imewataka wananchi kuwa waangalifu na taarifa zinazochapishwa kwenye mitandao ya kijamii, hasa zinazohusu matukio ya hali ya hewa, na kutumia taarifa zinazotolewa kupitia vyanzo rasmi vya TMA.

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi na kwa wakati, pamoja na kuzuia hofu inayoweza kusababishwa na taarifa zisizo sahihi kuhusu mwenendo wa hali ya hewa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here