Tuendelee kutumia huduma za kielektroniki katika malipo,utoaji wa zawadi na miamala mingine-Gavana Tutuba

NA GODFREY NNKO 

GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba amesema, fedha zilizotolewa kwa maburungutu katika tukio la Katoro mkoani Geita hazijathibitishwa kuwa ni bandia, huku akiwataka wananchi kuachana na utamaduni wa kutoa zawadi za fedha taslimu kwa mtindo huo na badala yake kutumia mifumo ya kisasa ya kifedha.
Ameyasema hayo leo Agosti 4,2026 katika mahojiano maalumu ndani ya kipindi cha Jambo Tanzania kinachorushwa na TBC1, wakati akizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu Benki Kuu ya Tanzania ikiwemo maadhimisho ya miaka 60 ya taasisi hiyo, thamani ya sarafu ya Tanzania, matumizi ya fedha na maendeleo ya mifumo ya kifedha nchini.

“Hata lile la Katoro nililiona, mpaka sasa sijapata taarifa kuwa fedha zile ni feki. Ila itumike njia ya kisasa ya utoaji zawadi, kubeba fedha kuna athari nyingi ikiwemo kuibiwa na kuporwa,"asema Tutuba.

Amesisitiza kuwa,matumizi ya mifumo ya kielektroniki, ikiwemo huduma za benki na mitandao ya simu ni salama zaidi na yanaweza kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza wakati wa kubeba kiasi kikubwa cha fedha taslimu.

Fedha ni tunu ya Taifa

Gavana Tutuba amesema,Benki Kuu ya Tanzania ina jukumu la kuchapisha na kusambaza fedha nchini, hivyo ni wajibu wa taasisi hiyo pamoja na wananchi kuhakikisha fedha hizo zinatunzwa ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Amesema,fedha za Tanzania ni miongoni mwa tunu za Taifa kwa kuwa zina nembo ya Taifa, hivyo wananchi wanapaswa kuzitunza na kuziheshimu kwa matumizi sahihi.

Kwa mujibu wa Gavana Tutuba, fedha zinapochakaa kabla ya muda wake, Serikali hulazimika kutumia gharama nyingine kuzichapisha upya, hali ambayo inaweza kupunguzwa iwapo wananchi watazitumia na kuzihifadhi kwa uangalifu.

Amesema,matumizi ya mifumo ya kielektroniki kupitia benki na mitandao ya simu yanaweza pia kusaidia kupunguza utegemezi wa fedha taslimu na hivyo kupunguza gharama zinazotokana na uchakavu wa noti.

Wakopaji someni masharti ya mikopo

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amewataka wananchi wanaokopa fedha kuhakikisha wanasoma na kuelewa masharti ya mikopo kabla ya kukubali, huku akisisitiza umuhimu wa kuwa na malengo ya wazi ya matumizi ya fedha wanazokopa.

Amesema,Benki Kuu imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kudhibiti kampuni zenye leseni za kutoa huduma za mikopo zinazokiuka sheria na taratibu, ikiwemo kampuni zinazowakandamiza wateja kupitia mikopo inayoweza kuwa na masharti yenye kuwaumiza wakopaji.

Gavana Tutuba amesema hadi sasa BoT imesajili kampuni 1,229 za daraja la pili za huduma za fedha (Microfinance) zinazotoa huduma za mikopo.

Amefafanua kuwa,nyingi ya kampuni hizo zinafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, huku zile chache zinazobainika kukiuka masharti zikichukuliwa hatua, ikiwa ni pamoja na kufungiwa kutoa huduma.

Aidha, amesema BoT hupokea malalamiko kutoka kwa wananchi wanaokopa dhidi ya watoa huduma za mikopo, lakini tathmini ya benki hiyo imeonesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya malalamiko hayo yanahusishwa na wakopaji wenyewe kushindwa kuzingatia masharti ya mikopo.

Pia,amesema baadhi ya wakopaji huingia kwenye mikopo bila kuwa na mpango au malengo ya wazi ya matumizi ya fedha wanazopata.

“Pale unapokopa ni vizuri kuelewa masharti yake, na uweke malengo ya fedha ile unayoipata,”amesema.

Amesisitiza kuwa,wananchi wanapaswa kuwa makini kabla ya kukopa, kuelewa gharama na masharti ya mkopo pamoja na kuhakikisha fedha wanazokopa zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa.

BoT yanunua tani 29 za dhahabu ndani ya miezi 20

Katika hatua nyingine, Gavana Tutuba amesema Benki Kuu imeweka mkakati maalumu wa kununua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wakubwa na wadogo kwa bei shindani zinazozingatia mwenendo wa soko la kimataifa.

Amesema, mkakati huo umeongeza hamasa miongoni mwa wachimbaji kuuza dhahabu yao moja kwa moja kwa Benki Kuu kutokana na BoT kuinunua bila kufanya punguzo lolote.

Kwa mujibu wa Tutuba, hatua hiyo imewezesha Benki Kuu kuvuka kwa kiwango kikubwa lengo lake la awali la kununua tani 20 za dhahabu ndani ya kipindi cha miaka mitatu.

Amesema,badala ya kufikisha tani 20 ndani ya miaka mitatu, BoT imefanikiwa kununua tani 29 za dhahabu katika kipindi cha miezi 20 pekee, hatua inayoonesha kuongezeka kwa ushiriki wa benki hiyo katika soko la dhahabu nchini.

Leseni za Bureau de Change zafikia 202

Gavana Tutuba pia amesema, Serikali imepanua wigo wa utoaji wa leseni kwa wafanyabiashara wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni (Bureau de Change), hatua iliyochangia kuongezeka kwa idadi ya maduka yanayotoa huduma hiyo nchini.

Amesema,hadi sasa Benki Kuu imetoa leseni 202 za maduka ya kubadilisha fedha za kigeni, ambazo zimegawanywa katika matabaka matatu kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma pamoja na usimamizi wa sekta hiyo.

Kwa mujibu wa Tutuba, Tabaka A linahitaji mtaji wa shilingi bilioni moja kwa wawekezaji wa kigeni na shilingi milioni 500 kwa Watanzania.

Tabaka B amesema kuwa,linamhitaji mwombaji kuwa na duka moja lisilo na matawi pamoja na mtaji wa shilingi milioni 200.

Aidha, Tabaka C limetengwa kwa ajili ya maduka ya kubadilisha fedha za kigeni yaliyopo katika hoteli za kitalii.

Amesema,mfumo huo umewekwa kwa kuzingatia mahitaji ya soko na unalenga kuongeza upatikanaji wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni kwa wananchi na wageni, huku ukihakikisha kuwa watoa huduma wanafuata viwango na masharti yaliyowekwa na Benki Kuu.

Aidha,Gavana Tutuba amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendana na mabadiliko ya mifumo ya kifedha kwa kutumia huduma za kielektroniki katika malipo, utoaji wa zawadi na miamala mingine badala ya kutegemea fedha taslimu pekee.

Amesema, hatua hiyo si tu itasaidia kuimarisha usalama wa fedha, bali pia itapunguza gharama za kuchapisha fedha mpya kutokana na uchakavu wa noti, kuongeza ufanisi wa miamala na kuimarisha matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha nchini.

Benki Kuu ya Tanzania imeendelea kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kusimamia sera ya fedha, kudhibiti na kusimamia sekta ya fedha, kuhakikisha upatikanaji wa fedha salama na kuendeleza mifumo bora ya malipo nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here