Tume ya Jaji Lila yaanza kuchunguza wahusika wa ghasia za Uchaguzi Mkuu wa 2025

NA DIRAMAKINI

MWENYEKITI wa Tume ya Uchunguzi wa Kijinai wa Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,Jaji mstaafu wa Mahakama ya Rufani, Shaban Ally Lila amesema,tume hiyo imeanza rasmi kazi ikiwa na hadidu tano za rejea zitakazoongoza uchunguzi wake na kubainisha wigo pamoja na mipaka ya mamlaka yake.
Jaji Lila ameyasema hayo leo Agosti 24,2026 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema, tofauti na uchunguzi wa awali uliolenga kubaini matukio ya ghasia na ukiukwaji wa sheria,tume anayoiongoza imepewa jukumu la kwenda hatua zaidi kwa kuchunguza na kubaini watu waliohusika katika kupanga, kufadhili, kuratibu na kutekeleza matukio hayo.

Kwa mujibu wa Jaji Lila, hadidu hizo tano ndizo msingi wa kazi ya Tume na zitaamua maeneo itakayochunguza pamoja na mipaka ya mamlaka yake katika kutekeleza jukumu hilo.

Akifafanua hadidu hizo, Jaji Lila amesema, hadidu ya kwanza ni kuchunguza na kubaini wahusika wa ghasia, pamoja na kutathmini namna kila mmoja alivyoshiriki katika kupanga, kufadhili, kuratibu au kutekeleza shughuli zilizohusiana na ghasia hizo.

Amesema,eneo hilo la uchunguzi linatokana kwa kiasi kikubwa na matokeo ya Tume iliyotangulia iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Othman Chande, ambayo ilibaini kuwa matukio ya ghasia na fujo yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi hayakuwa matukio ya bahati mbaya bali yalidaiwa kuwa yalipangwa, kuratibiwa, kufadhiliwa na kutekelezwa kwa mpango maalum.

Hadidu ya pili inahusu uchunguzi wa matukio mahsusi yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi, ikiwemo vifo visivyo vya kawaida vya watoto na watu kutoka makundi maalum.

Hadidu ya tatu inalenga kuchunguza taarifa na madai ya watu kupotea katika maeneo mbalimbali yaliyokumbwa na ghasia na uvunjifu wa amani tangu kipindi cha uchaguzi hadi baada ya uchaguzi.

Kwa upande mwingine, hadidu ya nne inahusu kuchunguza madai ya matumizi ya nguvu kupita kiasi, pamoja na kubaini iwapo taratibu, sheria na miongozo iliyowekwa ilizingatiwa katika kukabiliana na ghasia hizo wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.

Hadidu ya tano inaipa Tume nafasi ya kuchunguza suala lolote litakaloonekana kuwa muhimu na linalohusiana na utekelezaji wa majukumu yake.

Jaji Lila amesema, pamoja na kubaini wahusika wa ghasia, Tume itachunguza pia madhara yaliyotokana na matukio hayo, yakiwemo vifo, majeraha na watu waliopotea.
Amesema,uchunguzi huo utazingatia pia mazingira yaliyosababisha madhara hayo na, pale inapowezekana, kubaini wahusika waliohusika.

Akizungumzia matokeo ya Tume iliyotangulia, Jaji Lila amesema Tume iliyoongozwa na Jaji Chande ilibaini vifo vya watu 518 vilivyohusishwa na matukio hayo.

Hata hivyo, amesema Tume hiyo ya awali yenyewe ilionya kuwa idadi hiyo huenda ikawa kubwa zaidi kwa kuwa si waathirika wote waliweza kufikiwa au kupita katika taratibu za utambuzi.

“Tume ya Mheshimiwa Jaji Chande ilibainisha kuwa kulitokea vifo na ikataja kwa mujibu wa uchunguzi wao kwamba walibainisha vifo vya watu 518, lakini pia tume ile ilisema inawezekana idadi ni zaidi ya hapo kwa sababu si wote walipita kwenye utaratibu ambao wangeweza kutambuliwa,” amesema Jaji Lila.

Jaji Lila amesema, Tume anayoiongoza ina majukumu yanayotofautiana na yale ya Tume ya Rais iliyokuwa chini ya Jaji Chande.

Amesema,Tume ya awali ilijikita zaidi katika kuchunguza matukio yaliyotokea, aina ya vurugu, ghasia na uvunjifu wa amani uliojitokeza, wakati Tume mpya imepewa jukumu la kuchunguza kwa kina zaidi nani waliohusika na matukio hayo na nafasi waliyocheza.
“Sisi tumepewa jukumu la kwenda kuangalia wahusika ni kina nani, waliopanga, walioratibu, waliofadhili, waliotekeleza,” amesema.

Ameongeza kuwa,Tume pia itachunguza madhara yaliyotokana na ghasia hizo, ikiwa ni pamoja na watu waliojeruhiwa na waliopoteza maisha, huku ikitathmini aina na kiwango cha nguvu kilichotumika katika kudhibiti ghasia.

“Thamani ya mtu hailinganishwi na kitu kingine chochote,” amesema Jaji Lila.

Tume hiyo, ambayo imeanza kujulikana kama Tume ya Jaji Lila iliundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan na kuzinduliwa rasmi Agosti 7, 2026 ikiwa na jukumu la kuchunguza wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa sheria uliotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Tume hiyo ina makamishna sita, ikiongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Shabani Lila, akiwa Mwenyekiti na Kamishna. Wajumbe wengine wa ndani ni Majaji Wastaafu wa Mahakama Kuu, Jaji Gad Mjemmas, Jaji Awadh Bawazir na Jaji Aishieli Sumari, ambao kwa pamoja wanatarajiwa kutumia uzoefu wao wa muda mrefu katika masuala ya sheria na uchunguzi.

Tume pia imejumuisha makamishna wawili wa kimataifa, Petrus Tileinge Damaseb, Naibu Jaji Mkuu wa Namibia, na Jaji Cheborion Barishaki kutoka Uganda, hatua inayolenga kuongeza uwazi, weledi na mtazamo mpana katika uchunguzi huo.
Imepewa muda wa miezi mitano kutekeleza majukumu yake na kuwasilisha ripoti ya uchunguzi, huku hadidu tano za rejea zikiwa msingi wa kuelekeza mchakato huo.

Kwa kuzingatia hadidu hizo, kazi ya Tume inalenga si tu kuweka wazi kilichotokea wakati na baada ya uchaguzi, bali pia kuchunguza kwa kina mlolongo wa wahusika, madhara yaliyotokea na namna mamlaka mbalimbali zilivyotumia nguvu katika kukabiliana na ghasia hizo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here