NA DIRAMAKINI
KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetoa adhabu mbalimbali kwa klabu, wachezaji na mwamuzi kufuatia matukio yaliyojitokeza katika michezo ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Katika kikao chake kilichofanyika Agosti 21, 2026, Kamati hiyo ilipitia mwenendo wa ligi pamoja na matukio yaliyojitokeza katika mechi kadhaa na kufanya maamuzi kwa mujibu wa kanuni za mashindano.Miongoni mwa klabu zilizopewa adhabu ni Dodoma Jiji, Pamba Jiji, Namungo na Simba SC, huku wachezaji Ibraheem Jabaar wa Simba na Mathew Tegisi wa Singida BS nao wakikumbana na adhabu kutokana na matukio yaliyotokea uwanjani.
Dodoma Jiji yatozwa Shilingi milioni 5
Katika mchezo namba 001 uliowakutanisha Pamba Jiji na Dodoma Jiji ambao ulimalizika kwa sare ya bao 1-1, Klabu ya Dodoma Jiji imetozwa faini ya Shilingi milioni tano.
Faini hiyo imetokana na kitendo cha baadhi ya wachezaji wa klabu hiyo kuonekana wakifanya vitendo vilivyotafsiriwa kuwa vinaashiria imani za kishirikina kuelekea mchezo huo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wakati wa mazoezi wachezaji hao walijikusanya katikati ya uwanja na kutengeneza duara, huku wakionekana kufanya kitendo kilichoashiria kuomba dua. Hata hivyo, mmoja wao alionekana pia akichimbia vitu chini.
TPLB imesema,adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 48:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Pamba Jiji yapewa onyo kali
Katika mchezo huo huo, Pamba Jiji imepewa onyo kali baada ya kuchelewa kuwasili katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, kabla ya mchezo uliochezwa Agosti 14, 2026.
Kwa mujibu wa TPLB, Pamba Jiji ilifika uwanjani saa 6:51 mchana badala ya saa 6:30 mchana, jambo lililoelezwa kuwa ni kinyume na matakwa ya Kanuni ya 17:15 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Onyo hilo limetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 kuhusu Taratibu za Mchezo.
Namungo yaonywa kwa tabia ya Ball Boys
Katika mchezo namba 0010 kati ya Namungo na Geita Gold uliomalizika kwa Namungo kushinda kwa bao 1-0, Klabu ya Namungo imepewa onyo kali kutokana na mwenendo wa vijana waliokuwa wakihusika na kuokota mipira maarufu kama Ball Boys.
TPLB imesema vijana hao walionekana kuficha mipira iliyotoka nje ya uwanja na wakati mwingine kutokwenda kabisa kuichukua.
Kamati imekielezea kitendo hicho kuwa si cha kiungwana wala kuzingatia misingi ya uchezaji wa kiungwana, huku ikizikumbusha klabu zote kuhakikisha zinaheshimu na kuzingatia kanuni zinazotawala mashindano.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
Simba SC yatozwa Shilingi milioni 5 kwa vurugu za mashabiki
Katika mchezo namba 0012, ambao Pamba Jiji ilifungwa bao 2-1 na Simba SC, Klabu ya Simba imetozwa faini ya Sh milioni tano baada ya mashabiki wake kuwarushia chupa waamuzi wakati wa mapumziko.
Tukio hilo, kwa mujibu wa TPLB, lilisababisha waamuzi kushindwa kutumia vyumba vyao vya kubadilishia nguo.
Kamati imesema,adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 48:1 ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Klabu.
Ibraheem Jabaar asimamishwa
Aidha, mchezaji wa Simba SC, Ibraheem Jabaar, ametozwa faini ya Shilingi milioni tano kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji, Abdulkarim Iddy mwenye jezi namba 35.
Mbali na faini hiyo, TPLB imesema adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa mchezaji huyo itaendelea kubaki kama ilivyo.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 42:5(5.2) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mathew Tegisi afungiwa michezo mitatu
Katika mchezo namba 0013 kati ya Kagera Sugar na Singida Black Stars (Singida BS), uliomalizika kwa sare ya bao 1-1, mchezaji wa Singida BS, Mathew Tegisi, amefungiwa michezo mitatu na kutozwa faini ya Sh milioni tano.
Tegisi ameadhibiwa kwa kumpiga kiwiko mchezaji wa Kagera Sugar mwenye jezi namba 12, Salehe Seif.
Kwa mujibu wa TPLB, adhabu hiyo imetolewa chini ya Kanuni ya 42:5(5.2) kuhusu Udhibiti kwa Wachezaji.
Mwamuzi Tatu Malogo apewa onyo
Mwamuzi wa kati wa mchezo huo, Tatu Malogo kutoka Tanga, naye amepewa onyo kali kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni mapungufu ya kiuchezeshaji yaliyosababishwa na kushindwa kutafsiri ipasavyo sheria za mchezo wa mpira wa miguu.
Adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 43:1(1.8) ya Ligi Kuu kuhusu Udhibiti kwa Waamuzi.
TPLB yaweka msisitizo kwenye matumizi ya FVS
Katika taarifa maalum, Kamati imezikumbusha timu zote kuzingatia kikamilifu masharti ya Kanuni ya 20 yanayohusu matumizi ya teknolojia ya Football Video Support System (FVS).
TPLB imefafanua kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 20(4), ni Kocha Mkuu au kiongozi mwingine wa juu katika benchi la ufundi pekee mwenye mamlaka ya kuwasilisha ombi la marejeo ya tukio kupitia mfumo wa FVS.
Ombi hilo linapaswa kuwasilishwa kwa kuwasiliana na Mwamuzi wa Akiba (Fourth Official).
Aidha, Kanuni ya 20(4)4.1 inaelekeza kwamba mchezaji anapoona tukio fulani linahitaji kufanyiwa marejeo kwa kutumia FVS, anatakiwa kuwasiliana kwa ishara na Kocha Mkuu au kiongozi wa benchi la ufundi.
Kiongozi huyo ndiye mwenye jukumu la kuwasilisha ombi rasmi la marejeo kwa Mwamuzi wa Akiba.
Wachezaji waonywa dhidi ya kumshinikiza mwamuzi
Kamati imeweka wazi kuwa mchezaji haruhusiwi kumkabili, kumlalamikia au kumshinikiza mwamuzi moja kwa moja kwa lengo la kutaka tukio fulani lifanyiwe marejeo kupitia mfumo wa FVS.
Mchezaji atakayekiuka masharti hayo ataadhibiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 17:62 ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.
TPLB imesisitiza kuwa, itaendelea kusimamia utekelezaji wa kanuni za ligi na kuchukua hatua dhidi ya klabu, wachezaji au wahusika wengine watakaobainika kukiuka masharti yaliyowekwa.
Hatua hizo, kwa mujibu wa Kamati, zinalenga kuhakikisha Ligi Kuu Tanzania inaendeshwa kwa kuzingatia nidhamu, uadilifu, usalama na misingi ya uchezaji wa kiungwana.
Tags
Adhabu ya Bodi ya Ligi
Bodi ya Ligi Kuu Tanzania
Faini kwa Klabu Ligi Kuu
Habari
Ligi Kuu Tanzania Bara
Michezo