BRUSSELS-Vyombo vikubwa vya habari barani Ulaya vimeendelea kuiunga mkono Tanzania kwa kuunda Tume ya Uchunguzi wa Kijinai ya Matukio ya Ghasia ya Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 inayoongozwa na Jaji mstaafu Shabani Ally Lila.
Tume hiyo imeundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan chini ya mamlaka aliyonayo kwa Sheria ya Tume ya Uchunguzi Sura ya 32.
Aidha,tume hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mapendekezo ya Tume ya Kuchunguza Matukio ya Vurugu za Oktoba 29, 2025 zilizotokea siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani na baada ya hapo.
Taarifa zilizochapishwa na Indegazette.be ya Ubelgiji pamoja na The News Agency, yenye makao yake Brussels zimeangazia uteuzi wa Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Shabani Ally Lila pamoja na ushiriki wa majaji kutoka Tanzania,Namibia na Uganda.
Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan imeonyesha wazi kwamba Tanzania haikwepi kuchunguza yaliyotokea bali imechagua taasisi, sheria na ushahidi kutafuta majibu, hivyo vyombo vya habari Ulaya vimeipa Tume ya Jaji Lila alama ya uaminifu.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, muundo wa tume unaohusisha majaji kutoka nchi mbalimbali umepewa umuhimu katika kuonesha mtazamo mpana wa kisheria katika kushughulikia suala hilo nyeti.
Tume ya Jaji Lila imepewa jukumu la kuchunguza matukio ya jinai yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, pamoja na kubaini watu wanaoweza kuwajibika kwa vitendo hivyo.
Hivyo, hatua hiyo inaweka mkazo katika uchunguzi wa ushahidi, kubaini ukweli wa matukio na, pale inapobainika kuwa kuna wahusika waliokiuka sheria, kuweka msingi wa uwajibikaji kwa mujibu wa sheria.
Muundo huo unatofautiana na Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani Yaliyotokea Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, iliyoongozwa na Jaji mstaafu Othman Chande, ambayo ilikuwa na hadidu za rejea zilizolenga zaidi kuchunguza chanzo, mazingira na madhara ya matukio hayo pamoja na kutoa mapendekezo.
Moja ya mambo yaliyopewa uzito ni uwepo wa majaji kutoka Namibia na Uganda, sambamba na majaji kutoka Tanzania.
Ushiriki wa majaji kutoka nje unatoa mtazamo mpana katika mchakato wa uchunguzi wa suala ambalo limekuwa likijadiliwa kwa kiwango kikubwa ndani na nje ya Tanzania.
Aidha,kuundwa kwa tume hiyo kunaweka suala la matukio ya vurugu za uchaguzi katika mchakato rasmi wa uchunguzi unaoongozwa na majaji.
Kwa mtazamo huo, hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa ushahidi na uchunguzi wa kisheria kubaini kilichotokea, watu waliohusika na kiwango cha uwajibikaji wa kila mhusika, badala ya suala hilo kubaki katika eneo la madai na mijadala ya kisiasa pekee.
Tume hiyo sasa ina jukumu la kutumia mamlaka iliyopewa kuchunguza taarifa, ushahidi na nyaraka mbalimbali zinazoweza kusaidia kufikia ukweli kuhusu matukio hayo.
Uangalizi wa vyombo vya habari vya Ulaya unaifanya kazi ya Tume ya Jaji Lila kuwa miongoni mwa hatua zinazofuatiliwa katika mjadala mpana kuhusu namna Tanzania inavyoshughulikia matukio yaliyotokea baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025.
Mbali na Mwenyekiti wake, Shabani Ally Lila, tume hiyo inaundwa na majaji wastaafu Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Pia kuna majaji wawili wakuu kutoka nje ya Tanzania: Naibu Jaji Mkuu wa Namibia, Petrus Tileinge Damaseb, na Jaji Cheborion Barishaki wa Mahakama ya Rufani ya Uganda.


