DODOMA-Watumishi wa Wizara ya Ujenzi wametembelea na kujionea maendeleo ya utekelezaji wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato jijini Dodoma, ambapo mradi huo umefikia hatua za mwisho za kukamilika.
Ujenzi wa uwanja huo, unaotekelezwa katika eneo lenye ukubwa wa kilomita 10, unafanywa na kampuni za Beijing Construction Engineering Group (BCEG) kwa kushirikiana na Sinohydro Corporation Limited kutoka China.
Mradi huo unatekelezwa na Serikali kwa kushirikiana na ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ukiwa na lengo la kuongeza uwezo wa usafiri wa anga na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Jiji la Dodoma na maeneo mengine nchini.
Katika ziara hiyo iliyofanyika Agosti 14, 2026, watumishi hao walikagua hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi na kujionea kazi zilizofanyika kuelekea kukamilika kwa ujenzi wa uwanja huo wa kimataifa.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato ni miongoni mwa miradi muhimu ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kuboresha miundombinu ya usafiri wa anga na kuiwezesha Dodoma kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi na usafirishaji.
Tags
Dodoma City
Habari
Sekta ya Uchukuzi
Uwanja wa Ndege Msalato
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Msalato




