ARUSHA-Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo Nchini (STPU) kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 12 waliokuwa wakisafirisha kwa njia za magendo jumla ya mifugo 321 kuelekea nchi jirani.
Akizungumza Julai 31,2026 Kamanda wa STPU, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Simon Pasua amesema,operesheni hiyo imefanyika kupitia doria ya pamoja iliyolenga kudhibiti uhalifu unaohusisha wizi na usafirishaji wa mifugo kwa njia zisizo halali.
Kwa mujibu wa Kamanda Pasua, watuhumiwa wanane walikamatwa Julai 30, 2026 katika Kijiji na Kata ya Losoito Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha wakiwa na jumla ya mbuzi na kondoo 163.
Amesema kuwa,katika kuendeleza operesheni hiyo Julai 31,2026, polisi waliwakamata watuhumiwa wawili katika Kijiji cha Soitsambu, Wilaya ya Ngorongoro, wakiwa na mbuzi na kondoo 133.
Aidha, watuhumiwa wengine wawili walikamatwa katika Kijiji cha Posmoru wilayani humo wakiwa na ng’ombe 25, ambao pia walikuwa wakisafirishwa kuelekea nchi jirani kwa njia za magendo.
Kwa ujumla, operesheni hiyo imewezesha kukamatwa kwa watuhumiwa hao 12 pamoja na mifugo 321, ikiwa ni mbuzi, kondoo na ng’ombe waliokuwa wakitoroshwa nje ya nchi kinyume cha taratibu.
Kamanda Pasua amesema,uchunguzi zaidi unaendelea ili kubaini mtandao mzima unaohusika na usafirishaji huo, huku hatua za kisheria zikitarajiwa kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa baada ya kukamilika kwa taratibu za uchunguzi.
Amewataka wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo nchini kuacha kujihusisha na vitendo vya kutorosha mifugo nje ya nchi kwa kukwepa kulipa ushuru na kufuata taratibu za kisheria, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vina athari kwa mapato ya Serikali.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi, hususan wanaoishi katika maeneo ya mipakani, kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa kuhusu viashiria vya uhalifu wa mifugo, ikiwemo usafirishaji wa mifugo kwa njia za magendo.
Amesema,ushirikiano huo ni muhimu katika kuzuia vitendo vinavyoweza kulinyima Taifa mapato yanayostahili kutokana na biashara halali ya mifugo, pamoja na kuchangia katika ukiukwaji wa taratibu za ustawi na haki za wanyama.



