NA GODFREY NNKO
SERIKALI imetambua na kupongeza mchango wa wadau mbalimbali katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya nchini, ikiwemo Mfuko wa Msaada wa Matibabu wa Muslimah (Muslimah Medical Support Fund-MMSF) unaowezesha watoto kutoka familia zenye kipato duni kupata bima ya afya na elimu kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
Akizungumza leo Agosti 1, 2026 jijini Dar es Salaam, aliyewahi kuwa Afisa Mwandamizi wa Serikali na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Morogoro (MUM), Mwantumu Malale kwa niaba ya Kaimu Waziri wa Afya Zanzibar, Dkt.Saada Mkuya amesema,Serikali inathamini juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuwasaidia watoto wenye mahitaji ya kiafya.
Malale alikuwa akizungumza katika kongamano la mwaka la MMSF, lililowakutanisha wadau wa afya kujadili masuala mbalimbali ikiwemo afya ya akili na ukomo wa hedhi, pamoja na kuhamasisha jamii kushirikiana na Serikali kuhakikisha watoto wenye uhitaji wanapata huduma stahiki za matibabu.
Amesema,Serikali pekee haiwezi kumudu kutoa huduma zote za afya kwa wananchi bila ushirikiano wa wadau, hivyo mchango wa mashirika,wafanyabiashara, watu binafsi na taasisi kama MMSF ni muhimu katika kuongeza wigo wa huduma kwa jamii.
“Serikali peke yake haiwezi, lazima tuungane mashirika, wafanyabiashara, watu binafsi na taasisi kama hizi. Jamii ni yetu sote,” amesema.
Amesema,amevutiwa na kazi inayofanywa na madaktari wanawake kupitia MMSF, hasa juhudi zao za kuwawezesha watoto wadogo wenye mahitaji ya kiafya ambao, kutokana na hali za familia zao, hawana uwezo au fursa ya kugharamia huduma hizo.
Kwa mujibu wa Malale, jitihada za kuwasaidia watoto hao ni huduma muhimu kwa jamii na zinaendana pia na misingi ya mafundisho ya dini mbalimbali yanayohimiza watu kusaidiana.
Afya ya akili bado haijaeleweka vya kutosha
Akizungumzia mada ya afya ya akili iliyojadiliwa katika kongamano hilo, Malale amesema suala hilo bado halijaeleweka vya kutosha katika jamii, hali inayosababisha baadhi ya watu wenye changamoto za afya ya akili kutazamwa kwa mtazamo hasi.
Amesema,wakati mwingine mtu anayekabiliwa na changamoto hizo hutafsiriwa vibaya na jamii, akihusishwa na ukosefu wa imani au makosa mengine, badala ya kupewa uelewa na msaada unaohitajika.
Kwa msingi huo, amesema elimu kuhusu afya ya akili inapaswa kutolewa kwa upana na kwa mwendelezo, ili jamii iweze kuelewa sababu za changamoto hizo, namna ya kuzitambua, namna ya kuzuia baadhi yake na jinsi ya kuwasaidia watu wanaokabiliwa nazo.
Amesisitiza kuwa,changamoto ya afya ya akili ya mtu mmoja ni changamoto inayoweza kuathiri familia na jamii nzima.
Ametolea mfano mama anayekabiliwa na changamoto ya afya ya akili, akisema hali hiyo inaweza kuathiri uwezo wake wa kulea familia na kutekeleza majukumu yake ya kila siku.
“Ni jambo la muhimu na ni vema suala la afya ya akili lizungumzwe zaidi ili watu waweze kulielewa, waweze kuwahurumia na kulishughulikia, hasa kwa hao wenye matatizo,”amesema.
MMSF yatoa bima kwa watoto zaidi ya 850
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Muslimah Medical Support Fund (MMSF), Dkt.Asha Mahita amesema, taasisi hiyo ilianzishwa na madaktari wanawake kwa lengo la kuwasaidia watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 kupata bima ya afya.
Amesema,mpango huo ulianza mwaka 2020, awali kupitia makundi ya WhatsApp, huku dhamira ikiwa ni kutoa msaada kama sehemu ya sadaka na kuchangia juhudi za kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za afya.
Kwa mujibu wa Dkt.Mahita, tangu kuanzishwa kwake, MMSF imefanikiwa kuwakatia bima ya afya watoto zaidi ya 850, huku pia ikiwa imesaidia kugharamia matibabu ya watoto zaidi ya 150 ambao hawakutumia bima ya afya.
Amesema, taasisi hiyo imejiwekea utaratibu wa kuchangia kila mwezi, ikiwa na lengo la kuwasaidia angalau watoto 100 kila mwaka, ingawa mahitaji yaliyopo katika jamii ni makubwa zaidi.
Mtoto asiyeumwa pia anahitaji bima
Dkt.Mahita amesema, kuna umuhimu wa jamii kuelewa kwamba bima ya afya haipaswi kutolewa kwa mtoto baada ya kuugua pekee, bali inapaswa kupatikana mapema ili mtoto awe na uhakika wa huduma anapohitaji matibabu.
Amesema, kuwakatia watoto walio na afya njema bima ni sehemu ya kuimarisha mfumo wa bima, kwa sababu mfuko wa bima hauwezi kuwa endelevu endapo utawahudumia watu wanaougua pekee.
“Hauwezi kumkatia bima ya afya mtoto ambaye anaumwa tu, kwani mfuko wa bima utakufa. Tunawakatia bima ya afya watoto ambao pia ni wazima, ili awe na bima yake ya afya,” amesema.
Amesema, gharama za bima ya afya ni kubwa na Serikali haiwezi kubeba mzigo wote peke yake, hivyo ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha watoto wanaoishi katika mazingira magumu wanapata kinga ya kiafya kupitia bima.
MMSF yataka kuongeza idadi ya watoto wanaosaidiwa
Dkt.Mahita amesema,kutokana na ukubwa wa mahitaji yaliyopo, MMSF inalenga kuongeza idadi ya watoto wanaopatiwa bima ya afya na kufikia zaidi ya 1,000 kwa mwaka.
Amesema,juhudi zinazofanywa na taasisi hiyo bado ni sehemu ndogo ikilinganishwa na ukubwa wa mahitaji yaliyopo nchini, hivyo ametoa wito kwa wadau zaidi kujitokeza na kushirikiana katika kuwasaidia watoto kutoka familia zenye changamoto za kiuchumi.
Amesema,kongamano hilo pia lililenga kuwapa madaktari wanawake na washiriki wengine elimu kuhusu afya ya akili na ukomo wa hedhi, sambamba na kuhamasisha jamii kuchangia upatikanaji wa bima ya afya kwa watoto wenye uhitaji.
Kwa ujumla, kongamano hilo limeibua umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wataalamu wa afya, taasisi za kijamii na wananchi katika kupanua wigo wa huduma za afya, hususan kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu.
Juhudi za MMSF zinaendelea kuonesha kwamba jukumu la kulinda afya ya jamii ni la pamoja, huku uwekezaji katika bima ya afya kwa watoto ukiwa hatua muhimu ya kuzuia familia kuingia katika mzigo mkubwa wa gharama za matibabu pindi watoto wanapougua.





