DODOMA-Watumishi wa Wizara ya Fedha, wameshauriwa kufanya mazoezi na kufuata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuendelea kuwa na uwezo wa kutekeleza majukumu ya Serikali na kukuza uchumi wa nchi.
Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Wizara ya Fedha, Bw. Lusius Mwenda, wakati wa kikao maalum na Madaktari kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road, baada ya madaktari hao kukamilisha zoezi la utoaji wa elimu kuhusu saratani pamoja na vipimo vya uchunguzi wa awali wa saratani kwa watumishi wa Wizara ya Fedha, jijini Dodoma.Alisema kuwa Uongozi wa Wizara ya Fedha, unafahamu umuhimu wa watumishi kuwa na afya njema katika utekelezaji wa majukumu yake ili kuyafikia malengo yaliyowekwa kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, huku akiwasihi wataalamu hao wa afya kuendelea kutoa elimu kuhusu magongwa ya saratani kwa Wizara hiyo na wananchi kwa ujumla ili kuongeza uelewa na kujenga jamii yenye afya na uwezo wa kuongeza kipato na kukuza uchumi wa nchi.
‘’Tunawashukuru sana na salamu kwa Uongozi, naamini hata ukiwa na watu wa kutosha lakini hawana afya uwezekano wa kutekeleza majukumu ya msingi ya taasisi ipasavyo ni mdogo, lakini ambacho tunaomba kila baada ya miezi sita mkipata nafasi pengine mje kutoa elimu na huduma nyingine za afya ikiwemo vipimo kwa watumishi wetu,’’ alisema Bw. Mwenda.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga, Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Crispin Kahesa aliupongeza Uongozi wa Wizara ya Fedha na watumishi wake kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu kuhusu saratani pamoja kufanya vipimo vya uchunguzi wa awali wa saratani huku akiwasihi watumishi hao kufuata maelekezo na elimu waliyopata kuhusu ugonjwa huo na magonjwa mengine na kujenga mazoea ya kupima afya zao.
‘’Zoezi letu hili limeenda vizuri sana, shukrani sana kwa uongozi wa Wizara ya Fedha, kwa ushirikiano ambao wametupa na watumishi wameuonesha wakati wote, kwa kipindi hiki tumeweza kuwahudumia zaidi ya watumishi 300,’’ alisema Dkt. Kahesa.
Alisema, utambuzi wa saratani katika hatua za awali unaongeza nafasi ya mafanikio ya matibabu, hivyo jamii inapaswa kujenga utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya mara mara na kuchukua hatua za mapema katika kuzuia na kukabiliana na ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa, zoezi la kutoa elimu na kufanya vipimo vya awali kwa watumishi wa Wizara ya Fedha ni sehemu ya jitihada za kuimarisha uelewa wa watumishi na jamii kwa ujumla kuhusu afya na kuwahamasisha kuchukua hatua za mapema katika kuzuia na kukabiliana na saratani.



