Waziri wa Fedha na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) waangazia ushirikiano wa maendeleo

DAR-Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb) amekutana na kufanya mazungumzo na Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) nchini Tanzania, Bi. Susan Namondo katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, ambapo wamejadili namna ya kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Umoja wa Mataifa katika utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo vya Taifa.
Mazungumzo hayo yamelenga kuongeza ufanisi wa ushirikiano wa kimaendeleo katika kipindi ambacho Serikali inaendelea kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 pamoja na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV).

Katika mazungumzo hayo, pande hizo zimekubaliana kuendelea kushirikiana kwa kuzingatia Mpango wa Ushirikiano wa Umoja wa Mataifa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (United Nations Sustainable Development Cooperation Framework–UNSDCF), ambao umehuishwa na kuongeza muda wa utekelezaji hadi Juni 2028, kutoka muda wa awali wa Juni 2027.

Mfumo huo unaweka msingi wa ushirikiano wa kimkakati kati ya Serikali na mashirika ya Umoja wa Mataifa katika kusaidia utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo, hususan katika maeneo yanayolenga kuongeza fursa za kiuchumi, kuboresha huduma kwa wananchi na kuimarisha uwezo wa Taifa wa kufikia malengo ya maendeleo ya muda mrefu.

Aidha, walijadili kuendelea kwa ushirikiano katika kuendeleza upatikanaji wa vyanzo bunifu vya fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ikiwemo kusaidia Halmashauri, Serikali za Mitaa na taasisi za umma kupata fursa ya kutumia masoko ya mitaji kupitia utoaji wa hatifungani (bonds).
Katika eneo hilo, Umoja wa Mataifa umekuwa na mchango katika kuwezesha hatua mbalimbali zilizosaidia utoaji wa Hatifungani ya Kijani ya Tanga UWASA mwaka 2024, hatua iliyosaidia kuonyesha uwezekano wa kutumia ubunifu wa kifedha katika kugharamia miradi yenye manufaa kwa wananchi na kuchochea uwekezaji endelevu.

Pia, mazungumzo hayo yameangazia umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa Sekta Binafsi katika ngazi mbalimbali, kuanzia Halmashauri, Wilaya hadi Mikoa, ili kuongeza uwezo wa Taifa wa kupata rasilimali fedha zinazohitajika kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 na mipango yake ya utekelezaji.

Serikali inalenga Sekta Binafsi kuchangia takribani asilimia 70 ya mahitaji ya rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Dira hiyo na Mipango ya Maendeleo ya Miaka Mitano, kuanzia na FYDP IV ulioanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/27. 

Katika kufanikisha azma hiyo, Serikali na Umoja wa Mataifa wameona umuhimu wa kujenga uwezo wa wadau wa ndani na kuweka mazingira yatakayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika uwekezaji na utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Vilevile, wamejadili kuendelea kwa majadiliano ya kimkakati kati ya Serikali na Washirika wa Maendeleo (Strategic Dialogues), ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uratibu wa ushirikiano wa maendeleo na kuhakikisha rasilimali na utaalamu unaopatikana kutoka kwa washirika hao vinaelekezwa katika maeneo yenye kipaumbele kwa Taifa.
Katika hatua hiyo, maandalizi ya Mkutano wa Kilele wa Majadiliano ya Kimkakati (High-Level Strategic Dialogue) unaotarajiwa kufanyika Novemba 2026 yanaendelea.

Aidha, pande hizo zimepata fursa ya kujadili maandalizi ya mpango wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kuhamia Makao Makuu ya Nchi jijini Dodoma, hatua inayoratibiwa kwa pamoja na Wizara ya Fedha na Ofisi ya Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uratibu na ufanisi wa shughuli za Umoja wa Mataifa nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Know matter how large or small your business is, advertising here